UCHAMBUZI: Ni muhimu kuheshimu ubunifu wa wengine katika sanaa

Katika muziki hususani wa Bongo Fleva ni vyema kuzungumzia hakimiliki na hoja jadidi kuhusu viwango vya ubunifu wetu katika kazi za sanaa. Utayari wetu kuheshimu ubunifu wa wengine na kuomba ridhaa au ruhusa rasmi kwa makubaliano katika kutumia sehemu ya ubunifu wa wengine katika kazi zetu.

Hapa nimezingatia mambo matatu. Mosi kuheshimu na kabla ya kutumia kuomba ruhusa. Pili ni kutokuomba lakini kujiweka katika utayari wa kulipa fidia endapo shauri litafikishwa panapohusika na mwisho kuangalia ukomo wa kitambo cha uhai wa sheria ya hakimiliki.

Mambo haya matatu katika uzito wake yanahusu matumizi ya kazi za wengine. Pale ambapo msanii amefilisika ubunifu na kusudio la kuazima kwa mwingine.

Katika muziki hasusani wa Bongo Fleva kuna kifaa kinatumika kuzalisha midundo na kuchanganya mirindimo na milio mbalimbali.

Kifaa hiki huweza kuzalisha sampuli mbalimbali za milio ya kila kifaa cha muziki baada ya utunzi ambao ulitumia sampuli ya mapito ya mapulizo ya saxophone kama ile ya bendi ya Juwata Jazz Band katijka wimbo wake wa ajali ambayo imeamsha limeamsha suala la kisheria juu ya hakimiliki dhidi ya wimbo wa WCB maarufu kama Zilipendwa.

Utayari wetu kuheshimu ubunifu wa wengine na kuomba ridhaa au ruhusa rasmi kwa makubaliano katika kutumia sehemu ya ubunifu wa wengine katika kazi zetu.

Tuwe na utayari wa kulipa stahiki za matumizi bila ridhaa ya mhusika na kurejelea kimo cha muda wa kikomo wa uhai wa hakimiliki.

Lipo suala adhimu la mmiliki halali wa wimbo. Inafahamika vyema bendi maarufu ya Juwata Jazz Band kwamba enzi hizo jumuiya ya wafanyakazi ikiwa moja ya matawi tano muhimu ya CCM iliasisi uundwaji na ulezi wa bendi baadae ikawa imebadili jina na kuitwa Ottu Jazz Band na hatimaye sasa baada ya kukabidhiwa rasmi kwa wanamuziki wenyewe kuiendesha inaitwa Msondo Ngoma. Kimantiki mabadiliko ya majina yanaleta dosari katika madai ijapokuwa uhalali ungalipo kama miliki halali.

Wenye bendi ya Msondo ambao wamebadili majina kwa sababu mbalimbali halali wana haki ya kusimamia rasilimali zao dhidi ya upotevu wowote.

Historia ya sheria ya hakimiliki ni ndefu na ngumu. Ilianza rasmi na mwanzo wa machapisho ya maandishi hasusani udurufu wa magazeti na vitabu miaka ya 1800.

Jambo la msingi lilikuwa uhalali wa mmiliki wa andiko. Baadaye ikasambaa kwa wabunifu wa vitu, mashine, mitambo na nyimbo. Jamii mbalimbali Ulaya zilitofautiana katika namna ya kushirikisha wengine waliotofautiana katika matumizi ya kuboresha.

Wapo waliotofautiana katika viwango vya kuuziana ubunifu. Mathalani wazo bila kuundwa na kusajiliwa kwa jambo au kitu hakumpi mhusika uhalali. Kitu au jambo lililo buniwa na kusajiliwa mwanzoni lilipewa ukomo wa miaka 50 kabla mwingine kupata fursa ya maboresho au matumizi.

Taarifa ya msingi ina mambo mawili kwamba mosi ni takwa la malipo ya milioni 300 na pili kusudio la kushtaki.

Kwamba dhamira ya mdai ni taarifa yenye makusudio mawili. Mosi kulipwa na pili kushitaki. Hapa kimsingi shughuli ni madai basi mdaiwa anataarifiwa na kwa hivyo anao wajibu wa kupatana kwa kujibu waraka au kuamua kukaa kimya shauri lifikishwe mahakamani kwa maamuzi.

Njia zote ni halali kwamba yapo mapatano nje ya mahakama yanayo tambulika na kuheshimika aidha yapo maamuzi ya hukumu ya mahakama ambayo yanapaswa kuheshimiwa. Uchaguzi wowote wa njia ifaayo ni halali.

Katika muziki pametokea sintofahamu kuhusu madai ya bendi kongwe ya muziki wa dansi Msondo Ngoma dhidi ya WCB ambayo ni kampuni ya msanii maarufu Naseeb Abdul maarufu Diamond kuhusiana na kutumia bila ridhaa au makubaliano rasmi sehemu ya wimbo hasusani kionjo cha saxophone kilichomo kwenye wimbo wa Juwata Jazz Band ulioitwa “Ajali” na kutumika isivyo halali katika wimbo wa WCB ulioitwa “ Zilipendwa “.

Nimalize kwa kusema bendi au mwanamuziki anapotunga wimbo au hata albamu sehemu muhimu ya haki yake huhamishwa kwa yule anaye rekodi na kusambaza baada ya kuuziana, hivyo sehemu muhimu ya hakimiliki inahamia kwa msambazaji halafu katika fursa za kusikika na wigo mpana wa kidigitali muziki unapakuliwa na kusambazwa katika mitandao kwa gharama ndogo.

Hufanywa hivi ili kazi ya mwanamuziki iweze kufikia watazamaji na wasikilizaji wengi zaidi hapa vilevile haki miliki inahamika kwa sehemu fulani kwa mwenye mtandao unaotoa fursa.

Ukisikiliza nyimbo zote mbili ile sehemu ya mlio wa mapulizo ya saxophone ni kionjo muhimu lakini hakibadili ujumbe wa wimbo au mirindimo yake vilevile ni muhimu kwa wanamuziki kupenda kutumia ubunifu wao katika kazi.

Penye hitaji la matumizi ya ubunifu uliofanywa na wengine yafaa utanguliwe na makubaliano rasmi. Zipo kazi za wanamuziki wa bendi kubwa ambazo kimsingi wamebadili maneno tu vingine ni uigizaji wa kazi za ubunifu wa wengine.

Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa Mwananchi.