KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Barua ya kuomba kazi na sanduku la Posta

Muktasari:

Mmoja wa wahariri niliyetangulia kueleza swali hili alikaa kimya kwa sekunde kadhaa huku amenikodolea macho na hatimaye kuangua kicheko kilichoandamana na kuhema, huku ameshika tumbo kana kwamba linataka kudondoka.

Jumatatu wiki hii nilipokea swali. Hili hapa: “Wewe ndiye uliandika makala kuhusu jinsi ya kuandika barua ya kuomba kazi? Kama ni wewe, niambie hizo namba za Posta ninazipata wapi au ninabuni za kwangu?”

Mmoja wa wahariri niliyetangulia kueleza swali hili alikaa kimya kwa sekunde kadhaa huku amenikodolea macho na hatimaye kuangua kicheko kilichoandamana na kuhema, huku ameshika tumbo kana kwamba linataka kudondoka.

Alipotulia alisema, “…acha mizaha. Kuna kitu kama hicho? Mbona makala zako zitafukua hata wa pangoni.” Nilimhakikishia kwa sauti ya aliyeuliza swali lakini aliendelea kutikisa kichwa na kusema, “…simaini.”

Tangu nilipoandika makala mbili kuhusu jinsi ya kuandika barua ya kuomba kazi, miezi minne iliyopita, nimepokea maoni kutoka kwa wasomaji 53. Watano walikosoa palipoandikwa tarehe – upande wa anwani ya anayeomba kazi. Watatu walisema hakuna haja ya kujua kuandika barua kwa njia hiyo hivi sasa kwani “kila kitu ni mtandao.” Hawakutoa maelezo zaidi.

Wasomaji sita walisema makala za aina hii ziwe zinaandikwa mara kwa mara kwa maelezo kuwa zinatoa funzo kwa wale ambao hawakupata walichoita elimu ya kuandika barua. Waliobaki walipongeza tu kwa uamuzi wa kufundisha wasiojua.

Nilitaka kujua zaidi juu ya aliyeuliza swali. Niliuliza: Umekwenda shule? Akajibu: Ndiyo. Nikauliza: Hadi darasa la ngapi? Akajibu: Fomu Fo (hicho ni kidato cha nne). Nikauliza: Hamkufundishwa jinsi ya kuandika barua? Akajibu: Mimi nataka kujua hizo namba zinatoka wapi.

Nilipomuuliza iwapo alishaona watu wanakwenda Posta kuchukua barua na kama alishakuwa na shauku ya kujua wamepataje namba; muulizaji alijibu, “…mimi huwa ninaona wanakwenda lakini huwa hawatuambii wanazipataje.”

“Nataka kujua kama ninaandika barua, hizo namba ninaweka za rafiki yangu au mwajiri wangu au ninabuni zangu na kuweka. Mimi nataka hilo,” alinisisitizia. Hapo ndipo niligundua kuwa kuna tatizo na hakukuwa na sababu ya kuendelea kumuuliza maswali (ninahifadhi namba yake ya simu).

Nilianza kukumbuka jinsi nilivyopata Sanduku la Posta 71775 Dar es Salaam, Posta ya Zamani, kona ya Barabara ya Sokoine na Mkwepu.

Ilikuwa hivi. Nikiwa mwajiriwa barua zangu zote zilikuwa zikipitia kwenye sanduku la Posta la mwajiri wangu. Nilipohama kutoka mwajiri mmoja kwenda kwa mwingine, utaratibu uliendelea kuwa huohuo.

Lakini ninafahamu kuwa marafiki zangu walikuwa na masanduku ya barua na wale ambao hawakuwa nayo walipitisha barua au vifurushi vyao katika masanduku ya marafiki au ndugu zao. Nilikuwa nimetamani kuwa na sanduku binafsi la Posta. Siku moja nilipoteremka kwenye kituo cha mabasi cha Posta ya Zamani, nikajiambia: Kwa nini nisiingie pale Posta na kuuliza iwapo kuna masanduku ambayo hawajagawa kwa wateja.

Nilikuwa ninajua, tangu nikiwa shuleni, kwamba masanduku ya posta hupatikana Posta na namba za masanduku ya posta hupatikana kwa wanaotoa masanduku.

Niliingia posta. Nikaenda moja kwa moja eneo la Maulizo. Nikauliza niliyemkuta pale iwapo ninaweza kupata sanduku la posta. Akanielekeza kwa aliyemwita “muhusika” – mwanamme wa umri upatao miaka 30 hivi.

Ni hapa nilipoelezwa kuwa wakati huo hakukuwa na masanduku ambayo hayajagawiwa. Nikaelekezwa kuandika barua ya maombi ya sanduku la posta, kuipeleka pale ofisini na kusubiri hadi nitakapoarifiwa; au niwe ninakwenda kuuliza iwapo tayari sanduku limepatikana.

Haikuchukua mwezi mmoja. Nilipopita pale kuulizia, nikaambiwa kuwa tayari kuna sanduku. Nikapewa S.L.P 71775. Nikakabidhiwa funguo. Nikaambiwa kulipa gharama fulani, sikumbuki kiasi gani lakini hazikuwa zaidi ya Sh. 5,000. Nikatoka pale nikichelekelea. Nikawa ninatembea na funguo mkononi ili dunia ijue kuwa nina sanduku la Posta.

Hivyo ndivyo nilivyopata sanduku la posta. Hivyo ndivyo nilivyomweleza aliyeuliza swali ambaye alikuwa na kiu ya kujua jinsi ya kuwa na sanduku la Posta.

Nilieleza – hatua kwa hatua – nilivyopata sanduku; kwa kuamini kuwa alikuwa anafuatilia na angeweza kuelewa jinsi ya kufanya. Utaona kwamba sikumweleza jinsi sanduku la Posta linavyopatikana hivi sasa. Nilieleza ya kipindi kilichopita. Lakini kwa kuwa alikuwa anaita kutoka jijini Dar es Salaam, na sehemu nilizokuwa nikitaja alikuwa akisema kuwa anazifahamu, nilitarajia angeweza kufuatilia kama nilivyofanya na kufanikiwa. Na ndivyo alivyonieleza; kuwa ameelewa nilivyoeleza na kwamba atafuata mkondo huo. Kwamba ataanzia palepale maulizo nilipoanzia na kwamba atanifahamisha matokeo yake.

Hajanifahamisha iwapo amekwenda Posta, amepeleka maombi au amepata sanduku. Ninasubiri taarifa. Lakini wewe je, una sanduku la Posta?

Wasiliana na Mhariri wa Jamii kwa namba: 0713 614 872/0763 670 229