Serikali inaweza kujifunza uwazi kwa wapinzani?

Muktasari:

  • Vyama vya upinzani kinadharia ni Serikali zinazosubiri na hivyo ni lazima kuonyesha mfano kwa Serikali iliyopo madarakani. Uwazi ni moja kati ya maeneo mengi ambayo vyama vinapaswa kuonyesha mfano na kuwashawishi wananchi kwamba wao ni bora zaidi kuliko waliopo madarakani.

Moja kati ya mambo yanayoendelea kuumiza vichwa vya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini ni pamoja na iwapo vyama hivi vinaendesha mambo yao kwa uwazi na ni kwa kiasi gani wanachama wao na wananchi kwa ujumla wanaweza ama kuvichunguza au kuviwajibisha hivyo kuionesha Serikali njia kwa vitendo.

Vyama vya upinzani kinadharia ni Serikali zinazosubiri na hivyo ni lazima kuonyesha mfano kwa Serikali iliyopo madarakani. Uwazi ni moja kati ya maeneo mengi ambayo vyama vinapaswa kuonyesha mfano na kuwashawishi wananchi kwamba wao ni bora zaidi kuliko waliopo madarakani.

“Uwazi haupo ndani ya vyama vya siasa, si upinzani wala chama tawala,” anabainisha mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Hamad Salim.

Uwazi unaohitajika unapaswa kuonyesha ni kwa kiasi gani vyama vyenyewe vinaendesha uchaguzi wa ndani na upatikanaji wa viongozi wake, pia upokeaji na matumizi ya ruzuku kutoka serikalini kwa vile ambavyo vinapokea na uwajibikaji wao wa kifedha mpaka michango ya wanachama na faida zinazotokana na miradi ya kiuchumi ambayo vyama vimewekeza.

Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inaitaka Serikali kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyote vyenye uwakilishi aidha bungeni au katika halmashauri. Pia, kuna michango kutoka kwa watu wanaoguswa na harakati na misimamo ya vyama husika ama kwa uwazi au kwa kificho.

Katika mazingira kama hayo, na mengine ambayo hajaainishwa hapa, yanaufanya uwazi katika vyama vya siasa kuwa jambo la msingi na wala si la kupuuza katika uendeshaji wake.

Ni wazi kuwa mtu anaweza kuhoji kwamba kwa nini shughuli za upinzani ziwe, jibu ni rahisi sana. Ni upinzani ambao kama ilivyodokezwa hapo juu, huwashawishi wanachama wao na wananchi kwa ujumla kwamba wao ni bora kuliko chama tawala na hivyo wanapaswa kupewa dhamana ya kuunda Serikali.

Ni vyama vya upinzani ambavyo mara kwa mara vimekuwa vikiishinikiza na kuitaka Serikali iendeshe mambo yake kwa uwazi huku wakibainisha kuwa kwa kufanya hivyo itarahisisha uwajibikaji wake kwa wananchi na kuwa na jamii itafahamu vizuri mambo wanayoyafanya.

Katika hali kama hiyo mtu yeyote angetemea kuwa upinzani ungeonyesha njia kwa mfano. Lakini, uzoefu unaonyesha kuwa hilo halifanyiki kwa sasa. Hili ndilo linalowaumiza vichwa wafuatiliaji wa siasa na masuala ya utawala bora nchini.

“Ni uwazi upi haswa unaweza kuzungumzia kutoka kwenye vyama vya upinzani? Siuoni,” anasema Richard Mbunda mhadhiri na mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Upinzani hauna mamlaka ya kimaadili ya kuhoji uwazi Serikalini.”

Mfano, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa kauli ambayo ujumbe wake haukuwa wazi kwake mwenyewe kama kiongozi wa umma na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini.

Siku hiyo ya Desemba 31, 2017, ambapo Mbowe alikusudia kuanisha vipaumbele vya chama chake kwa mwaka 2018, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Rai Mwema, Godfrey Dilunga alimuuliza mbunge huyo wa Hai (Chadema) kama alikuwa amewasilisha fomu za tangazo la mali na madeni kwa Sekretarieti ya Maadili. Wakati huo viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali walikuwa wako hamkani wakipanga foleni kuwasilisha fomu zao katika Sekretarieti hiyo. Akijibu swali hilo la mwandishi, Mbowe alisema:

“Niliwasilisha fomu zangu za mali na madeni tangu tarehe 27 Desemba 2017, kabla ya hata Rais (John Magufuli). Tumehakikisha kuwa wabunge wetu wote wanakusanya fomu zao pia kwani hatuna kitu cha kuficha.”

Kiukweli, hili lilikuwa jibu sahihi kulingana na swali la mwandishi aliyeuliza kama tu lingeishia hapo. Kwa bahati mbaya halikuishia hapo.

Mbowe aliongeza kuwa wao (Chadema) wanawataka wale walioko madarakani wasiishie kupeleka fomu zao za mali na madeni katika tume ya maadili tu bali kama kweli wanatakiwa waaminiwe waziweke hadharani watu wazione.

“Hiyo ndiyo changamoto kwa bwana mkubwa kama kweli anataka awe msafi,” aliongeza Mbowe.

Ni bahati mbaya kwamba hakukuwa na nafasi ya kuuliza swali la nyongeza au pengine mwandishi aliyeuliza swali lenyewe hakuona umuhimu wa kufanya hivyo.

Lakini, ilikuwa ni busara kumuuliza Mbowe kuwa ni wapi yeye na viongozi wenzake wa Chadema na upinzani kwa ujumla wameweka hadharani tamko lao la mali na madeni kama anavyotaka wenzake wa Serikali wafanye.

Ukiondoa kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, simjui kiongozi mwingine yeyote wa umma aliyeweka tangazo lake la mali na madeni hadharani. Hii ni pamoja na walioko serikalini na upinzani pia.

Kushindwa kuweka hadharani matamko yao ya mali na madeni ni miongoni mwa viashiria vingine kadhaa vinavyoonyesha jinsi vyama vya siasa vinavyoendesha mambo yao gizani na kwa kificho.

Ingawaje msemaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent anasema ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa kila mwaka hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, hii haiviondolei vyama vya siasa ulazima wa kuendesha mambo yao ya fedha kwa uwazi.

Zaidi ya mara moja kumesikika manung’uniko miongoni mwa wanachama wa vyama vya siasa kuhusu uwajibikaji wa kifedha wa vyama na viongozi wao.

Kwa teknolojia za habari na mawasiliano zilizopo sasa vyama vya siasa vina uwanja mpana wa kuzibadilisha taasisi zao kuwa wazi zaidi na wajibikaji kwa wanachama na wafuasi wao.

Teknolojia hizi huvipatia vyama vya siasa majukwaa kama vile tovuti na mitandao ya kijamii ambayo kama itatumiwa vizuri si tu itaboresha uwazi wao bali pia itaboresha mahusiano yao na wanachama au wafuasi wao.

Kwa bahati mbaya, hali haikuwa hivyo katika vyama vingi vya siasa.

Kwa mfano, Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, hakina tovuti ya kujitegemea isipokuwa blogu ambayo haimsaidii mtu yoyote atakayeonyesha nia ya kutaka kukifahamu chama na uwajibikaji wake kwa jamii.

Ingawaje Chadema kinatumia mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter, taarifa zinazosambazwa na chama hicho katika majukwaa haya haziakisi uwazi na uwajibikaji wa chama chenyewe badala yake taarifa nyingi hujikita na matukio na habari za viongozi wao.

Chama cha Wananchi (CUF) licha ya kwamba kina tovuti na kipo kwenye mitandao ya kijamii, mara ya mwisho kutumia majukwaa haya ilikuwa Oktoba 2015 kabla ya uchaguzi mkuu. Ni kama vile kilianzisha tovuti na kuingia Facebook kwa ajili ya uchaguzi tu.

Hali ni hivyo hivyo kwenye chama cha ACT-Wazalendo ambacho website yake mpaka sasa inamtambua Anna Mghwira kama mwenyekiti wa chama na Profesa Kitila Mkumbo kama mshauri wa chama. Wawili hawa walishajiuzulu nafasi zao na wamehamia CCM.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa Msemaji wa CUF, Mbarara Maharagande, msemaji wa Chadema Tumaini Makene amekanusha kama wanaendesha masuala yao ya kichama bila kuwapo uwazi wa kutosha.

Kwa nyakati tofauti, wamebainisha kuwa wao kama vyama vyama vya upinzani wanauishi uwazi na kwamba hawajawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa mtu yoyote iwe ni mwanachama au mfuasi wa vyama vyao.

Wasemaji hao wanasema kama ni hesabu za matumizi zinakaguliwa na wakaguzi wa ndani na nje na ripoti zao hujadiliwa katika vikao rasmi vya chama katika ngazi zote ambako wanachama wanaweza kufanhamu chama kinaendesha vipi mambo yake.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema uwazi ndio msingi unaojenga chama chao. Amesema tovuti yao kwa sasa ipo chini ya matengenezo, lakini ikikamilika taarifa zote kuhusu chama zitapatikana huko.

Alipoulizwa kama ofisi ya msajili inaridhishwa na jinsi vyama vya siasa vinavyoendesha masuala yake kwa uwazi, Monica anasema hawezi kusema ndiyo wala hapana.

Anabainisha kuwa kinachowahusu wao ni vyama vya siasa kuendesha mambo yao kwa mujibu wa katiba na huingilia tu kama kutakuwa na ukiukwaji katika suala hilo.

“Naweza kuwa najua kuna manung’uniko yanaendelea kuhusu ni namna gani vyama vya siasa vinatumia ruzuku zao, lakini hakuna aliyeleta malalamiko rasmi kwetu na hivyo hatuwezi kuingilia.”

Kwa upande wake, Mbunda anasema vyama vya upinzani visipokuwa makini na kurekebisha hili vinaweza kukumbwa na “msukosuko wa uhalali”.

Dk Salim anatahadharisha kuwa kama hali itaendelea kama ilivyo kitakachotokea ni kifo cha demokrasia.

“Hutegemei vyama vinavyopigania demokrasia kwenda kinyume na misingi ya demokrasia,” anasema.

0716 874 501