Abdul Hilal; Kutoka African Lyon hadi Tusker

Muktasari:

  • Kuonyesha msisitizo, Diego Maradona ambaye 1982 alijiunga na FC Barcelona kwa dau lililoweka rekodi ya dunia Dola5mil aliwahi kusema kuwa ili mafanikio yaje ni lazima kuwepo na juhudu hakuishia hapo aliendelea kwa kudai bahati haipaswi kutegemewa

Mafanikio ya nyota kadhaa wenye majina makubwa duniani kama Christiano Ronaldo wa Ureno na hata Lionel Messi wa Argentina yametokana na juhudi zao kwenye utafutaji wa maisha ya soka.

Kuonyesha msisitizo, Diego Maradona ambaye 1982 alijiunga na FC Barcelona kwa dau lililoweka rekodi ya dunia Dola5mil aliwahi kusema kuwa ili mafanikio yaje ni lazima kuwepo na juhudu hakuishia hapo aliendelea kwa kudai bahati haipaswi kutegemewa.

Juhudi za wachezaji wa Kitanzania wanavyojitahidi kutafuta maisha ya soka nje ya mipaka ya Tanzania zinaweza kuja kuzaa matunda kwa siku za usoni kuanzia kwao wenyewe na hata kwa Taifa.

Spoti Mikiki tunaendelea kukuletea nyota hao wa Kitanzania wanaoonyesha juhudi kwenye utafutaji wao, wiki iliyopita tulikuwa na Salum Shebe ambaye anaichezea Al-Mudhaibi ya Oman, wiki hii tunaye Abdul Hilal wa Tusker ya Kenya.

Abdul (22) aliitwa kwa mara ya kwanza Taifa Stars na kupata dakika kadhaa za kucheza kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na Malawi, Uwanja wa Uhuru.

Winga huyo wa Tusker amezungumzia mazingira yalivyokuwa kwa mara ya kwanza alivyopata taarifa za kuitwa timu ya Taifa Stars,maisha ya kambini yalivyokuwa kwake na hata alivyopata nafasi ya kucheza mchezo ule wa kirafiki.

“Nilikuwa nafahamu kama kocha alikuwa ananifuatilia na uzuri Ligi yetu ya Kenya inaonyeshwa na vituo vya Luninga ambavyo hata kwa Tanzania vinapatikana, nilichokiamini ni kuwa kutakuwa na wepesi wa kuniona.

“Kilichokuwa kinanipa moyo ni kuamini kwangu kuwa inawezekana mbona rafiki yangu Hamisi Abdallah wa Sony Sugar aliitwa kwenye mchezo wa nyuma ule, niliamua kujituma na mwishowe muda ulipofika nikapata taarifa za kuitwa timu ya Taifa.

“Nilishtuka na kuona hatimaye naenda kulitumikia Taifa langu, nilifurahi sana na mara moja nilianza taratibu za kuja Tanzania kwa ajili ya kujiunga na kambi ya timu ya Taifa, nilivyofika mara moja niliwasili kambini na kukutana na wachezaji wengine wakubwa,” anasema Abdul.

Mchezaji huyo aliendelea kwa kusema alifurahi na kubadilishana mawazo na wachezaji wengine ambao walikuwa wamepiga hatua zaidi yake hivyo alijua maisha yao yalivyo huko wanapocheza soka.

“Niliona ni nafasi nzuri kujua mengi kutoka kwa Mbwana Samatta, Saimon Msuva na hata wengine wa ndani, kitu ambacho ninacho huwa napenda kujifunza vitu vipya kutoka kwa ambaye nipo naye ngazi moja, niliyemzidi na aliyenizidi.

“Maisha ya mpira yanaweza kubadilika hivyo ni muhimu sana kujua mengi ambayo yapo ndani ya mpira na hata nje, maisha ya kambini niliyafurahia sana kwa sababu tulikuwa wote kama familia moja,” anasema.

Hata hivyo, alimalizia kwa kusema alivyoingia kucheza kwenye ile mechi ya kirafiki na Malawi aliingiwa na shauku ya kutaka kubadilisha hali nzima ya mchezo kwa kuisaidia Taifa Stars ambayo hata hivyo iliishia kusawazisha bao lenyewe kupitia Saimon Msuva.

Hapa anaelezea safari yake ya kucheza mpira wa kulipwa nje ya Tanzania ilivyokuwa mpaka akapata nafasi ya kujiunga na Tusker inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

“Kuna kituo hivi kinaitwa D.Y.O.C kipo maeneo ya Sigara TCC Chang’ombe hapo ndipo nilipoanza kucheza mpira wakati nikiwa mdogo na makocha walikuwa, Aluko Simango, Sizza Mpunda, Eddo na Brown Elnest.

“Hiyo ilikuwa 2002 na nilikaa kwenye hicho kituo kwa miaka nane baada ya hapo maisha yalisogea na nilikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walichanguliwa kwa ajili ya mashindano ya Copa Coca-Cola kwa Temeke ilikuwa 2010, tuliambulia nafasi ya tatu.

“Baada ya mashindano nilijiunga na African Lyon, kwa mara ya kwanza nilisaini mkataba wa miaka miwili, nilikuwa mdogo lakini nilikuwa napata nafasi ya kucheza kwa kipindi hiko ilikuwa tayari ipo Ligi Kuu,” anasema winga huyo tegemeo wa Tusker kwa sasa.

Maisha yake yaliendelea akiwa na Lyon lakini anadai kuwa ndoto yake ilikuwa ni kucheza soka la kimataifa kwa kucheza nje ya nchi hivyo ilibidi aanze mchakato wa kwenda kufanya majaribio kwenye mataifa ya karibu.

“Nilianza Congo kwenye timu ya FC Lupopo, nilifanya majaribio vizuri na rais wa timu ile alionyesha nia ya kunisajili kwenye timu yake na moja ya vitu ambavyo aliahidi kuvifanya kama akipita kwa sababu walikuwa kwenye uchaguzi mwingine ni pamoja na kunisajili. “Mambo yalienda fyongo na aliingia rais mwingine na kukosa nafasi ya kujiunga nao, ilibidi nijiongeze kwa kwenda Kenya, sikupata wakati mgumu kwenye majarinio ya Tusker kwa sababu ilipogusa mpira wangu wa kwanza waligundua kuwa mimi ni mchezaji hivyo waliamua kuniweka pembeni.

“Hawakutaka kabisa niendelee na majaribio waliamua kunipa kabisa mkataba na nikaanza kuichezea timu yao, nahitaji kuendelea kupiga hatua kwa kwenda kwenye Ligi nyingine kubwa zaidi kasha kama Mungu akipenda nicheze hata England,” anasema Abdul.