KUZA FURSA: Wafiche watu wasijue kiasi cha fedha ulizobeba

Kila atafutaye hutarajia kufaidi matunda ya jasho lake hapo. Ni muhimu kujali usalama wa fedha na mali kwa kuweka mikakati thabiti wakati wote. 

Hii ni kwa sababu fedha na mali zinatafutwa kwa taabu, nguvu na maarifa ya ziada kukabiliana na vikwazo vilivyopo hivyo inapopatikana tunapaswa kuitunza kwa usalama mkubwa ili zitufae.

Tujenge tabia ya kuchukua tahadhari kwa kuhifadhi fedha na mali zetu kwa usahihi kuepuka kuibiwa, kunyang’anywa, kuungua ama kupotea. Kikubwa zaidi ni kusalimisha uhai kwa kutowashawishi wenye nia mbaya kujeruhi hata kukuua.

Zipo njia nyingi ambazo ni salama za kutunza fedha na mali ambazo zinajumuisha kufungua akaunti benki. Epuka kuhifadhi fedha nyumbani ama kuzichimbia chini kwa ajiri ya usalama wako na fedha zenyewe.

Unaweza kutumia mitandao ya simu. Teknolojia imekua hivyo huna haja ya kupoteza fedha zako. Mitandao ya simu mingi ina huduma ya kuhifadhi fedha ambazo haziwezi kupotea hata kama simu itaibwa na hakuna atakayejua una kiasi gani.

Kulipa kwa hundi au cheki ni namna nyingine salama kwako. Zipo akaunti za biashara zinazokupa nafasi ya kumlipa mtu kwa kumuandikia cheki. Hapa huna haja ya kubeba fedha taslimu ili kuwalipa unaofanya nao miamala ya aina tofauti. Jizoeshe kulipa kwa mfumo huu kuepuka upotevu wa fedha zako.

Tumia kadi za benki. Njia ya kisasa ya kutunza na kufanya manunuzi ama malipo kwa usalama ni kutumia kadi za benki ambazo ni salama kwa fedha zako. Benki nyingi zina huduma hii, chagua uipendayo.

Beba fedha kwa siri. Unapotakiwa kubeba fedha nyingi taslimu kutoka sehemu moka kwenda nyingine mfano kupeleka benki, jitahidi kufanya hivyo kwa siri kuepusha kuvamiwa. Hakikisha watu hawakuzoei ili kuwanyima nafasi ya kukuhujumu.

Kila unapolipa msainishe mpokeaji. Kuhifadhi fedha ni pamoja na kujua malipo yote uliyoyafanya kwa kuweka kumbukumbu vizuri. Isitokee umefanya malipo halafu hujui umemlipa nani na kiasi gani, hapo utakuwa umepoteza fedha zako kwa uzembe. Hivyo, hakikisha unapomlipa yeyote, anasaini.

Toa risiti unapouza na dai unaponunua ili uweze kujua gharama halisi za ununuzi na mauzo. Hii itasaidia kufanya mahesabu yako kwa usahihi.

Ni vizuri kukata bima. Bima ni ahadi ya malipo ya fidia inayotolewa na kampuni ya bima kwa wateja wake juu ya hasara wanazoweza kupata muda wowote kwa malipo ya  ada ama mchango kwa muda maalum. Mteja anachangia kiasi cha fedha ndani ya muda maalum na kampuni husika inaahidi kumfidia mteja huyo kwa aina ya hasara atakayopata mteja kwa mujibu wa makubaliano.

Wajasiriamali na wafanyabiashara wanawekeza nguvu na fedha katika miradi yao wakati wa kuanza na kukuza miradi hiyo. Inapotokea uharibifu wowote katika biashara na miradi itakayosababisha hasara ambazo zingeweza kufidiwa na bima, mjasiriamali huchukua tena muda mrefu kupata mtaji na kurudi katika biashara kama hatakata tamaa.

Bima ni muhimu kwasababu inalinda biashara kutokana na majanga yasiyo tarajiwa. Vilevile, inalinda wafanyakazi dhidi ya magonjwa au tatizo lolote la kiafya.

Inasaidia kulinda katika eneo lako la kazi, kumlinda mwenye biashara kutokana na hasara au majanga na kuweka mazingira bora ya ufanisi wa biashara yako.

Bima ni muhimu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara ambao wanawaza kupata faida tu na kuchukulia bima kama ni gharama ya bure ama hudhani ni gharama kubwa na hawawezi kuilipa.

Ni vyema kwa uwezo wako, udogo ama ukubwa wa biashara yako ukaanza kupata maelezo ya aina za bima kutoka kwa kampuni na mawakala mbalimbali kuona wapi utaweza kujiunga na kufaidika na huduma ya bima muhimu kwa maendeleo ya biashara yako.

Maswali na majibu:
Simu: 0672 050 285
Baruapepe:[email protected]
SkyLink Agency