PIRAMIDI YA AFYA: Sababu mwanamke kutoka uchafu mweupe sehemu za siri

Kila mwanamke anapaswa kujichunguza kila siku ya maisha yake maeneo yake ya uzazi na matiti, vile vile kuichunguza nguo ya ndani aliyokuwa ameivaa siku hiyo kama kuna uchafu wowote.

Kufanya hivi kunaweza kumsaidia kugundua kuwa ana tatizo la kiafya. Nasema hivi kwani wapo baadhi ambao hawafahamu kuwa kila siku huwapo ute ute unaomtoka amabo ni hali ya kawaida.

Ute huo unaweza kuwa na ujazo wa nusu kijiko cha chai na huwa na harufu asilia ya uke na huwa na rangi nyeupe au kahawia mpauko kama chai isiyokolea rangi bila kuwa na harufu mbaya.

Utokaji wa ute huo ni mojawapo ya njia ya uke kujisafisha kwa kutiririka pamoja na mabaki ya hedhi au takataka za mwili au zilizotoka nje ya mwili.

Ute huu huzalishwa na kuta za nyumba ya uzazi na huzifanya tezi za ukeni kushuka chini kutokana na kani ya nguvu za uvutano (gravity).

Kutokwa na uchafu mweupe au wa kijivu ulio kama maziwa ya mgando ukeni ni tatizo la kiafya, ni dalili mojawapo ya ugonjwa wa fangasi za ukeni kitabibu hujulikana kama Vaginal Candidiasis.

Inakadiriwa katika maisha yao ya kila siku, wanawake karibuni wote wana historia ya kuwahi kuugua tatizo hili.

Tatizo hili halipo katika makundi ya maradhi yatokanayo na kujamiana (STI), ingawa kugusana kwa kujamiana kunaweza kusambaza. Hata wanawake ambao hawashiriki tendo la kujamiana wanapata tatizo hili.

Kwa kawaida uke wenye afya njema huwa na bakteria rafiki na kiasi cha seli za fangasi (yeast cells), inapotokea mabadiliko ya usawa wa vimelea hawa wa fangasi huanza kujistawisha na kuzaliana.

Hali hii huweza kuleta viashiria na dalili za mwasho, kuvimba na kukereketa. Kutoka uchafu mweupe kama maziwa ya mgando na mwasho huwa ni ndani au nje ya uke, uchafu huo huweza kuwa na harafu mbaya.

Mashavu ya uke kuvimba, kupata hisia za kuwaka moto wakati wa kukojoa au kujamiana, maumivu wakati wa kujamiana, michubuko, tishu za ukeni kuwa nyekundu, kutoka vidonda na vipele, hizo zote ni dalili.

Tatizo hili linawapata wanawake mara kwa mara kutokana na maumbile ya uke yalivyo, huwa ni ya unyevu nyevu hivyo mfumo wa ulinzi wa uke huweza kuharibiwa na kuwapa nafasi fangasi kustawi.

Tunashauri wanawake kuepuka kutumbukiza kitu chochote ukeni ikiwamo kuweka kemikali, manukato au vifaa vya plastiki, lengo ni kulinda mazingira ya ukeni yasiharibike ili bakteria rafiki walinzi waendelee kuwadhibiti fangasi.

Mambo mengine ambayo yanayochochea tatizo hili ni ujauzito, mabadiliko ya hali ya hewa (joto kali), mabadiliko ya viwango vya vichochezi vya kike (hormones), dawa za matibabu (antibiotiki), ulaji ovyo wa vyakula vya sukari, kutokuwa msafi kimwili na kutolala.

Vile vile kuwa na maradhi ya akili (msongo wa mawazo na sonona), maradhi sugu ikiwamo kisukari na yanayopunguza kinga mwilini (Mfano VVU, saratani na lishe duni).

Ni kawaida tatizo hili likawa la muda likaisha lenyewe bila dawa yoyote au linaweza kuwa tatizo sugu linalodumu zaidi ya wiki mbili au likatibiwa na dawa mara kwa mara likawa linajirudia rudia.

Kwakuwa katika hatua za awali ni rahisi kutibiwa na kupona, ni vizuri kufika mapema katika huduma za afya pale unapoona dalili na viashiria nilivyovitaja hapo awali.