KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kitendawili cha kuumba na kuumbua

Ndimara Tegambwage

Kutoka Meza ya Mhariri wa Jamii

Nina kitendawili kina maelezo marefu.

Niliwahi kukitega mara nne katika sehemu mbalimbali lakini hakuna aliyeweza kukitegua.

Nami sikuwasaidia kukitegua, wala sikuomba au kudai mji. Sasa ninakileta mbele ya wengi. Hiki hapa:

“Kitendawili! Kuna kitu kimoja hakionekani kwa watu wengi ingawa ni muhimu kwao.”

Wanapita pale. Wanakanyaga pale. Wanaona watu wakitenda shughuli isiyoisha; ama wakiumba au kuumbua – kila baada ya miezi miwili au mitatu. Hata wanaojigamba kuwa na macho makali, ama hawakioni au wanakiona na kushindwa kukitaja.”

Kwa kitendawili hiki, hata nikitaka miji yote mikubwa nchini; hata nikitaka miji yote mikubwa duniani kote, hata nikitaka nchi zenyewe; anayetaka jibu atalazimika kunipa nitakacho kwa kuwa jibu halipatikani kwa mwingine.

Kwa shabaha ya kuwalegezea wanaoendelea kufikiri, hebu niseme kuwa kitu hiki kipo Jijini Dar es Salaam, katika Wilaya ya Kinondoni, karibu na eneo linaloitwa ‘Kwa Kopa.’

Bado sioni wa kupata jibu, labda awe mwandishi wa habari. Naye simuoni haraka. Hebu nilegeze kidogo: Kitu hicho kinaonekana karibu na Hospitali ya Mwananyamala. Bado tu?

Hebu niendelee kulegeza kitendawili. Kitu hicho kipo karibu na soko la vyakula na matunda la Mwananyamala.

Kama mpaka hapo bado hajapatikana mwenye jibu hata mwandishi wa habari, basi hakuna mteguaji.

Sitaki mji wa mtu yeyote, ndani au nje ya nchi. Sitaki nchi ya watu wowote. Sitaki kitu chochote. Acha nile hasara kama kuna hasara. Si husemwa: Poteleambali!

Sasa nategua. Ninafanya hivyo kwa shabaha ya kusaidiana na waandishi wa habari wenzangu.

Ni juu ya matumizi ya macho, masikio na pua. Ni juu ya udadisi na kile tunachoita “umuhimu wa kuona zaidi ya kila mmoja anavyoona.”

Ninategua! Ni barabara. Lakini siyo kila barabara, bali ni ile itokayo kiungo cha Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, eneo la Viktoria, kupitia soko la Mwananyamala, Hospitali ya Mwananyamala hadi kiungo cha Barabara ya Mwinyijuma. Sasa soma wanaoona zaidi. Wanaoona sana. Wanaoona kuliko wengine. Wanaoona vitu vya nyongeza.

Barabara hii, kutoka Viktoria hadi Mwinyijuma, inaweza kuitwa ‘barabara ya lami.’ Hakika kuna lami.

Lakini kitendawili huwa kuanzia eneo la Soko la Mwananyamala hadi eneo linaloitwa kwa Kopa.

Ni kwenye eneo hili ambako lami imebomoka. Hapana! Ndipo lami hubomoka. Labda na hilo siyo sahihi. Siyo kubomoka tu, bali ni ambako barabara huchimbika.

Wakati kumebanduka, kumebomoka, kumechimbika; foleni ya magari huwa ndefu kiasi kwamba huchukua hata zaidi ya dakika 30 kutoka kiungo cha Mwinjuma hadi Ali Hassan Mwinyi, urefu wa karibu nusu kilometa.

Kinachofurahisha hapa ni kwamba, mibanduko na mashimo huzibwa mara kwa mara.

Yaweza kuwa mara tatu au nne kwa mwaka; au kila baada ya miezi mitatu au minne.

Kingine kinachofurahisha ni jinsi waziba mashimo wanavyofanya kazi yao.

Ni hivi; Penye shimo au mbanduko, “wataalamu” hawa huweka udongo wenye changarawe kiasi na kushindilia.

Ukikuta mafundi wamefunga barabara hiyo huku na kule wakichekecha udongo na changarawe wengine wakichanganya wanachochanganya, wakikimimina ama kwenye michubuko, mibanduko au kwenye shimo, jasho likiwachuruzika huku mashine ya kukandamizia “udongo” ikirindima, hakika utasema wako kazini.

Na wanakuwa kazini kweli. Udongo wenye changarawe unakandamizwa unalingana na ilipokomea lami iliyobakia.

Wataalamu wanaondoa vyombo vyao. Magari yanaanza kwenda kwa kasi.

Ni kasi yenye madhara pia. Inayokwangua maeneo yaliyowekwa ‘udongo’ hasa madereva watukutu wanapofunga breki kwa kustukiza na kutifua mlingano uliowekwa na wataalamu, na kuibua vumbi. Vumbi likaenea kote, hasa sokoni na kutua kwenye machungwa, maembe, maparachichi, mapapai, samaki wakavu, karoti, viazi, magimbi, mihogo, ‘urembo wa machinga,’ mahindi ya kuchoma, vichwani na midomoni mwa waendao sokoni.

Kwahiyo kunakuwa na mmomonyoko unaoletwa haraka na magari, upepo, mvua na miguu ya binadamu waliovaa viatu au hata pekupeku.

Waharibifu zaidi ni watunza usafi wa barabara hii. Wameapa kuondoa mchanga barabarani. Kila uchao wao na fagio mkononi.

Ni wapinzani wa wataalamu waliomwaga ama kifusi, kokoto au mchanga wenye changarawe katika mashimo yaliyo kwenye lami.

Unakuwa mzunguko: Mashimo au mibanduko; mchanga wa magari, viatu na pekupeku; mchanga wa wataalamu, fagio la maadui wa mchanga; mashimo na mibanduko mipya, mchanga wa magari, viatu na pekupeku; mchanga wa wataalamu…

Unaweza kumudu kubaki Dar es Salaam kwa ajira hii. Uliza wahusika. Kitendawili!