ALLY YAKUTI: Tulikosea kuzitosa tamthilia

ALLY YAKUTI aliyeandika filamu zaidi ya 100 zikiwamo maarufu kama Swahiba, Agano la urithi, Yellow Banana, Oprah, Hot Sunday, Family Tears, Fake Smile, Peace Of Mind, More Than Pain, Devil Kingdom na Foolish Age.

Muktasari:

Huyu ni mtunzi mahiri Afrika Mashariki, Ally Yakuti. Akifanya mahojiano na Starehe Yakuti anayataja mambo manne ambayo kwa njia moja ama nyingine yamerudisha nyuma soko la filamu nchini.

Ameandika filamu zaidi ya 100 zikiwamo maarufu kama Swahiba, Agano la urithi, Yellow Banana, Oprah, Hot Sunday, Family Tears, Fake Smile, Peace Of Mind, More Than Pain, Devil Kingdom na Foolish Age.

Huyu ni mtunzi mahiri Afrika Mashariki, Ally Yakuti. Akifanya mahojiano na Starehe Yakuti anayataja mambo manne ambayo kwa njia moja ama nyingine yamerudisha nyuma soko la filamu nchini.

Swali: Unasikia malalamiko ya kuporomoka kwa ubora wa filamu?

Yakuti: Nayasikia na ninaona kunachofanyika sicho tulichokitarajia wakati tunaamua katika utengenezaji wa filamu.

Swali: Fafanua?

Yakuti: Yap, nafahamu kuna watakaokubali na watakaokataa, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa mimi, marehemu Steven Kanumba na Vicent Kigosi au Ray kama anavyoitwa na mashabiki ndiyo tulianzisha msisimko wa filamu nchini. Wakati huo ilikuwa watu wanaigiza kwa mapenzi na siyo ajira na kazi kama sasa.

Tuliona hiyo ni fursa na tukajiuliza tufanye nini, tukaja na maazimio manne. Kwanza tulikubaliana kuwapo na malengo ya muda mfupi ikiwamo kubadili mfumo wa kuigiza tamthilia pekee ambao ulikuwa umeshika kasi wakati huo na kuja na filamu. Pia kuwe na mabadiliko katika tasnia ya filamu kila baada ya miaka 10 yaani tukae na kufanya tathmini ya yale tuliyoyafanya na nini kifanyike ili kusonga mbele.

Azimio jingine lilikuwa ni kila mmoja kusimama katika eneo lake, wakati ule Kanumba alikuwa anaweza kuongoza filamu, Kigosi halikadhalika na mimi pia, lakini tulikubaliana ili tufanye kwa ufanisi kila mmoja asimame katika nafasi yake. Hivyo mimi nikawa mtunzi, Kigosi na Kanumba waigizaji.

Azimio jingine lilikuwa kuhakikisha kunakuwa na sera itakayosimamia tasnia ya filamu yenye meno.

Swali: Unadhani hayo yote mliyokusudia hayajafanyika?

Yakuti: Hakuna sera ya filamu, Serikali imetilia mkazo kwenye mapato kiduchu ya filamu, kumbe sera hiyo ingeboreshwa tasnia hii ina fedha nyingi.

Yaliyokuwa malengo ya muda mfupi ndiyo yamekuwa ya muda mrefu, matokeo yake hakuna mabadiliko ndiyo maana vitu vinajirudia.

Lakini kwa sasa kila mtu ni mtayarishaji, mtunzi, mwongozaji, mwigizaji na wakati mwingine hivyo vitu vinafanya na mtu mmoja.

Sababu hizo na nyingine ndiyo zimechangia kulitingisha soko, lakini kuna namna ya kuinuka ambayo mimi binafsi naanza kuifanyia kazi, nimeandika andiko nitakaloliwasilisha kwa Waziri mwenye dhamana ya sanaa ili kuangalia tunafanyaje kurudisha hamasa ya filamu nchini.

Swali: Unadhani watunzi wa sasa wanakosa nini?

Yakuti: Sitaki kusema kwamba hawajui, bali wanakosa vitu vingi kutokana na kutojifunza zaidi. Ninajifunza kila kukicha ikiwamo kutoka kwa watunzi wa nje na wenye mafanikio, lakini nasoma sana vitabu.

Dakika chache kabla ya kuzungumza nawe nilikuwa nasoma kitabu cha siku nyingi, lakini ninajifunza hadi sasa cha Mtunzi James Hadley Chase kiitwacho Mission to Venice.

Swali: Unakumbuka vitabu vingapi kwa mtunzi huyo umewahi kuvisoma?

Yakuti: Vingi sana, lakini ninavyokumbuka haraka haraka ni pamoja na A coffin from Hong Kong, An Ace Up My Sleeve, My Laugh Comes Last.

Swali: Unazungumziaje kurudi kwa tamthilia?

Yakuti: Kwanza tulifanya makosa tulipoamua kuziacha na kujikita kwenye filamu pekee, lakini inawezekana hiki kilio cha kudorora kwa filamu kikawa kikubwa zaidi kama hatukuamka na kujipanga.

Tayari baadhi ya tamthilia zimeshakuwa gumzo, hivyo sasa ni changamoto kwa watayarishaji, waongozaji, watunzi na waigizaji wa filamu wanatakiwa wafanye kitu kikubwa tofauti na vinavyofanywa kila siku kwenye tamthilia, tofauti na hapo watu watahama kabisa na kuangalia tamthilia.