Friday, May 18, 2018

UCHAMBUZI: Hatuhitaji darasa kuwapa wagonjwa tabasamu

Rais John Magufuli akiwajulia hali wagonjwa

Rais John Magufuli akiwajulia hali wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Picha na Maktaba 

By Florence Majani

Unaingia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ukiwa hoi, maumivu ya tumbo ni makali na mwili wako wote hauna nguvu.

Unapokewa na kuingizwa katika chumba cha matibabu. Unakutana na muuguzi anayeanza kukufokea, amekunja ndita usoni na analalamika mfululizo. Hapana shaka maumivu yako yatazidi.

Lakini inakuwaje basi pindi unapokuwa katika hali ya maumivu makali na ukakutana na muuguzi anayekupa tabasamu huku akikutia moyo kuwa utapona? Hakika neno hilo la faraja na tabasamu lake, vitakupa ahueni.

Tabasamu ni sehemu ndogo tu ya wajibu wa muuguzi lakini yenye umuhimu mkubwa kwa afya ya mgonjwa.

Mei 12, dunia iliadhimisha siku ya wauguzi duniani na malengo makuu ya siku hiyo ni kuukumbuka wajibu wa wauguzi duniani.

Tunapozungumzia wauguzi, hatuwezi kumtenga mwasisi wa taaluma hiyo, Florence Nightangle. Wauguzi huadhimisha siku hii wakiikumbuka siku ya kuzaliwa kwa Nightngale Mei 12, mwaka 1820, huko Italia.

Nightagle alijitolea kwa moyo, kuwauguza majeruhi wanajeshi wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Nightangle atakumbukwa kwa ukarimu wa hali ya juu aliowanyesha wanajeshi hao. Aliifanya kazi hiyo kwa huruma bila kujali malipo. Kama tunamuasisi Nightangle, basi tuyakumbuke na yale aliyoyafanya. Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mengi ya wagonjwa wanaodai kutolewa lugha chafu au hata kusukumwa na wauguzi.

Baadhi wamedai kukumbana na matusi wanapolalamika au hata kuachwa wakiwa wamejisaidia usiku kucha.

Haya na mengine mengi, yameitia doa taaluma hii adhimu ya uuguzi.

Yapo mengi mazuri yanayofanywa na wauguzi nchini, lakini haya machache yanayolalamikiwa mara kwa mara ni vyema yakaepukwa.

Wauguzi wanapokwenda kusomea taaluma hii na wanayo mengi ambayo wanafundishwa, lakini suala la tabasamu na ukarimu kwa mgonjwa halihitaji darasa bali ni ukarimu na upendo unaojengwa kutoka katika wito wa kazi hiyo.

Pasipo ukarimu, muuguzi hataifanya kazi yake kwa mafanikio kwani huenda akawa chanzo cha kudorora kwa afya ya mgonjwa. “Neno la faraja moja tu kwa mgonjwa, huweza kuchagiza uponyaji wake.” Hivyo ndivyo, Florence Nightngale alivyosema.

Kadhalika, Nightngale alisema, “hakuna binadamu, au hata daktari anayeweza kutoa tafsiri ya muuguzi anavyotakiwa kuwa zaidi ya kujitoa na uvumilivu.”

Hata katibu tawala wa Mkoa wa Tanga, Zena Saidi aliwahi kuwaasa wauguzi akisema, “wauguzi hamhitaji kupewa kozi ya namna ya kutabasamu kwa wagonjwa wenu kwa sababu kozi kama hiyo sijasikia ikitolewa mahala popote, akini tabasamu la muuguzi humpa moyo wa kupona mgonjwa.”

Tusifikie mahali wagonjwa wakaamua kuacha huduma za afya zinazotolewa katika hospitali zetu kwa kuhofia matusi na mkong’oto. Ni lazima tujenge mazingira rafiki kwa wagonjwa ili hospitali, vituo vya afya na zahanati viwe maeneo yanayompa faraja mgonjwa.

Hakuna haja ya akina mama kukimbilia kwa wakunga wa jadi wakihofia kutukanwa na wauguzi, bali hospitali liwe kimbilio la kwanza.

Wakati huohuo, ni vyema Serikali ikazifanyia kazi changamoto wanazokumbana nazo wauguzi kwani nao wanakabiliwa na mengi ikiwamo uhaba wa vifaa.

Juzi wakisoma risala yao wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, wauguzi mkoani Tanga walisema hawajalipwa stahiki zao.

Mishahara kiduchu na rasilimali kazi ya uchache wao huenda ni sehemu ya sababu zinazowafanya baadhi yao kukosa morali ya kazi hata kuwasababishia hasira wawapo kazini.

Ni matumiani yangu Serikali itachukua hatua madhubuti kutatua kero zao, lakini kubwa na la muhimu ni wauguzi kujenga tabasamu usoni mwao.

-->