MAONI YA MHARIRI: Mabango haya yanaonyesha udhaifu wa utendaji serikalini

Vitendo vya wananchi kubeba mabango katika ziara za viongozi wakuu wa nchi sasa vimekuwa kama ada.

Ukweli ni kuwa tangu kuingia madarakani kwa utawala wa Awamu ya Tano, kumekuwapo na ongezeko kubwa la watu kubeba mabango hasa katika ziara za Rais John Magufuli.

Kinachotia matumaini ni kuwa Rais amekuwa akiyasoma yanayoandikwa na kuyafanyia kazi papohapo na mengine kuahidi kuyashughulikia.

Kasi hii ya wananchi kubeba mabango ilijitokeza zaidi wakati Rais Magufuli alipofanya ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kiasi cha kuibua vurugu.

Kwa hali ilivyo, tutarajie kuongezeka ziadi kwa kasi hii ya kuonyesha mabango kwenye ziara za viongozi, hasa baada ya mapema wiki hii Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuagiza wananchi wanaokwenda na mabango mikutanoni wasizuiwe kwa kuwa kufanya hivyo ni kuonyesha hisia zao.

Hata hivyo, ujumbe mwingi unaoandikwa katika baadhi ya mabango hayo, unatupa shaka kiasi cha kulazimika kuhoji, ikiwa kero na kadhia wanazolalamikia wananchi haziwezi kushughulikiwa na viongozi mbali ya Rais au Waziri Mkuu.

Unapoyasoma mabango hayo katika maeneo mbalimbali aliyotembeleaa Rais, utagundua kuwa baadhi hayahitaji kabisa mkono wa Rais wala wa Waziri Mkuu.

Ni masuala yanayoweza kutatuliwa kirahisi na mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mameya na watendaji wengine serikalini. Lakini hilo halifanyiki, kila kitu sasa watu wanakimbilia kwa Rais au Waziri Mkuu.

Kwa nini tufike mahala hata suala kama la kugawa mashamba kwa wananchi, lishindwe kutatuliwa na viongozi katika ngazi husika mpaka wananchi waandike mabango na kuyaonyesha katika ziara za viongozi wakuu?

Ni dhahiri kuwa uko udhaifu kwa viongozi wengi. Ni udhaifu wa ama kutojua maana ya uongozi au kutojua wajibu wao kwa wananchi.

Tunaamini kuwa kama watendaji serikalini wataendelea na mtindo huu wa kusubiri mamlaka za juu kutoa uamuzi, halitakuwa jambo la ajabu kuona Rais na pengine Waziri Mkuu wakiwafunika viongozi wengine jambo ambalo tunadhani kwamba halitakuwa suala lenye afya kiutendaji hasa kwa nchi yetu inayoendeshwa kwa misingi ya uongozi wa ushirikishwaji.

Kwa nini tujinasibu kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa mfumo wa ugatuaji wa madaraka ya kiuongozi na kiutendaji, ikiwa viongozi walio wengi wanamezwa na utendaji wa viongozi wakuu?

Ni wakati sasa wa watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali za kiuongozi kuamka na kuweka taratibu madhubuti za kukutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi kwa haraka. Hatuwezi kuendelea kwa mtindo huu wa kuwa na viongozi wakaa ofisini na wasio na uwezo wa kuchukua hatua kwa mambo madogo. Watekeleze agizo la Rais la kuwafuata wananchi na kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi.

Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa ili tuendelee, tunahitaji pamoja na mambo mengine viongozi bora. Hawa ni viongozi wanaojua wajibu wao, wanaoujua kuwa wao ni watumishi wa wananchi kwa ajili ya ustawi wao.

Viongozi na watendaji wasipobadilika kiutendaji, tusahau maendeleo na tuifute kabisa ndoto ya safari ya nchi yetu kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.