Mwanga wa matumaini chanjo ya ebola huu hapa

Wataalamu wa afya duniani wamekuna vichwa na kupiga hatua. Wametoa mwanga wa matumaini kwa wananchi wengi.

Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) huenda sasa wakaanza kupepesa macho na kuvuta pumzi kwa furaha baada ya maofisa wa afya kuanza kutoa chanjo katika mji wa Mbandaka uliokumbwa na visa vya ugonjwa wa ebola.

Kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo ni matokeo ya juhudi za muda mrefu zilizowagonganisha vichwa wataalamu kutoka kona mbalimbali duniani.

Chanjo hiyo ilidhibitika kuwa sasa ni madhubuti kuanza kutumika baada ya kufanyiwa ukaguzi kwa muda wa miaka miwili kabla ya wataalamu hao kuja na kauli moja itumike. Majaribio hayo yalipata nguvu zaidi mwaka 2014 wakati ugonjwa huo ulipozikumba nchi kadhaa za Afrika Magharibi na kusababisha watu zaidi ya 11,000 kupoteza maisha.

Kufikia sasa, watu 25 wamethibitishwa kufariki dunia tangu ugonjwa huo ulipozuka mwishoni mwa Aprili huko Congo. Chanjo hiyo imekuwa ikitolewa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Serikali ya Congo.

WHO ilisema makundi ya kwanza kupatiwa chanjo hiyo ni wahudumu na baadaye itasambazwa kwa wananchi katika eneo ambalo virusi hivyo vimeripotiwa kuibuka.

Ugonjwa wa ebola unatajwa kuwa ni miongoni mwa magonjwa hatari duniani na mara nyingi husababisha vifo vya ghafla. Ripoti zinasema idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na maradhi ya nchini Congo imeongezeka hadi watu 27.

Wizara ya Afya ya Congo imesema kumeripotiwa kifo kimoja zaidi katika eneo la Wangata mjini Mbandaka ambako ndiko ulikozuka kwa mara ya kwanza mwaka huu. Kufikia sasa kuna visa 51 vya ebola vilivyoripotiwa nchini humo tangu mlipuko huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza na kati ya visa hivyo 28 vimethibitishwa.

Kuzuka kwa ebola kunasababisha kujaribiwa kwa chanjo mpya ya ugonjwa huo ambayo ilionekana kufanya kazi vyema Afrika Magharibi miaka michache iliyopita. Zaidi ya vipimo 4,000 vya chanjo hiyo vimewasili nchini Congo wiki hii huku vipimo zaidi vikitarajiwa kufika.

Changamoto kuu itakuwa kuiweka chanjo hiyo katika hali ya baridi katika eneo ambalo lina miundo mbinu duni na umeme katika sehemu chache.

Tangu mwaka 1976, huu ni mlipuko wa tisa wa ebola nchini Congo hali ambayo imewafanya wataalamu waanze kuna vichwa vyao mara mbilimbili.

Virusi vya ugonjwa huu vinasambazwa kwa watu kutoka kwa wanyama wa porini wakiwemo popo na tumbili. Hadi sasa wakati wataalamu wakiendelea kutoa chanjo hakuna tiba maalum ya ugonjwa huo.

Dalili zake ni homa, kutapika, kuharisha, maumivu ya misuli na wakati mwingine kuvuja damu ndani na nje ya mwili. Ebola inaweza kusababisha vifo katika asilimia 90 ya visa.

Duru za habari zinasema chanjo hiyo inatarajia kupanuliwa zaidi kuanzia leo huku watu 600 wakilengwa kupatiwa. Hata hivyo, shirikisho la msalaba mwekundu limeonya kuwa bado mlipuko huo haujadhibitiwa kikamilifu na kusisitizia jamii kuwa waangalifu na kuwazika watu waliokufa na ugonjwa huo kwa njia salama ili kuepuka maambukizi zaidi.

Ugonjwa umesambaa kutoka maeneo ya mashambani hadi katika mji wa Mbandaka, ambao ni kitovu muhimu cha shughuli za uchukuzi katika maeneo yanayounganisha Mto Congo. Jambo hilo linadaiwa kuongeza wasiwasi kwamba huenda maradhi hayo yakasambaa hadi katika mji mkuu Kinshasa au nchi jirani.

Hata hivyo, shirika hilo limeeleza imani yake kwamba ugonjwa huo utadhibitiwa.“Tuna imani kwamba hali hii itakabiliwa ili kutoleta madhara zaidi,” lilisema kwenye taarifa.

Juzi, Naibu Waziri, Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile alisema hadi sasa Tanzania bado haijakumbwa na virusi vya ugonjwa huo na akaahidi kuendelea kuongeza udhibiti katika maeneo ya mipakani.

Tangu wiki iliyopita mikoa ambayo imepakana na Congo, ikiwemo Kigoma, Katavi na Rukwa wananchi wanaingia nchini kupitia maeneo hayo yamekuwa wakifanyiwa uchunguzi ili kubaini kama wameambukizwa maradhi hayo.

Katika mkutano wa dharura uliofanyika baada ya kuzuka kwa ugonjwa huo wataalamu wa WHO walisema hali ebola nchini Congo haijafikia ya kuutangaza “janga la kimataifa”.

Tayari, kamati yake ya huduma za dharura imetoa ushauri maalum kwa serikali ya taifa hilo kuendelea kushirikiana ili kuimarisha mikakati ya kukabili maenezi ya ugonjwa huo. “Bila ushirikiano wa kutosha, kuna hatari kwamba hali hii itakuwa mbaya zaidi,” ilionya kamati ya wataalamu wa WHO kupitia taarifa yake iliyotolewa baada ya mkutano wa dharura.

Aidha, kamati pia imetoa wito kwa jamii ya kimataifa, wanasayansi na wataalamu wa afya kushirikiana ili kutoa habari muhimu zitakazosaidia kupatikana kwa tiba yake.

Wataalamu wa WHO wamesema hatua za haraka zimeweza kuzuia kuenea kwa mlipuko huu mpya uliotangazwa siku 12 zilizopita.

Chimbuko la virusi vya ebola

Virusi vya ebola ni vidogo kiasi kwamba ni vigumu kuweza kuonekana kwa macho ya kawaida. Vinaweza kuonekana kwa njia ya darubini vikionekana kama uzi pindi vinapochunguzwa na chombo hicho.

Virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976 na watafiti wa magonjwa katika kijiji kimoja katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire).

Virusi hivyo vilipewa jina la ebola kuashiria jina la mto unaopakana na kijiji hicho, ambao ni Mto Ebola. Baadaye kulizuka milipuko mingine mitatu nchini humo na pia chini Sudan katika miaka ya 1970.

Baadaye virusi hivyo vilipotea hadi mwaka 1994 wakati ugonjwa huo ulipozuka tena. Kuzuka kwa ugonjwa wa ebola nchini Gabon, ndio ulikuwa mwanzo wa kusambaa kwa virusi hivyo hadi katika mataifa mengine ya Afrika Magharibi.

Hadi sasa ugonjwa huu wa ebola umezuka mara 20 ingawa mara nyingi umekuwa ukidhibitiwa. Wakati wote huo ugonjwa huu ulipozuka, idadi ya watu walioambukizwa haikuwa kuzidi 430.

Mara ya mwisho ebola ilizuka nchini Guinea mwaka 2013 na kisha kwa haraka ulisambaa hadi nchini Sierra Leone na Liberia ambako watu 11,000 walifariki dunia na wengine zaidi ya 10,000 kuambukizwa virusi hivyo. Ugonjwa huu sasa umetangazwa kuwa janga katika mataifa hayo.

Mojawapo ya sababu zinazotajwa kuchangia kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huu wa ebola, ni kwamba mwanzoni mataifa yaliyoathirika na hata jamii ya kimataifa ilipuuza uzito wa janga hili.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa huo katika mataifa ya Afrika Magharibi, juhudi za kupata dawa ya kuutibu zimeimarishwa kote duniani. Shirika la Afya Duniani (WHO) lina matumaini ya kutoa chanjo kwa maelfu ya watu wanaoishi katika mataifa yanayoathirika zaidi na ugonjwa huu kufikia katikati ya mwaka 2019. Hata hivyo hilo halikufanikiwa mpaka chanjo hiyo ilipobidi kusubiri kwa muda wa miaka kadhaa ikiendelea kufanyiwa majaribu.

Awali WHO ilikadiria kuwa kufikia mwishoni mwa mwaka huo wa 2015 lingekuwa limetoa chanjo kwa watu milioni moja dhidi ya ugonjwa huo.

Kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo nchini Congo kumeleta matumaini siyo tu kwa taifa hilo bali hata kwa mataifa jirani yaliyoanza kujihami na maambukizi yake.