Abbah: Kichwa nyuma ya nyimbo za Darassa

ABBAH

Muktasari:

Wasanii anaowakubali:

1. Darassa
2. Steve RnB
3. Neyba
4. Diamond
5. Ali Kiba
6. Chidi Benzi
7. Ray C
8. Profesa Jay
9. Mangwair
10. Lady Jay Dee

Unasikiliza ‘Muziki’ wa Darassa, wimbo unakugusa kiasi kwamba unatamani kumfahamu zaidi huyu jamaa aliyeimba. Unasema hapana, unatafuta wimbo wake mwingine, mara unaupata ‘Kama Utanipenda’, wimbo ambao Darassa ameimba akimshirikisha Rich Mavoko.

Kabla hata Darassa hajaanza kuimba unasikia sauti inasema Abbah halafu wimbo unaanza.

Sasa je, umeshawahi kufahamu Abbah ni nani?Je, jina la mtu, wimbo au Studio?

Jibu la uhakika ni kwamba hilo ni jina la mtayarishaji aliyetengeneza mdundo wa wimbo huo,  pia ni miongoni mwa watayarishaji watatu walioshirikiana kupika wimbo uliovunja rekodi nchini ‘Muziki’ unaoendelea kushika chati ndani na nje ya nchi.

Jina lake kamili ni Sweetbart Charles, Msukuma aliyezaliwa na kukulia jijini Dar es Salaam. Ni mtoto wa pili kati ya watatu kwenye familia yao.

Ameshafanya kazi na wasanii wengi ndani na nje ya nchi kama vile Darassa, Baraka Da Prince, Nikki wa Pili, Rich Mavoko, YC kutoka nchini Nigeria na wengine.

Yafuatayo ni mahojiano aliyofanyiwa na Starehe, ameeleza mengi kuhusu maisha binafsi, kazi ya utayarishaji anayoifanya na tasnia ya muziki kwa ujumla.

Starehe: Jina la Abbah limetoka wapi?

Abbah: Abbah sio nickname unajua? Ni jina langu halisi pia. Hili Sweetbert nilipewa na wazazi wangu, na hili la Abbah alilichagua babu yangu. Ni jina lenye asili ya Kiyahudi na limaanisha ‘Baba’. Abbah lilipata nguvu kwa sababu nilikuwa sipendi kuitwa Sweetbert.

Starehe: Nini kilikusukuma kuingia kwenye muziki?

Abbah: Naweza kusema muziki unaishi kwenye damu yangu, na hicho ndicho kilichonisukuma kufanya ninachokifanya leo. Kwa mfano kuna siku tulipokuwa wadogo, baba alikuwa anatoka nyumbani, akatuuliza niwaletee nini nikirudi? Kaka yangu akachagua begi la shule, mimi nikaomba niletewe kinanda.

Nilichagua kinanda kwa sababu nilikuwa napenda muziki, nilitamani sana kuwa sehemu ya muziki mzuri. Baba aliporudi aliniletea kinanda na nikaanza kujifunza mwenyewe kuanzia hapo.

Starehe: Wazazi wengi huwa wagumu kuwaruhusu watoto wao kujiingiza katika muziki? Kwa upande wako, wazazi walikuwa na mtazamo gani juu ya ulichochagua?

Abbah: Nashukuru Mungu amenipa wazazi waelewa, hawakuwahi kuniwekea ‘ngumu’ ingawa kuna mambo tulishwahi kuvutana kuhusu muziki. Nilipokuwa sekondari mahudhurio yangu yalikuwa mabovu kwa sababu nilikuwa natumia muda mwingi studio nikiwatengenezea watu beats (ala za nyimbo). Hata hivyo, kilichokuwa kinawapa imani wazazi wangu ilikuwa ni matokeo yangu, yaani mimi sijawahi kuwa mtu wa tatu kwenda mbele. Ni wa pili au wa kwanza.

Starehe: Sasa ulikuwa unafaulu vipi wakati ulikuwa na mahudhurio mabovu shuleni.?

Abbah: Kutokwenda shule haina maana kwamba nilikuwa sisomi, isipokuwa nilikuwa na ‘staili’ yangu ya kupiga  kitabu. Nilikuwa nasoma kama mtoto anayebembelezwa kula, yaani unamuwekea chakula na vimidoli pembeni, sasa mimi nilikuwa napiga kitabu huku nasikiliza muziki kidogo.

Starehe:  Tukirudi kwenye muziki, utayarishaji rasmi ulianza lini na kwenye studio gani?

Abbah: Nilianza rasmi 2004, na studio yangu ya kwanza kufanya kazi ilikuwa inaitwa Natal Records, ipo Kigogo Mburahati. Nikiwa pale nilifanya kazi na  Rich Mavoko na Sharomilionea. Kipindi hicho bado nilikuwa mwanafunzi, kwa hiyo kuna muda wasanii walikuwa wanakuja studio, lakini wananisubiri mpaka mtayarishaji wao nitoke shule.

Starehe:Mtayarishaj gani aliyekuwa anakuvutia kiasi kwamba ulikuwa unatamani ufike alipo yeye?

Abbah: Kuna watayarishaji wengi tu nilikuwa nawakubali na naheshimu kazi zao,  lakini Lamar alikuwa ananiumiza kichwa kwa sababu kipindi kile alikuwa yupo kwenye chati halafu nikimuangalia naona tunalingana umri na nilikuwa naamini nina uwezo wa kufanya kazi bora zaidi ya zile alizokuwa anafanya.

Starehe: Ukizungumza na wasanii na watayarishaji wengi huwa kuna watu wanawataja kuwa waliwasaidia kufikia walipo. Kwa upande wako ni nani aliyegundua uwezo wako na kukushika mkono kukuleta juu?

Abbah: Mimi aliyenishika mkono ni Adam Juma. Alikuja studio nilipokuwa nafanya kazi ili wasanii wake watengenezewe ‘biti’ na warekodi. Nilipofanya nao kazi moja tu akanikubali, akataka tufanye kazi zaidi. Akaniambia kwamba anifungulie studio iwe chini yangu lakini yeye hatachukua hata senti itakayopatikana, isipokuwa tu nitakuwa nikiwafanyia kazi wasanii wake ambao walikuwa ni kundi linaloitwa ‘Waswazi’.

Starehe: Kwa hiyo ulitokaje kwa Adamu Juma mpaka kufika ulio leo?

Abbah: Ile ‘ishu’ ya Adam kutochukua fedha tunayopata studio ndiyo ilinisaidia. Mimi nilivyokuwa nafanya kazi nilikuwa nahifadhi fedha kidogo kwa ajili ya kununua vifaa vipya ili kukuza studio. Kwa hiyo Adam alivyoona nimepiga hatua akaniachia studio, na ndiyo mpaka sasa nina studio yangu hiyo inaitwa Vipaji Tz. Pia kwa sasa nafanya kazi na Studio nyingine ambayo ni kubwa zaidi ambayo wamiliki wake walinitaka nikashirikiane nao.  Studio inaitwa Insticks.

Starehe: Mlikutana vipi na Darassa hata mkaweza kutengeneza wimbo wenu wa kwanza wa ‘Kama Utanipenda’?.

Abbah: Naweza kusema ilianza kama ajali. Mimi nilikuwa nafahamiana na Rich Mavoko na sio Darassa. Siku hiyo wao walikuwa wanaenda kwa mtayarishaji mwingine kutengeneza wimbo huo, lakini gari ya Rich ilikuwa gereji, kwa hiyo wakapita studio kwangu kupoteza muda wakati wanasubiri gari iletwe. Wakati wako studio Darassa akanambia kwa masihara tu kwamba nifanye kitu aone, basi fasta nikatengeneza ‘biti’ palepale. Yaani nilitumia kama nusu saa tu kukamilisha kila kitu. Darassa akanikubali na tukarekodi siku ile ile, na tangu hapo nikaanza kufanya kazi naye.

Starehe: Unafanya kitu gani kingine kwa ajili ya kupata nguvu kiuchumi?

Abbah: Nina biashara zangu. Nina  ‘car wash’ (sehemu za kuoshea magari) mbili, moja ipo Mbagala na nyingine Mburahati. Nina bodaboda tatu, bajaj moja na saluni ya kiume.

Starehe: Umewekeza kiasi gani cha pesa kwenye studio yako?

Abbah: Unazungumzia mtaji sio? Nimewekeza kama Sh20 milioni hivi.

Starehe: Na ili ufanye kazi bora zaidi unadhani unahitaji uwekezaji wa kiasi gani cha pesa kwenye studio yako?

Abbah: Mh! Angalau niwe na studio yenye uwekezaji wa kama Sh100 milioni.

Starehe: Ni msanii gani unayetamani kufanya naye kazi.

Abbah: Binafsi natamani kufanya kazi na Oliver Mtukudzi. Napenda anavyoimba.

Starehe: Kama mtayarishaji wa muziki, unajua kupiga chombo gani?

Abbah: Naweza kupiga kinanda,  ngoma, tumba na sasa najifunza kupiga gitaa.

Starehe: Ni nani anayesema ‘Abbah’ kwenye nyimbo ambazo umetengeneza wewe?

Abbah: Yule anaitwa Baghdad.

Starehe: Nini malengo yako kama mtayarishaji?

Abbah: Kwanza kujijenga na kufanikiwa zaidi ya hapa kisha kuanzisha familia.

Starehe: Nini kifanyike kuwasaidia wasanii na vijana wa Kitanzania ambao wanaonekana waathirika wakubwa wa dawa za kulevya?

Abbah: Nadhani  Serikali inatakiwa kuziba mianya ambayo inatumika kuingiza dawa hizo nchini kwa sababu zisipokuwapo wanaouvuta watakosoa cha kuvuta na ambao bado hawajaanza kujitumbuliza huko hawatakuwa na pa kuanzia.