Mwasho unavyoweza kusababishia matatizo ya akili, msongo wa mawazo

Kuwashwa ngozi ya mwili ni moja ya tukio ambalo linalosababisha kujikuna ili kukabiliana na hisia hiyo ya kukereketa lakini kumbe pia kufanya hivyo kunaweza kuongeza makali ya kuwashwa zaidi.

Ni kawaida kadiri mtu anavyojikuna, mwasho nao huongezeka na hivyo kumfanya aongeze kasi ya kujikuna zaidi kiasi cha kujijeruhi na kupata michubuko au vidonda.

Wanadamu hupata hili hiyo na hutumia kucha zao au kujiegemeza mahali kwenye kitu au kutumia hata kibanzi ili tu kujikuna. Unapojikuna wengine hupata hisia nzuri au maumivu ama kupata vyote.

Kuwashwa katika ngozi ya mwili ni kitu kinachomfanya mwanadamu kukosa utulivu kutokana na kero anayopata. Hutokea mwanadamu kukumbwa na mwasho wa hata kuaibisha ikiwamo ule wa sehemu za siri.

Lakini wataalamu wanasema tatizo la kuwashwa linaweza kumwathiri mtu kiasi cha kumsababishia matatizo ya kiakili ikiwamo kujitenga, kutojiamini mbele za watu, kuwa na aibu, huzuni na sonona.

Tatizo la kuwashwa mwili linaweza kuwa ni la muda mfupi tu na likaisha, lakini inapotokea tatizo likawa la mara kwa mara kwa zaidi ya siku 14, maana yake limekuwa sugu.

Kuwashwa pia kunaweza kuambatana na hali ya kupata viuvimbe, vimiinuko kama mawimbi au vipele katika ngozi kutegemeana na chanzo.

Na wakati mwingine muathirika hujikuta hata rangi ya mahali panapomuwasha, huweza kubadilika rangi na kuwa pekundu.

Kwanini kuwashwa mwili

Kuwasha ngozi ya mwili inaweza kuwa ni dalili ya uwapo wa maradhi yanayoleta mapele au kubabuka ngozi na vile vile inaweza kuwa ni dalili ya kuwapo kwa maradhi ya figo na ini.

Viko vitu mbalimbali ambavyo mara kwa mara huchangia kujitokeza kwa hali ya muwasho ambayo huweza kuwa na asili ya kemikali, vimelea, vumbi, mazoa ya wanyama, vyakula na dawa.

Nikianza na tatizo la ukavu wa ngozi ambalo kitabibu linaitwa ‘Xerosis’. Hili husababishwa na matokeo ya vitu vilivyomo katika mazingira yakiwamo ya hali ya hewa ya joto au ya baridi.

Mfano mtu akitumia kiyoyozi kwa muda mrefu au kuoga maji, kunaweza kuleta ukavu katika ngozi na kusababisha mwasho

Sababu ya pili ni maradhi ya ngozi na yale yanayoleta mapele ikiwamo ukurutu, vipele vya tete maji, shambulizi la ngozi na mba au fangasi.

Mengine ni maradhi ya ogani za ndani ya mwili kama zikishindwa kufanya kazi, husababisha mwasho. Ogani hizo ni pamoja na ini na figo. Kama zikishindwa kufanya kazi, zinaweza kusababisha mrundikano wa taka sumu zinazoweza kusababishwa mwili kuwasha.

Vile vile maradhi ya saratani, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na maradhi ya tezi ya shingo, pia yanaweza kuleta mwasho.

Pia, kuathirika kwa mishipa ya fahamu, inaweza kusababisha mtu kupata hali ya mwasho, mfano wagonjwa wakisukari na mkanda wa jeshi, huharibu mishipa ya fahamu na kuwafanya wapate hisia za kuwasha.

Vitu kama nguo, kemikali, sabuni tunazoogea, mafuta, krimu, vipodozi na vumbi, pia vinaweza kuleta uchokozi na kusababisha kutokea kwa mzio (allergy).

Mzio hutokea baada ya mwili kuchokozwa na kujibu mapigo na kutiririsha kemikali za mfumo wa kinga zinazosababisha kuwasha.

Vile vile mtu anaweza kupata mzio baada ya kula vyakula, mfano vyakula vinavyoongoza kuleta hali kama hizi ni pamoja na mazao ya baharini na jamii ya karanga.

Kuhusu dawa na wajawazito

Baadhi ya dawa za antibayotiki, fangasi, malaria na za maumivu zinaweza kuwa na madhara madogo ikiwamo ya kumsababishia mtu mwasho na vipele.

Hali ya kuwa ujauzito huleta mabadiliko ya kimwili yanayoweza kuchangia wajawazito kupata mwasho hasa katika maeneo ya tumboni, mikononi, mapajani na katika matiti.

Kukabiliana na mwasho

Ikumbukwe unaweza ukapata mwasho na kutumia kasi na nguvu kujikuna mpaka kusababisha michubuko katika ngozi ambayo inaweza kuleta majeraha na kukaribisha uvamizi wa vimelea mwilini.

Hivyo, ni vizuri kuepuka kujikuna na badala yake tumia matibabu salama ya nyumbani ambayo huandaliwa na vitu ambavyo tunavyo katika sehemu tunazoishi.

Maji safi na salama ya bombani ni moja ya tiba salama ya mwasho, unaweza kutumia maji yanayotiririka na kuyalengesha katika eneo lenye mwasho.

Au tumia bomba la mvua la kuogea kujimwagia mwilini kama mwasho uko sehemu kubwa ya mwili. Vile vile unaweza kutumia kitambaa au taulo safi na kulichovya katika maji kisha weka panapowasha.

Maji yanasaidia kuondoa vitu vilivyoshikamana na ngozi vinavyosababisha kuwasha, vile vile maji hupoza mwasho katika ngozi na kufifisha kukereketa.

Njia ya pili ni kutumia magadi soda kwa kuyachanganya na maji na kumwagia kwa wingi sehemu inayowasha au kuyaoga maji hayo.

Magadi yanasaidia kupunguza makali ya mlipuko wa kinga ya mwili ambao hutiririsha vitu vinavyochangia kuwashwa.

Namna ya kuyatumia

Tumia kijiko kimoja cha magadi katika ndoo ndogo ya maji, unaweza kuweka maji hayo kwa dakika kumi katika eneo linalowasha, fanya hivyo kwa siku mara moja.

Njia ya tatu ni Maji yaliyowekwa chumvi. Hayo husaidia kupunguza makali ya mwasho puani uliotokana na mzio au mafua wakati wa baridi ambao huambatana na kupiga chafya na mafua wakati wa baridi.

Changanya chumvi robo kijiko na nusu lita ya maji ya uvuguvugu na kukoroga kisha dondoshea matone kadhaa ukiwa umelaza kichwa upande mmoja, ili maji hayo yatokee tundu la pili la pua. Badili upande mwingine kwa kufanya hivyo hivyo.

Maji yenye chumvi yanasaidia kupunguza mwasho au waliopata mzio puani uliosababishwa na baridi au mzio kwa asilimia 50.

Njia ya nne ni matunda yenye tindikali asili ya Citric na Acetic ambazo zina uwezo wa kukata makali ya mwasho, kuzuia kukereketa kwa ngozi na kuweka ganzi.

Unaweza kuchukua ndimu au limao moja au mawili na kuyakamua juisi yake. Tumia pamba kwa kuchovya kwenye juisi hiyo na kupaka eneo lenye mwasho, fanya hivyo mara mbili kwa siku.

Vile vile unaweza kutumia siki itokanayo na tunda la epo ambayo imetengenezwa viwandani kwa ajili ya kiungo katika chakula.

Siki ina tabia ya kuondoa makali ya mwasho kama ilivyo kwa limao na ndimu.

Ushauri, kama njia hizi zisiposaidia ni vizuri kufika katika huduma za afya mapema kwa ushauri zaidi.