KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Uandishi wa habari ni ukweli unaowasilishwa kwa usahihi bila kupotoshwa

Wasomaji 21 wa gazeti hili wameomba Mhariri wa Jamii achapishe hotuba yake aliyotoa tarehe 12 mwezi huu, jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kutoa Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari (EJAT) kwa kazi za mwaka 2017. Mhariri wa Jamii alikuwa Jaji Kiongozi wa majaji wanane waliofanya uamuzi wa kitaaluma.

Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo iliyohaririwa.

Mgeni rasmi, Profesa Issa Shivji, hapa leo, ndipo jopo la majaji linapohitimishia kazi liliyopewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na wadau wake.

Niseme tu kwamba, tumefanya kazi tuliyotumwa na tumeikamilisha.

Natoa shukrani za dhati kwa majaji wote kwa pamoja, na jaji mmoja mmoja, kwa ushirikiano uliowezesha kazi hii kukamilika katika muda uliopangwa.

Mgeni rasmi, uandishi wa habari ni zaidi ya kupashana taarifa. Jukumu la kupashana taarifa ni la kila mmoja aliyehai na katika mazingira ya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kuwa na mawazo na uhuru wa kutoa maoni.

Teknolojia imeleta fursa kwa watu wengi kuwasiliana kwa njia ya simu ya kiganjani na mitandao ya kijamii; na kupashana taarifa.

Lakini uandishi wa habari unabaki kuwa uandishi wa habari – kwa kusomea, kwa kufunzwa kazini, kwa maelekezo mbalimbali, kwa kufundwa kimaadili na kwa misingi yake – ikiongozwa na msingi mkuu: ukweli unaowasilishwa kwa usahihi.

Ni katika muktadha huu, majaji walitafuta habari na siyo taarifa.

Walifanya hivyo kwa kuzingatia kwamba shabaha ya kushindanisha waandishi wa habari ni kukuza elimu, maarifa, stadi, mbinu, kuimarisha misingi ya uandishi na kujenga umahiri (weledi).

Bali umahiri hauji baada ya kuandika na kuchapisha andiko – katika gazeti, kusomwa redioni na au kuonyeshwa katika televisheni, katika kupiga picha na katika kuchora katuni. Hapana.

Umahiri huandaliwa; kuanzia kupata wazo la kufuatilia, malengo yake, mipango, matarajio yake, umuhimu wa kinachofuatiliwa, ukusanyaji taarifa, utafiti, uchambuzi, uthibitishaji; na kwa kuandika kwa usahihi na katika lugha inayoeleweka; au kuchora wazo na maana yake (katuni); na siyo tu kuchora picha.

Nyuma ya mwandishi kuna mwelekezaji; muite mhariri, msanifu wa habari au menta.

Huyo ndiye anaona kazi ya mwandishi wa habari na anayepaswa kuibua kasoro, kumhoji, kuziba mapengo na kuelekeza jinsi ya kufuma andishi lisiloacha maswali.

Huyo pia ndiye awezaye kukomaza mazingira ya kushindana na kushinda; lakini pia kudhihirisha kuwa uandishi wa habari ni kazi ya ufundi na ya maana katika jamii.

Lakini majaji wameona mawazo mazuri yaliyoibuliwa na waandishi; ambayo yameandikwa kijuujuu; haraka na harakaharaka; yaliyokosa vielelezo na ushahidi; yaliyoandikwa na kuwasilishwa katika redio na televisheni bila mpangilio kitaaluma na yaliyokosa weledi wa kuyatupia jicho kabla ya kuchapishwa au kutangazwa.

Kazi nyingine hazikuwa zimefuata vigezo na masharti ya MCT.

Ni hatua hii inayoibua umuhimu wa MCT na wadau wake, kupeleka mrejesho kwa wenye vyombo vya habari, wahariri na washindani wengine, juu ya kilichojiri wakati wa “kuhukumu” kazi zao.

Hakika wanastahili kujua walianguka wapi na kwanini. Hili limependekezwa na Jopo la Majaji.

Aidha, wiki iliyopita nilikutana na Katibu Mtendaji wa MCT na kumhakikishia kuwa mimi na majaji wawili wengine, tuko tayari kutoa mrejesho kwa wahusika walioko Dar es Salaam; kwa kutembelea vyombo vyao vya habari au kukutana nao ukumbi wa MCT. Ameonekana kufarijika. Ninatumaini atafuatilia.

Hatua kama hizi ndizo zinafanya jukumu la MCT na wadau wake, liwe na lionekane kuwa, la kukuza weledi na siyo kushindanisha tu waandishi wa habari.

Kuna haja pia ya MCT kuandaa utaratibu wa kufikia walioko mikoani.

Maeneo matatu ambako MCT inapaswa kuwasisitizia washindani kujikita ni kategoria ya Kodi na Ukusanyaji Mapato; kategoria ya Kilimo na Kilimo Biashara na kategoria ya “uandishi wa habari wa kutumia data.”

Maeneo haya hayahitaji kuripoti tu, bali hasa kufanyia uchunguzi na uchambuzi kutokana na umuhimu wake kwa taifa; na kutokana na kuwa maeneo mahususi ya kupimia na kupima uwajibikaji.

Uandishi wa “kutumia data” – ambao unatumia tarakimu na grafu ili kuelezea hoja kwa ubora na wepesi zaidi; na kujenga muktadha wa unachoandika, ndiyo njia bora ya kuripoti na kuchambua; lakini bado waandishi wengi wa habari hawajamiliki matumizi yake. Kuna haja ya kujifunza zaidi.