Aeesha Kamara: Miss Tanzania USA anayeamini urembo si kipaji

Miss Tanzania USA mwaka 2015, Aeesha Kamara

Muktasari:

Huyu ni Miss Tanzania USA mwaka 2015, msomi wa shahada ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Towson Maryland.

Dar es Salaam. Aeesha Kamara msichana mwenye umri wa miaka 20, ni mcheshi na mrembo. Mwonekano wake hasa urefu wa mwili ni kati ya vitu vitakavyokuvuta zaidi unapokutana naye kwa mara ya kwanza.

Huyu ni Miss Tanzania USA mwaka 2015, msomi wa shahada ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Towson Maryland.

Kitu kinachovutia zaidi kwa Aeesha ni namna anavyojitathimini yeye mwenyewe, lakini pia uelewa wake wa mambo ikilinganishwa na umri alionao.

Licha ya kushinda taji hilo, Aeesha aliendelea kupigania taji la Miss Africa USA na kufanikiwa kuingia hatua ya 10 bora. Katika safari yake nchini Tanzania, mrembo huyu ametembelea mbuga mbalimbali za wanyama na kuutangaza utalii wa ndani ya nchi.

Mbali na hilo pia Aeesha alifanya ziara kadhaa nchini ikiwa ni sehemu ya kuitumikia jamii, kabla ya kufanya mahojiano na Starehe mapema wiki hii kuelezea hali halisi ya tasnia ya urembo nchini na kile anachokiamini katika wadhifa alionao.

Swali: Safari yako kuelekea Miss Tanzania USA ilikuwaje?

Aeesha: Haikuwa rahisi kushinda taji hilo hapo awali, lakini nilikuwa na ndoto za kuiwakilisha nchi yangu katika fani ya urembo. Hivyo nilikuwa natafuta namna gani nitafanikisha ndoto yangu hiyo.

Swali: Hali ilikuwaje baada ya kufanikiwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho?

Aeesha: Nilipoingia niliona hakuna namna zaidi ya kupambana, nilijitahidi kusimamia mtizamo wangu kuhusu fani ya urembo na kile nilichokiamini, mengine kuhusu urembo na jinsi ya kuonekana nilijifunza baadaye, nilijikita zaidi katika vitu ninavyoviamini.

Swali: Unafikiri nini hasa mrembo anachotakiwa kufanya?

Aeesha: Kuna mambo mengi ambayo mrembo anapaswa kuyafanya, ikiwamo kujitambua, kujua atawajibika vipi kwenye jamii yake, nilihudhuria mafunzo ya Miss Morogoro wiki moja iliyopita kwa bahati mbaya ninawauliza nini wanafikiri wajibu wao hawajui chochote, hivyo wanaoshiriki shindano la urembo wajengewe uwezo kabla ya kujitosa watambue wanatakiwa kufanya nini kabla na baada.

Swali: Nini hasa kazi ya Miss Tanzania USA?

Aeesha: Kikubwa ni kuitangaza na kuiwakilisha nchi katika mataifa mengine, kubwa zaidi ni kutangaza utalii wa nchi na utamaduni ikiwamo vyakula vya asili yetu na maisha kwa ujumla.

Kwa mfano mimi nimekuwa nikitangaza mavazi ya Tanzania kwa kupita shule mbalimbali za upili nchini Marekani, kutokana na kazi hiyo nimegundua kuwa wapo watu wanaodhani kwamba Afrika ni masikini sana kiasi kwamba tunavaa magome ya miti, hivyo najaribu kuwaelimisha.

Swali: Watanzania wananufaika vipi na taji hilo?

Aeesha: Miss Tanzania USA ana nafasi kubwa ya kufanya kazi kadhaa za nchi yake, baada ya kushinda taji huwa na nafasi ya kutembelea Tanzania kwa ajili ya kufanya shughuli za kujitolea na kuona watu wa jamii yake pia.

Swali: Unadhani Tanzania ina nafasi ipi katika kulitumia taji la Miss Tanzania USA, Je? Wahusika wanatumia nafasi iliyopo?

Aeesha: Tuna nafasi kubwa ya kuitangaza nchi ya Tanzania kupitia taji hili, lakini kwa bahati mbaya Bodi ya Utalii na Wizara ya Habari Utamaduni, Wasanii na Michezo hawatutumii katika kuhakikisha tunafanya kazi za kuitangaza nchi kimataifa. Kwa mfano Bodi ya Utalii inafanya nami kikao kwa mara ya kwanza wiki hii nilikiwa mbioni kuondoka nchini kurejea Marekani baada ya wiki tatu za kukaa hapa.

Swali: Nini ambacho warembo wa Tanzania wanakikosea?

Aeesha: Kwa bahati mbaya asilimia kubwa ya warembo waliowahi kushika mataji Tanzania hawakujua nini maana ya urembo, wengi walidhani kwamba ni kitendo cha kupanda jukwaani kuonyesha mavazi, mikogo katika kutembea na uzuri wa umbo na sura. Lazima wajue nini wanaweza kufanya kwa ajili ya jamii yao na si fasheni pekee.

Swali: Unadhani ndoa ni muhimu zaidi kwa msichana wa sasa?

Aeesha: Wasichana wa sasa wanatakiwa kupoteza muda wao kushughulikia ndoto zao kwanza, masuala ya ndoa ni baadaye sana. Ifahamike kuwa ndoa si kila kitu kwa maana kwamba ukitimiza ndoto zako na kupata mafanikio maishani utapata mume bora zaidi kuliko ungeweka kipaumbele cha kutafuta mume mapema.

Swali: Nini kinachomkwamisha mwanamke wa Kiafrika?

Aeesha: Mwanamke wa Kiafrika anashindwa hasa anapokosa uthubutu na ujasiri wa kufanya jambo, wanawake licha ya kwamba hawapewi ushirikiano, lakini wana nguvu kubwa wakiamua kufanya jambo ikilinganishwa na wanaume.