Picha na Mtandao wa Crafthubs.com 

Muktasari:

Iwe umeanza kazi hivi karibuni au upo katika ajira kwa muda mrefu, kumbuka unaweza kupata mafanikio katika kazi unayofanya.

Ni ndoto ya kila aliyeajiriwa kupata mafanikio katika kazi anayofanya.

Iwe umeanza kazi hivi karibuni au upo katika ajira kwa muda mrefu, kumbuka unaweza kupata mafanikio katika kazi unayofanya.

Dhana nzima ya mafanikio katika muktadha huu simaanishi kuwa tajiri au kupata cheo kikubwa sana katika kampuni.

Mafanikio ninayoyazungumzia yamejikita katika mawanda kama vile kuwa na uwezo wa kuifanya kazi yako vizuri na kwa ufanisi, kujihisi kuwa umetimiza na kukamilisha malengo na majukumu yako kazini, kuboresha thamani yako katika soko la ajira na hivyo kuwa na uwezo wa kunufaika kiuchumi, pamoja na kutambulika na kuheshimiwa na bosi wako na wafanyakazi wenzako.

Haya ni baadhi tu ya mafanikio katika ajira. Ikumbukwe kuwa mafanikio kazini si kitu rahisi ambacho kila mtu anaweza kukipata.

Kuna siri nyingi za kuyafikia mafanikio katika ajira. Baadhi ya siri hizo ni kama zifuatazo:

Moja, jitihada na bidii kazini ni ufunguo wa mafanikio kazini. Watu wenye kupenda mafanikio daima huwa na tabia za kufanya mambo ambayo daima watu wavivu hawapendi kuyafanya.

Katika zama tulizo nazo imekuwa ni vigumu kupata wafanyakazi waaminifu na wenye kujituma. Wengi wamekuwa ni watu wa kutafuta fursa ziwe nzuri au mbaya za kujinufaisha binafsi.

Katika mazingira kama haya ili ufanikiwe inakubidi ujipambanue kama mpambanaji usiyekubali kushindwa. Tekeleza majukumu yako kwa viwango vya juu na daima pigania kuwa wa kwanza kwa ufanisi.

Katika kuyafanya haya unaweza kujijengea maadui kazini kwani baadhi ya wafanyakazi wanaweza kukuona unajipendekeza au una kiherehere cha kazi.

Tambua kuwa upo ofisini kwa faida yako na ya mwajiri, kwa hiyo maneno ya mtu yasikupe presha. Hata hivyo, waheshimu wafanyakazi wenzako, pokea ushauri wao na msaidiane katika kazi zenu za kila siku.

Usijisifu kuhusu utendaji wako bali waache watu watambue na wayaeleze mafanikio yako kazini.

Tabia njema ni moja ya siri kubwa za mafanikio kazini. Ukiwa na tabia mbaya hata kama ni mchapakazi kiasi gani, hakuna mwajiri atakayeridhika na wewe. Kiburi, dharau na kujifanya unajua kila kitu vinaweza kukuharibia maisha yako ya ajira.

Kuna wafanyakazi ambao siku zote hulalamika tu kana kwamba hawajawahi kutendewa jema hata moja na waajiri wao!

Kama una malalamiko yanayokwaza utendaji wako kazini, yafikishe mahali husika ili yatafutiwe ufumbuzi badala ya kuendekeza majungu.

Wafanyakazi wenye ufanisi daima hufanya mambo mawili: hufanya kazi zao vizuri na huziwekea vipaumbele. Usifanye tu kazi bali jitahidi uifanye kazi yako vizuri na kwa weledi.

Kazi bora itatambuliwa tu kwani itajipambanua na zile zilizofanywa chini ya kiwango. Acha kazi iongee. Fanya kazi kwa kufuata kanuni na siyo kwa njia za mkato zinazoweza kukugharimu.

Tambua kuwa mteja ni mtu muhimu sana kwa uhai wa kampuni au taasisi. Bila mteja hakuna biashara. Wafanye wateja wajihisi kuwa unafurahi kuwahudumia.

Ninaposema wateja hapa ni kila unayemhudumia katika utekelezaji wa majukumu yako kazini. Dhana ya mteja haishii kwa wafanyabiashara pekee.

Tafuta mbinu ambazo zitawafanya wateja waridhike na huduma yako. Wateja ni watu muhimu sana kwani wanaweza kuyatangaza mafanikio yako mbali na eneo lako la kazi.

Unatakiwa kuwajali wateja kama ni watu muhimu sana na hawa ndio watakaopeperusha bendera ya mafanikio yako.

Usiogope kufanya zaidi ya kile ulichopangiwa. Kama unaweza kufanya na ziada kwa manufaa ya ofisi na wafanyakazi wenzako fanya badala ya kutekeleza yale majukumu machache uliyopangiwa.

Unapoajiriwa unakuwa sehemu ya kampuni, jitahidi uwe mwanafamilia bora badala ya kuwa mnafiki unayeisimulia vibaya ofisi, kwa kuwa tu matakwa yako fulani hayakamilishwa.

Kwa nini ubaki kuwa mnafiki katika ofisi unayodhani haikujali? Tafuta njia ya kutoka hapo na kwenda unapoona kuna masilahi zaidi.