Mambo manne yanayomfanya bosi aaminiwe na wafanyakazi

Mojawapo ya sababu zinazotajwa kuchangia utendaji hafifu katika maeneo ya kazi ni ari duni miongoni mwa wafanyakazi. Ingawa mara nyingi viongozi hurusha lawama kwa wafanyakazi wao, lakini wafanyakazi hawa nao kwa upande wao huwalaumu viongozi wao kwa kushindwa kuweka mazingira yanayowafanya wawe na ari ya kufanya kazi.

Namna moja ya kuongeza ari ya wafanyakazi ni imani wanayokuwa nayo kwa kiongozi wao. Mfanyakazi asiye na imani na kiongozi wake, huishi kwa tahadhari ya hali ya juu, huogopa kukosea na kutoa mawazo chanya na wakati mwingine husita kujaribu mambo mapya ambayo pengine yangefanyika yangesaidia taasisi au kampuni kupata mafanikio.

Katika makala haya tunajadili umuhimu wa kiongozi kuamika kwa wafanyakazi wake kwa kupendekeza maeneo manne yanayoweza kumfanya kiongozi wa taasisi au kampuni kuaminiwa.

Kujali utu wa unaowaongoza

Binadamu, kwa asili yake, anahitaji kubwa la kuheshimiwa. Heshima kwa utu wake ndiyo inayochochea imani yake kwa mtu mwingine.

Katika mazingira ambayo hamwamini mtu, ni vigumu kujibidiisha kutumia vipaji vyake kwa manufaa ya taasisi au kampuni anayoifanyia kazi.

Kwa maana hiyo, kiongozi makini ana kazi ya kufanya jitihada za makusudi kuonesha anawajali wafanyakazi wake.

Hili linaanzia kwenye uelewa kuwa watu hawawezi kuwa sawa na mitambo inayoendeshwa bila kujali hisia na mahitaji yao.

Kiongozi makini anapojali hisia za watu anaowaongoza, kwa kawaida, huwa na mguso chanya unaoweza kuwa sababu ya mabadiliko makubwa katika eneo la kazi.

Kiongozi anayejali utu wa watu anaowaongoza hufurahia kushughulika na mahitaji yao. Hutengeneza mazingira mazuri ya watu wake kujisikia huru kumfikia kirahisi na kumueleza changamoto zao za kikazi na zile binafsi. Nakumbuka dada mmoja aliyekuwa ameajiriwa kama mpish, alipokuwa anapika, kwa bahati mbaya mafuta yaliyokuwa yamechemka yalimwagika.

Dada huyu alipomwambia mwajiri wake, swali la kwanza kuulizwa lilikuwa, “Vipi, mafuta yamebaki?” Mwitikio huu uliwaudhi wafanyakazi wengine, kwa sababu mategemeo yao angeuliza kuhusu usalama wa yule aliyekuwa anapika kwanza.

Ndivyo ilivyo katika maeneo ya kazi. Wafanyakazi wana tabia ya kumwamini kiongozi anayejali utu wao na anayeelewa mazingira magumu wanayoyapitia katika kufanya kazi zao. Unapofanya hivi kama kiongozi, unaongeza uwezekano wa watu wako kukuamini.

Ishi unayotarajia wengine wayafanye

Huwezi kuaminika ikiwa huwi mfano wa kuishi yale unayotaka walio chini yako wayafanye. Ni kwa sababu mara nyingi wafanyakazi hufanya sawa sawa na yale wanayoyaona yakifanywa na viongozi wao.

Kwa mfano, wafanyakazi wanapojua kiongozi wao ni mwaminifu kwenye masuala ya fedha, na wao hali kadhalika, hujifunza kuwa waaminifu. Viongozi wanapokuwa wabunifu, wanaotukuza bidii, hekima na maarifa, huchochea utamaduni huo kwenye taasisi zao.

Udhaifu wa taasisi mara nyingi huwa ni udhaifu wa kiuongozi katika taasisi husika. Tabia za kiongozi wa taasisi unaweza kuziona kwenye kila kona ya taasisi, kwa sababu kwa kujua au kwa kutokujua anayoyafanya kiongozi, yanaambukizwa kwa watendaji wake.

Kama kiongozi unayetaka kuaminiwa, jifunze kutangulia mbele kuonyesha mfano wa yale unayotaka yafanyike. Maisha yako yaseme kwa sauti kuliko hotuba na maelekezo mengi yasiyoakisi kile unachokiamini.

Jifunze namna ya kuwasiliana

Si nyakati zote utaridhishwa na utendaji wa wafanyakazi wako. Wakati mwingine utakatishwa tamaa na baadhi yao wasiotekeleza majukumu yao kwa uzembe.

Suala la muhimu ni namna gani unaonyesha kutokuridhika? Unafoka na kulaumu mbele ya halaiki? Je, unaweza kuonyesha upungufu wa mtu bila kuumiza hisia zake?

Tumeona baadhi ya viongozi wakiwadhalilisha walio chini yao wakati mwingine mbele ya kadamnasi. Wanafanya hivi wakiamini watasaidia kuwatisha wengine wawe makini zaidi.

Lakini matokeo yake hawa wanaodhalilishwa wanakata tamaa na kazi na wale wanaoshuhudia haya yote yakitokea, wanakosa imani na kiongozi wao. Wanaanza kuwa na wasiwasi na usalama wao na taratibu wanaanza kukosa imani na kiongozi wao.

Jifunze kukosoa katika mazingira ya faragha. Unapomheshimu aliyekosea, si tu unamfanya apunguze kujitetea, lakini pia utakuwa umemfanya akuamini.

Sambamba na kuepuka kumdhalilisha aliye chini yako, jifunze kutoa pongezi hadharani. Hata kama mafanikio ni adimu. Ukiwa na mtazamo chanya hutakosa kuona vitu ambavyo watu wamejitahidi kuvifanya. Ukivitambua vitu hivyo, itakuwa rahisi kwako kuaminiwa.

Walinde unaowaongoza

Tangu zamani za kale, watu waliwategemea wafalme kuwa ngome ya usalama wao. Nyakati za vita, madhalani, wafalme walikuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano dhidi ya maadui. Walihatarisha maisha yao kwa maslahi ya watu wao. Kiongozi hakujigeuza mnyapara anayengoja ripoti ofisini.

Ikiwa unataka watu wako wakuamini, wahakikishie kuwa usalama wao ndiyo kazi kubwa uliyonayo kama kiongozi wao.

Wafanye waamini wewe ndiyo kimbilio katika nyakati za shida. Usiwe kiongozi anayeonekana kuweka mbele maslahi yako binafsi na kikundi chako. Usiwe kiongozi mwenye upendeleo.

Fikiria baba mwenye familia anayeona moto unawaka nyumbani na yeye anakimbilia nje kujiokoa wakati mke wake na watoto hawajui nini cha kufanya. Baba wa namna hii anapoteza sifa ya kiongozi mlinzi wa watu wake.

Huwezi kuaminika kama hujaweza kuwashawishi watu kuwa umeweka maslahi yao mbele. Zinapokuja nyakati za dhoruba kwenye kampuni au taasisi, onekana ukifanya jitihada za kunusuru mustakabali wa watu wako hata ikibidi kuhatarisha nafasi yako.

Tunawafahamu viongozi wengi mashuhuri walioaminika sana na jamii zao kwa sababu tu walithubutu kuchukua hatua zisizo za kawaida lakini zenye kuleta faida kwa watu wao. Hatua kama hizi hugusa mioyo ya watu na kuongeza ushawishi wa viongozi kwa watu wao.

Gidion Obeid mwandishi mshiriki wa makala haya ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na mwanafunzi wa Shahada za Uzamivu (PhD). Kwa ushauri wasiliana naye kwa namba 0625698050.

Utility

Jifunze kukosoa katika mazingira ya faragha. Unapomheshimu aliyekosea, si tu unamfanya apunguze kujitetea, lakini pia utakuwa umemfanya akuamini.