Ningekuwa kiongozi wa upinzani, nisingepuuza waraka wa Masha

“...Natambua kwamba kukosoa ni kazi muhimu ya chama cha upinzani, (lakini) kazi hii pekee haikifanyi chama kuwa chama mbadala cha kuunda Serikali.” Hii ni sehemu ya maneno aliyoyaandika Lawrence Masha katika waraka wake wa kutangaza kujivua uanachama wa Chadema.

Katika aya nyingine ya waraka huo wa Novemba 14, Masha nasema: “Upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa kutegemea udhaifu wa CCM badala ya uwezo wake kama mbadala.”

Akitumia kanuni hii kuutathimini upinzani wa Tanzania, Masha anasema Chadema imeendelea kujikita katika kukosoa na kuonyesha madhaifu ya Serikali na hasa Rais John Magufuli na kwamba upinzani wa sasa umeridhika na hali ya kuendelea kuwa wakosoaji ili kusaidia CCM kujirekebisha.”

Maana yake ni kwamba, wapinzani wameshindwa kuonyesha uwezo wao kama chama mbadala na kwa sababu hiyo, Masha anamalizia waraka wake kwa kutangaza kujivua uanachama wa Chadema.

Kwa maoni yangu, huu ni waraka wa kujitoa katika chama kistaarabu kuwahi kuandikwa katika siasa za Tanzania za hivi karibuni.

Kauli ya Sugu na Zitto

Akizungumza bungeni hivi karibuni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, ‘Sugu’ alisema: “Tulipofika hapa (bungeni), tulipoanza hili Bunge ilifika sehemu hata sisi wapinzani tulisema, ‘da! Sasa huyu jamaa aliyekuja tutakuwa na hoja gani?’ (Serikali) Mnaleta hoja wenyewe (kwa maana udhaifu wenu unatubeba)”

Nikitumia maneno yangu kufafanua, Sugu anasema ufanisi wao, kama wapinzani unategemea makosa ya Serikali iliyopo, na wala hataji kuwa wanategemea mipango, mikakati na ubunifu wao utakaozidi ile ya Serikali ya chama tawala.

Ni kwa sababu hii wapinzani walihofia mustakabali wao katika siku za awali za utawala wa Rais Magufuli. Kauli hii ya mbunge huyu machachari wa upinzani, inaakisi maono yao na hivyo inadhihirisha ukweli wa kauli ya Masha.

Ni rahisi kutamani kitu kitokee, lakini ni suala jingine kukifanyia kazi kitu husika ili jambo unalolitamani litimie. Wapinzani wanataka watwae nchi 2020, kama Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Majini anavyoandika kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Maandishi ya Zitto yanaanza kwa kauli “2020 Magufuli kukoma urais, kisha akaendelea... Tunatuma salamu kwake. Mwaka 2020 will be certainly the end of Magufuli’s presidency (Mwaka 2020 ndio mwisho wa Magufuli kuwa Rais wa Tanzania). Watanzania si wajinga kiasi hicho. Watanzania wa sasa tuna akili, tumesoma na tuna uelewa. Hatutamuacha Ikulu.”

Nataka uzingatie kipande cha kauli ya Zitto ya kujiaminisha kuwa upinzani utamshinda Rais Magufuli 2020. Inawezekana kuwa Rais Magufuli, Serikali yake na CCM anayoiongoza wana mapungufu mengi, lakini mapungufu hayo pekee hayatoshi kuwapa wapinzani ushindi, kama Masha anavyoandika.

Bado Watanzania watapima nguvu na udhaifu za kila upande kabla ya kuamua wampe nani ridhaa ya kuwatawala.

Kinachowaongoza watu kuchagua

Ni kweli kuwa kiasi cha udhaifu wa chama tawala kinaweza kuchangia katika urahisi au ugumu wa kushindwa, lakini si kigezo pekee. Hii ndiyo hoja ya Masha, na ni hoja ambayo inaungwa mkono na hata baadhi ya nadharia za siasa zinazohusiana na namna watu wanavyochagua chama au mgombea wa kumuunga mkono.

Katika pitapita yangu kweye vitabu vya sayansi ya siasa, nilikutana na nadharia mbili zinazoongoza watu katika kuchagua chama au mgombea fulani katika mazingira ya upinzani, moja inaitwa ‘spatial’ (kushindanisha sera na nyingine) na nyingine inaitwa ‘valence (imani kwa chama au mgombea).’

Nadharia ya ‘spatial’ inasema kwamba, wapiga kura wanatathmini misimamo ya vyama kuhusu masuala mbalimbali ya kinadharia na kisera, na kisha huchagua chama ambacho kiko karibu zaidi ya wanachoamini kitawapa faida kutoka katika uwanda mpana wa mawazo yanayoshindana.

Ingawa, nadharia hii pia inasema upo uwezekano wa watu kuchagua kwa mazoea, yaani kurejelea uzoefu wa nyuma na kuchagua kile alichokuwa akichagua kule nyuma, lakini kimsingi katika mazingira yenye hali ya kisiasa iliyobadilika, kufuatia uelekeo mpya wa sera za CCM, kwa vyovyote tutegemee 2020 watu wengi kufanya tathmini upya.

Katika muktadha wa siasa zetu, swali ni je, baada ya wapinzani kuonyesha udhaifu wote wa CCM, wao wanakuja na sera, mipango na mikakati gani ambayo ni bora zaidi kuliko ile ya CCM, kwani haitoshi kukosoa tu bila kuleta sera mbadala.

Kauli ya Sugu kwamba, walihofia kuwa kwa Serikali hii wangekosa cha kukosoa ni dalili ya aidha kukosa sera na mipango au kama wanayo kutoizingatia.

Wananchi wanataka kusikia, wapinzani wangefanya nini ili kuletea wananchi maendeleo, kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa namna endelevu. Mipango hiyo inatokana na nadharia gani za maendeleo na wapi mipango ilijaribiwa ikafanikiwa?

Nadharia ya ‘valence’ inasema muhimu katika uchaguzi ni mtazamo wa wapiga kura kuhusu uwezo wa viongozi na chama kupambana na matatizo makubwa yanayoikumba nchi. Kinachofanywa na wapiga kura ni kulinganisha uwezo wa kiutawala au uongozi wa mtu katika kuwaletea wananchi mafanikio katika changamoto zao.

Nadharia hii ni kinyume na ile ya spatial kwa sababu, wapiga kura wanaelewa udhaifu wao wa kuelewa mambo ya kiufundi katika sera na mipango, hususan ya kiuchumi, kwa hiyo muhimu kwao ni imani katika uwezo wa viongozi au chama husika.

Katika muktadha wa siasa za Tanzania, hususan ufanisi wa wapinzani, tunaona kwamba, ni muhimu vyama vya upinzani na viongozi wao wajijengee imani kwa wananchi kwamba kweli wakipewa nchi wanaweza kuiongoza vema, lakini bado vinatia shaka juu ya uwezo wao wa kuiongoza nchi. Nitatoa mifano.

Vyama vya upinzani, havina demokrasia ndani ya chama, ingawa vinahubiri demokrasia kitaifa. Vina migogoro kila uchao inayotishia hata uhai wa vyama vyenyewe. Fikiria, ingekuwaje kama mgogoro wa CUF ungejitokeza wakati chama kipo madarakani? Vyama vya upinzani vinakosa misimamo imara katika masuala ya maadili. Leo kiongozi huyu ni mbaya, fisadi lakini kesho akienda upinzani, ni mwema.

Hakuna jambo ambalo Watanzania wanalithamini kama ‘utaifa’ lakini baadhi ya vyama vya upinzani vinaonekana kuwa na ushawishi katika baadhi tu ya maeneo fulani tu na kutokuwapo kabisa katika maeneo mengine. Kuna hata ‘mitazamo’ kuwa chama kina mvuto kwa Wakristo na kile kwa Waislamu. Katika hali hii, njia pekee ya kuishinda CCM ni kuunganisha nguvu aidha kuunda chama kimoja au muungano, mfano wa Ukawa.

Lakini hebu angalia hali ya Ukawa sasa hivi. Huku kuna CUF – Lipumba ambao hawataki muungano. Chadema na CUF nao wanawawekea ngumu ACT – Wazalendo wasijiunge nao. Katika hali hii, tutakuwa na Ukawa 2020 ambapo upinzani unahitaji kila kura moja kuishinda CCM?

Vyama vya upinzani pia vimeshindwa kujipanga kufanya siasa nzuri ya kupima hoja, kusifu panapostahili na kukosoa inapopasa. Katika hili, kutokana na kauli za kukatisha tamaa za wapinzani, na kutotambua walau hata juhudi tu zinazofanyika kwenye maeneo machache, hata kama hazina mafanikio, na hivyo kuthibitisha dhana kuwa wao kazi yao ni kupinga tu. Haya ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwafanya wapiga kura iwawie rahisi kuamini CCM, licha ya kuvurunda kwao kuliko wapinzani.

Wapinzani jipangeni

Kwa ufupi, hoja yangu ni ileile ya Masha, kwamba licha ya udhaifu wa CCM, wapinzani wanatakiwa si tu wakosoe bali waje na mbadala wa sera na mipango ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Watu wanaweza kuona wazi kuwa chama tawala na serikali yake wanaendesha nchi hovyo, lakini watajiuliza pia tuna mbadala? Wakati watu wanajiuliza hivi, zingatia pia kuwa kwa kawaida ni jambo ngumu zaidi watu kubadilika kuliko kubaki katika hali iliyopo, yaani unahitaji nguvu ya ziada kushawishi watu kujaribu jambo jipya, kuliko kuwafanya wabakie katika hali iliyopo.

Kubadilika ni kwenda usikokujua hakika yake zaidi ya ahadi, ambayo inaweza kuwa ni fikra zisizo na uhalisia. Kwa kutumia saikolojia hii, CCM wanahitaji kuonyesha mafanikio yao katika miaka mitano 2015 – 2020 na kuwatisha wananchi juu ya hatari ya wapinzani kuwapeleka wasikokujua.

Kwa wapinzani kazi ni ngumu zaidi. Mabadiliko yoyote yanakuja na hatari zake, kwa hiyo ili watu waweze kubadili kilichopo lazima uwashawishi kwelikweli kuwa wakikuchagua wanafanya uamuzi sahihi. Vinginevyo, watu watasema: “Zimwi likujualo halikuli likakwisha.”