Mtazamo kuhusu kodi za kimataifa na uhamishaji mtaji kutoka Afrika

Muktasari:

  • Katika kitabu kilichoandikwa katika mradi wa utafiti wa masuala ya kodi uitwao (kodi, taasisi na ushiriki) Taxation, Institutions and Participation (TIP), mitizamo mbalimbali imewekwa bayana. TIP ni mradi wa utafiti wa miaka minne (2014–2018) chini ya ufadhili wa Tume ya Utafiti ya Norway unaotekelezwa Tanzania, Angola na Zambia.

Kuna mitizamo tofauti kuhusu kodi za kimataifa na uhamishaji wa mitaji kutoka nchi za Afrika. Ni sehemu chache mitizamo hii imewekwa pamoja kama vile kuandikwa vitabuni.

Katika kitabu kilichoandikwa katika mradi wa utafiti wa masuala ya kodi uitwao (kodi, taasisi na ushiriki) Taxation, Institutions and Participation (TIP), mitizamo mbalimbali imewekwa bayana. TIP ni mradi wa utafiti wa miaka minne (2014–2018) chini ya ufadhili wa Tume ya Utafiti ya Norway unaotekelezwa Tanzania, Angola na Zambia.

Kwa Tanzania mradi upo Chuo Kikuu Mzumbe ukisimamiwa na mwandishi wa makala haya.

Kuhusu kitabu

Kitabu hiki kinaweka mitazamo mbalimbali pamoja kikiwa kimehaririwa na Profesa Odd-Helge Fjeldstad, Sigrid Klaeboe Jacobsen na Peter Henriksen kutoka Norway na Prosper Ngowi wa Chuo Kikuu Mzumbe. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa utafiti na maoni kutoka sehemu mbalimbali duniani kuhusu upotevu wa fedha kutoka Afrika kupitia kodi za kimataifa na uhamishaji wa mitaji. Tafsiri isiyo rasmi ya jina la kitabu kutoka lugha ya Kiingereza ni Ufunuaji wa Ushungi wa Siri: Mitizamo ya Kodi za Kimataifa na Uhamishaji Mitaji Kutoka Afrika.

Kilizinduliwa Oktoba jijini Nairobi ingawa uzinduzi rasmi utafanyika Chuo Kikuu cha Mzumbe katika tawi lake lililopo jijini Dar es Saaam, mwishoni mwa mwezi huu.

Dhana ya kodi

Sehemu ya kwanza ya kitabu inaelezea dhana na haki za kikodi. Pia inaeleza wajibu wa serikali kwa atu wake; maficho ya kodi duniani na juhudi zinazofanywa na jumuiya za kimataifa kuhakikisha kunakuwapo mfumo wa kodi ulio wa haki.

Ujumbe mkuu ni kuwa kodi ni jambo muhimu kwa serikali kupata fedha za uhakika kugharamia miradi ya maendeleo zikiwamo huduma za jamii. Hata hivyo, kuna fedha nyingi za umma zinatoroshwa kwa njia na sababu mbalimbali na kuwekwa katika nchi zinazojulikana kuwa maficho ya kodi.

Kitabu hiki pia kinatizama kwa ukaribu matokeo ya maficho ya kodi na mfumo wa siri za fedha. Pia kinatizama kiasi cha fedha zinazopotea kutoka nchi zinazoendelea na athari zake katika maendeleo ya nchi hizi.

Jambo kuu ni kuwa nchi ambazo ni maficho ya kodi hutoa vivutio mbalimbali ili wenye fedha wazipeleke humo. Kilichobainika, kivutio kikubwa ni usiri wa wateja unaowekwa na vyombo vya fedha katika nchi hizi. Haziwajibiki kuweka wazi taarifa za wateja wa benki zao.

Kimsingi nchi hizi zinafaidika kiuchumi kutokana na mitaji hii kuingia katika mifumo yao ya fedha hivyo si rahisi ziwe na motisha ya kuzuia fedha zinazoingia kwao.

Kitabu hiki pia kinatoa picha ya jumla ya wawezeshaji wa utoroshwaji fedha na mitaji duniani ambao wanajumuisha wakaguzi wa hesabu za fedha, wahasibu, wanasheria, benki za biashara, kampuni za kimataifa na serikali za nchi yalipo maficho ya kodi. Kila mmoja kati yao, anaweza kusaidia kwa njia moja au nyingine utoroshwaji fedha na mitaji.

Maliasili

Ipo sehemu ya kitabu hiki inayotizama uziduaji wa rasilimali kama vile gesi, mafuta na madini yanayojumuisha dhahabu, shaba, almasi na tanzanite. Sekta ya maliasili ni miongoni mwa kubwa zaidi za kiuchumi Afrika ikilinganishwa na biashara za aina nyigine.

Kwa hiyo serikali duniani, hasa Afrika lazima ziwe makini zinapotengeneza mifumo ya kodi ya sekta hii. Pamoja na mambo mengine, ni muhimu kutambua kwamba baadhi ya maliasili hazijizalishi. Zikishavubwa kutoka ardhini au kwingineko zinakwisha na nchi husika kupungukiwa hazina kwa kiasi kilichovunwa.

Kama thamani iliyochimbwa haitapatikana kwa kodi, mirabaha na tozo nyinginezo nchi hubaki masikini zaidi. Fedha zinazoptikana kutoka kwenye sekta hii lazima zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo kuliko ya kawaida huku vizazi vijavyo vikiwekwa katika fikra za watunga sera na watawala waliopo.

Vilevile, kitabu kinatoa picha ya jumla ya kazi za sasa za mashirika ya kimataifa na ya ndani katika mapambano dhidi ya upotevu wa fedha na rasilimali nyingine. Wadau hawa ni pamoja na Shirika la Maendeleo ya Uchumi (OECD). Mengine ni Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Benki ya Dunia.

Kwa miaka mingi mashirika haya yamekuwa yakitafuta njia za kuwa na mfumo wa kimataifa wa kodi wenye haki. Pamoja na juhudi hizi bado mfumo huu haupo katia nchi nyingi hasa zinazoendelea.

Kitabu kilifanyiwa uzinduzi wa awali, Oktoba 11 jijini Nairobi katika kongamano la kimataifa kuhusu utoroshwaji fedha Afrika. Uzinduzi huu wa awali ulifanywa na taasisi ya Christian Michelsen Institute (CMI), Chuo Kikuu Mzumbe na Tax Justice Network Norway.

Uzinduzi mwingine unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, Chuo Kikuu Mzumbe jijini Dar es Salaam kasha maeneo mengine duniani.