APR walivyoacha vumbi Dar

Muktasari:

  • Walifanya kweli. Timu zote zilionekana kujiandaa kwa mashindano, na ndiyo maana zilitwaa ubingwa kwa wanawake na wanaume.

Kama timu za Tanzania zilikuwa zinadharau bila kuyapa uzito mashindano ya wavu ya Nyerere, basi APR za Rwanda kwa maana wanawake na wanaume hawakuja kutania.

Walifanya kweli. Timu zote zilionekana kujiandaa kwa mashindano, na ndiyo maana zilitwaa ubingwa kwa wanawake na wanaume.

Kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Chama cha mpira wa Wavu Tanzania, TAVA, iliandaa mashindano ya kimataifa ya mchezo huo, yaliyofanyika Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Timu za APR zimetwaa ubingwa wa mashindano hayo na kuziacha timu za hapa nyumbani vichwa chini kwa kuambulia nafasi za pili na mshindi wa watatu.

Mashindano hayo ambayo yalianzishwa miaka 15 iliyopita kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa na mwaka huu, yalianza kutimua vumbi Oktoba 10 huku yakishirikisha jumla ya timu 13 kwa wanaume na 6 wanawake.

Wanaume walianza kucheza kwa hatua ya makundi. Kundi A lilikuwa na timu za APR (Rwanda), Nyuki (Zanzibar), Chui, Mjimwema na Makongo ya Dar es Salaam.

Kundi B lilikuwa na timu za Jeshi Stars , JKT (Dar es Salaam), Police (Zanzibar) na Kigoma wakati Kundi C lilikuwa na Magereza (Dar es Salaam), Shinyanga (Shinyanga) , Pentagon na Flowers (Arusha) na kwa upande wa wanawake wenyewe waliocheza kwa mfumo wa Ligi kulikuwa na APR (Rwanda), Makongo, Magereza, Jeshi Stars, Mjimwema na JKT za Dar es Salaam.

Michezo ya fainali ya mashindano hayo ambayo kilele chake kilikuwa juzi Oktoba 14 ilikuwa kati ya timu za majeshi ambazo ni APR na Jeshi Stars kwa wanaume na wanawake.

APR imeonyesha kuwa hawakuja kimatembezi kwa kushinda michezo yote miwili ya fainali ya wanaume na wanawake kwa seti 3-0,3-0.

Kocha APR, Nkuranga Alexis anasema kuwa japo mashindano yalikuwa na ushindani lakini wamepata walichotaka na haikuwa bahati kwao kushinda mataji hayo.

“Tulipoanza safari ya kuja Tanzania tuliweka malengo ya kufanya vizuri kwa kutwaa mataji ndicho kilichotokea, Tanzania ina timu nzuri ambazo zinaweza kushindana,” anasema kocha huyo.

Kocha wa Jeshi Stars wanaume, Lameck Mashindano anasema kuna haja ya timu za Tanzania kushiriki mashindano mengi ya kimataifa ili kujijenga zaidi kiushindani na kujiamini.

“Tumeshindwa kutetea taji lakini ndiyo michezo ilivyo ukikosa leo unaweza kupata kesho, mashindano ya kimataifa yatazijenga timu zetu, APR ilikuwa bora na ubora wao umechangiwa na kushiriki kwao mashindano mengi ya kimataifa.” anasema kocha huyo.

Nahodha wa APR, Mwizere Ezic anasema siri ya wao kufanya vizuri kwenye mashindano hayo ni uzoefu ambao wamekuwa nao wa kushiriki mashindano mengi ya kimataifa.

Naye nyota mwingine wa APR kwa wanawake, Kihozo Lyuzozo amezifisia Makongo, Magereza na Jeshi kwa kusema wana timu nzuri ambazo kama zikiendelea kukaa pamoja zinaweza kuja kufanya vizuri kwenye mashindano yajayo.