MAONI YA MHARIRI: Hongereni Wazanzibari kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi

Leo Wazanzibari wanasherehekea miaka 54 ya Mapinduzi, ikiwa ni kumbukumbu muhimu kwa wakazi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Tarehe kama ya leo mwaka 1964, wananchi wa Zanzibar wakiongozwa na mwasisi wa Mapinduzi, Sheikh Abeid Amani Karume na wenzake kupitia kilichokuwa chama cha Afro Shirazi Party (ASP), waliung’oa utawala wa Kisultan uliokuwa ukitawala visiwa hivyo kwa miaka mingi.

Utawala huo ulidumu Zanzibar kwa zaidi ya karne moja na nusu tangu mwaka 1804, huku ukiwa unalindwa na Waingereza.

Sote tunajua kuwa Mapinduzi haya hayakutokea tu pasipo sababu. Kulikuwa na dhamira na sababu maalumu zilizowasukuma Wazanzibari kubeba silaha na kuuangusha utawala wa Kisultani.

Wazanzibari wakati huo pamoja na mambo mengine walitaka Zanzibar inayotawaliwa na wananchi wenyewe, Zanzibar ambayo raia mwenye asili ya Kiafrika awe na haki sawa na raia mwingine.

Haya yalikosekana kwa muda mrefu; Wazanzibari wanyonge wakataka kujikomboa na ndio maana Karume akawaongoza wananchi wenzake katika mapambano ya kujikomboa kutoka kwa Sultani.

Dhamira ya mwasisi huyu na wenzake ilikuwa ni kuiona Zanzibar ya maendeleo na haki kwa kila raia hasa Waafrika ambao kwa muda mrefu waliminywa kimaendeleo na wageni.

Dhamira hii ndiyo ambayo leo tunaposherehekea sikukuu hii, hatuna budi kuwakumbusha Wazanzibari kuwa bado ipo na inapaswa kusimamiwa kwa nguvu na msukumo uleule uliokuwa wakati wa kina Sheikh Karume. Tunakiri kuwa mengi ya kuvutia na kupigiwa mfano yamefanywa chini ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuanzia awamu ya kwanza mpaka awamu ya sasa inayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein. Atakayesema hakuna maendeleo yaliyoletwa na Mapinduzi, pengine ana lake jambo au hataki kukubali uhalisia uliopo.

Hata hivyo, mafanikio hayo yasifanye Serikali na Wazanzibar kwa jumla kubweteka.

Safari ya Zanzibar ya maendeleo, haki na utawala wa sheria bado ingalipo na kwa umoja wao Wazanzibar hawana budi kuhakikisha inafanikiwa tena kwa kiwango kikubwa zaidi.

Miaka 54 ya Mapinduzi pamoja na jitihada za Serikali, bado Wazanzibari wanakabiliwa na matatizo kama huduma duni za afya, makazi na elimu, ukosefu wa ajira na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana.

Aidha, Mapinduzi yalikusudiwa kufuta unyonge wa wananchi wa tabaka la chini, kuwatoa katika lindi la umaskini na kuwainua kiuchumi.

Tunapoadhimisha kumbukumbu hii muhimu haya ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kutiliwa maanani na kila Mzanzibari.

Zanzibar haitaendelezwa na mgeni bali Wazanzibari wenyewe. Na ili maendeleo hayo yapatikane lazima Wazanzibar kwa kutumia dhamira ya Mapinduzi wakubali kuweka pembeni tofauti zao na kufanya kazi ya kuiendeleza nchi kama umma mmoja uliogubikwa na mshikamano na usalama wa nchi kwa jumla.

Ili Zanzibar ifike huko inahitaji uongozi madhubuti mithili ya ule wa Sheikh Karume ambao kwa muda mfupi ulifanikiwa kuibadilisha kwa namna mbalimbali sura ya visiwa vya Unguja na Pemba. Sura hii ni pamoja na ujenzi wa makazi ya nyumba za ghorofa ambazo mpaka leo umekuwa alama muhimu na urithi wa utawala wake.

Hongereni Wazanzibar kutimiza miaka 54 ya kujitawala.