Kemikali ya zambarau huzuia shinikizo la damu

Wataalamu wa masuala ya Lishe wanashauri kuwa sharubati ya matunda halisi bila kuweka sukari ina faida nyingi kwa afya ya mwili na akili. Pia, sharubati ya matunda na mbogamboga husaidia kuzalisha mkojo kwa wingi ambao huondoa sumu mwilini, kusafisha damu na kuongeza maji mwilini.

Matunda yakiwamo ya zambarau, embe, pera, tufaa, zabibu na stawberries, hutengeneza virutubisho mwilini kutokana na ukweli kwamba huliwa na ngozi zake na hiyo ni kutokana na mwanga wa jua ambao hutengeneza virutubisho mwilini ambavyo ni muhimu katika kuimarisha ulinzi wa afya ya binadamu.

Kwa upande wa zambarau ambalo ni tunda la msimu, likitumika vizuri, huweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata shinikizo la damu.

Hata hivyo, tunaelezwa kuwa zambarau ina kemikali ya asili iitwayo anthocyanins ambayo pamoja na mambo mengine, husaidia kukulinda dhidi ya shinikizo la damu. Kwa wale wasiofahamu zambarau, zina fanana na zabibu lakini tofauti iliyopo, zabibu haina kokwa, wakati zambarau ina kokwa kubwa. Wataalamu wa Masuala ya Lishe , wanasema njia bora za kupunguza shinikizo la damu ni kula vyakula vinavyosaidia mishipa itanuke ili kuufanya moyo usiweze kufanya kazi kupita kiasi.

Faida nyingine ya tunda hili katika mwili wa binadamu ni pamoja na kusaidia kumpa nafuu mgonjwa wa kisukari. Kwa matokeo mazuri, badala ya kuziosha vizuri kwa maji safi na salama na kisha kuzila, sasa unaweza kuzichemsha zambarau kwa muda usiopungua dakika 20, kisha ziipue na ziache zipoe.

Zikishapoa, zitoe mbegu huku ukizikamua kamua kwa kutumia mkono na baada ya hapo chuja ili uweze kupata sharubati au juisi ambayo unaweza kuongeza sukari na ndimu kama utapenda.

Baada ya hapo, unaweza kuiweka kwenye friji ili iweze kupata baridi na baada ya muda unaweza kushushia kinywaji chako na chakula chochote unachopenda.

Mbali na juisi, pia unaweza kukausha mbegu za zambarau na kisha kuzisaga ili kupata unga laini, ambao unaweza kuutumia kila siku asubuhi kabla ya kula chakula chochote kwa kuchanganya nusu kijiko cha unga huo katika glasi moja ya maji na kunywa.