MAONI YA MHARIRI: Ushindi wa MwanaFA, AY uchochee haki kwa wasanii

Muktasari:

Miaka kadhaa iliyopita, wanamuziki hao vijana Hamisi Mwinjuma (MwanaFA) na Ambwene Yesaya (AY), walifungua kesi ya madai katika Mahakama ya Ilala mkoani Dar es Salaam wakiituhumu kampuni hiyo kutumia nyimbo zao kama sauti za miito ya simu kwa wateja pasipo makubaliano wala ridhaa yao, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Baada ya muda mrefu wa mvutano wa kisheria, hatimaye Mahakama Kuu ya Tanzania imeiamuru kampuni ya Mawasiliano ya Mic Tanzania Limited maarufu kwa jina la Tigo, kuwalipa wasanii wawili wa muziki wa kizazi kipya.

Miaka kadhaa iliyopita, wanamuziki hao vijana Hamisi Mwinjuma (MwanaFA) na Ambwene Yesaya (AY), walifungua kesi ya madai katika Mahakama ya Ilala mkoani Dar es Salaam wakiituhumu kampuni hiyo kutumia nyimbo zao kama sauti za miito ya simu kwa wateja pasipo makubaliano wala ridhaa yao, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Nyimbo zilizotumika katika miito hiyo ni Usije Mjini na Dakika Moja.

Tigo haikuridhika na hukumu ya awali iliyotolewa na Mahakama ya Ilala Aprili 11, 2016 ya kutakiwa kuwalipa wanamuziki hao maarufu nchini kiasi cha Sh2.18 bilioni.

Baada ya kukata rufani na kesi hiyo kusikilizwa katika Mahakama Kuu Dar es Salaam, bahati ya mtende imewaangukia MwanaFA na AY; sasa wanatakiwa kulipwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kama matunda ya kazi waliyoitolea jasho wakiwa wasanii.

Hukumu ya kesi hii imetugusa tukiwa wadau muhimu wa sanaa na wasanii nchini.

Hii ni kada ya watu ambao kwa muda mrefu imekuwa ikilalamika kuwa pamoja na kazi kubwa inayoifanya ikiwamo ubunifu, baadhi ya watu wamekuwa ama wakiwapunja au kuwadhulumu haki zao.

Siyo kwenye muziki pekee, wasanii kwa ujumla wao, wanasema hawaoni matunda ya kazi wanazofanya. Pamoja na kujituma kwao kwa kiwango kikubwa, jasho lao linapotea katika mikono ya watu wachache wanaotumia kazi zao kujinufaisha.

Kwa wasanii kama wa muziki, ukiondoa kazi zao kutumika kama miito ya simu kama ilivyotokea katika sakata hili la Tigo, kilio chao kikubwa ni kazi zao kutumiwa na vyombo vya habari kama vituo vya redio na televisheni pasipo ridhaa yao na hata panapokuwa na ridhaa, aghalabu wanalaliwa kimalipo au hata kudhulumiwa.

Wakati MwanaFA na AY wakimaliza safari yao ya miaka zaidi ya minne kupambana kisheria na Tigo, bado wasanii nchini wana vita isiyokoma na watu kama vile wasambazaji, mapromota, wafadhili na hata mameneja wa wasanii hao.

Pamoja na kuwapo kwa sheria za Hakimiliki na Hakishiriki na hata vyombo vya kusimamia haki za kisanii, tunafikiri upo udhaifu mahala unaosababisha wasanii kudai kuwa wanadhulumiwa. Ni wakati sasa kwa vyombo husika, sio tu kushupalia wajibu wa wasanii lakini pia kuwa mstari wa mbele kusimamia na kulinda haki na masilahi ya wasanii.

Vijana wanapoamua kuwa wabunifu iwe katika sanaa au nyanja nyingine zozote, wanatarajia kuona matunda yao. Huko ndiko kwenye ajira zao hasa katika wakati huu ambao ajira rasmi nchini ni suala adimu kwa vijana wengi.

Tumetaja udhaifu kwa vyombo husika, lakini wasanii nao wanapaswa kuamka na kutambua kuwa nchi ina sheria kamili kuhusu hakimiliki.

Wafanye sanaa lakini wasiifanye ‘kisanii’ kwa sababu huko ni kujirudisha nyuma. Msanii makini ni yule anayejua wajibu na haki zake. Ukijua haki zako, hutokubali kufanya kazi na watu kiholela pasipo kuwa na mikataba wala maridhiano ya kisheria.