KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kila mwandishi alianza tofauti kufika alipo, nawe anza

Wiki iliyopita, kwenye ukurasa huu, yalichapishwa maoni ya waandishi wa habari wanne wakieleza jinsi walivyopata kazi ya kuandika habari; elimu yao, mafunzo ya nyongeza na wengine kutaja walipo hivi sasa.

Hao walikuwa wakijibu hoja za waandishi wa mitandaoni (blogu) waliotaka Mhariri wa Jamii awaeleze “…unaanzia wapi hasa ili uwe mwandishi wa habari magazetini? Uwe na nini na uweje?”

“Nimechapisha makala kwenye blogu yangu lakini kiu yangu haijakatwa; ni mpaka nipate fursa ya kufanya kazi nikiwa mwandishi wa habari katika kampuni ya magazeti,” amelalama mmoja wa wanaoomba ushauri.

Mhariri wa Jamii alitaka waandishi walioko kazini na siyo yeye, watoe majibu na kueleza pia sifa walizotakiwa kuwa nazo na walizokuwa nazo; na wanazofikiri zilisababisha wawe chaguo la mwajiri.

Mpaka jana, Alhamisi idadi ya wanaoomba kushauriwa ilikuwa imefikia 21 – ongezeko la wataka maoni 10 tangu Alhamisi iliyopita. Soma majibu ya baadhi yao hapa chini:

Mwandishi 1: Si ukitaka kazi unaomba? Hao wameomba na kukataliwa au wanaogopa kuandika barua za maombi na labda baadaye kuitwa kwenye usahili?

Mimi nilikuwa na hamu ya kuwa mwandishi. Hamu tu. Nikafaulu kupata kazi katika kampuni ya magazeti. Ilikuwa kazi ya uboi ; kufagia, kupiga deki na kusomba magazeti kutoka eneo moja hadi jingine.

Nilipowaambia wahariri kuwa ninataka kuwa mwandishi, mmoja wao akanijibu: Andika! Unataka kuwa mwandishi asiyeandika? Niliandika malalamiko. Yakachapishwa siku iliyofuata. Ndio mwanzo wangu wa kuandika.

Lakini hii ilikuwa miezi kumi na moja (11) baada ya kuajiriwa. Wakati fulani mhariri mkuu aliishawahi kuniambia mbele ya watumishi wengine, “…wewe unaweza kuwa mwandishi. Udadisi wako unanifurahisha.”

Nilikabidhiwa kwa ripota mzoefu kwenda kuandika stori za mahakamani. Baadaye nikapangwa kuandika habari za makao makuu ya polisi na hatimaye kusukumwa hospitali kuu ya nchi, Muhimbili ili kapata taarifa za wagonjwa, ajali na vifo.

Sasa nina digrii ya kwanza ya Habari na Mawasiliano. Ninaaminiwa katika maeneo mengi. Bali mwanzo ulikuwa mgumu.

Mwandishi 2: Ni mhitimu Chuo Kikuu cha Tiba na Afya, Muhimbili. Ni daktari kamili. Nilikwenda moja kwa moja, barua mkononi, kwa mhariri wa gazeti na kumuomba niajiriwe ili niwe ninaandika habari za sayansi-elimu tiba.

Ilikuwa baada ya mjadala mrefu; nikijieleza kuwa mradi nina elimu nitajifunza na kushika haraka; mhariri alisema, ‘nenda uandike barua ya maombi; jieleze vizuri na ilete hapa kesho au keshokutwa.’ Niliajiriwa. Mpaka sasa nimekwenda kozi mbili fupi za uandishi wa habari – moja nje ya nchi.

Mwandishi 3: Mpaka sasa sina cheti, stashahada wala digrii. Ninauza sauti yangu tu. Niko katika kituo cha redio. Mwaka huu ndio utawala umeweka utaratibu wa kusoma na mimi nataka kuanza na digrii moja kwa moja.

Hamu yangu ilikuwa kutangaza. Mkuu wa vipindi alinipa usaili. Baada ya kunisikiliza akasema ‘sauti hii inafaa.’ Nikaajiriwa. Nikakuta kumbe kutangaza nako ni uandishi. Lazima ujue jinsi ya kuandika vile ambavyo utatangaza. Nikajifunzia humohumo.

Nitaanza shule msimu wa mafunzo ujao. Natamani kuwa na kitambulisho; kuonyesha nimesomea kazi yangu.

Mwandishi 5: Ninaona kwamba ili uwe mwandishi wa habari unahitaji kuwa na hamu ya kazi hii. Uwe unafuatilia wanaoifanya katika magazeti, redio na televisheni. Ujenge vionjo maalum vinavyokufanya ukose usingizi mpaka uipate.

Ninaona sharti uwe na sababu mbili au tatu za kutaka kuwa mwandishi. Nimekutana na wewe Mhariri wa Jamii katika darasa kwa siku tano na mwanzoni ulituuliza: Kwanini ulichagua kuwa mwandishi wa habari; na ili iweje.

Nilikuelewa sana. Sikujua ningekutana na wewe tena hapa. Ile nia na shabaha ya kuwa mwandishi ndiyo inakupeleka kuomba kazi na kuonyesha kwa vitendo kuwa unapenda na unaweza.

Nilifanikiwa kushawishi waajiri wangu wa sasa kunipa kazi kabla sijaisomea; lakini nikiwa ninaifanya kwa kuandika habari fupi na kupeleka redioni; na kuandika makala magazetini. Ukionyesha unajua na ukathibitisha hivyo, basi unaaminika.

Nimemaliza diploma. Natarajia kuanza masomo ya digrii mwakani. Kusoma kunaniongozea elimu na maarifa.”

Hii ndiyo makala ya mwisho katika mfululizo wa maoni ya waandishi wa habari walioko kazini, kwa wale wanaotaka kuwa waandishi katika magazeti na vyombo vingine vya habari.

Meza ya Mhariri wa Jamii inawashukuru wote walioshiriki kutoa majibu; na inaamini waliouliza wamenufaika.