Africab na dhamira ya kusambaza umeme nchini

Muktasari:

Shirika la Umeme (Tanesco) linalozalisha umeme na kusambaza ikishirikiana na Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) imekuwa mstari wa mbele kufanikisha lengo hilo la Serikali ya awamu ya tano kuipata Tanzania ya viwanda.

Wakati Serikali ikipambana kuongeza watumiaji wa umeme mchango wa wadau wa sekta binafsi ni muhimu kufanikisha hilo. Kuongeza hamasa hasa kupunguza gharama za nishati hiyo.

Shirika la Umeme (Tanesco) linalozalisha umeme na kusambaza ikishirikiana na Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) imekuwa mstari wa mbele kufanikisha lengo hilo la Serikali ya awamu ya tano kuipata Tanzania ya viwanda.

Hata hivyo juhudi hizo hazitoshi bila kuungwa mkono na sekta binafsi. Mashindano ya kampuni Bora 100 (Top 100) zinazoibukia yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam yakihusisha zaidi ya washiriki 200 kabla ya kupata waliokidhi vigezoi, yameonyesha maendeleo makubwa ya viwanda hasa kwa sekta binafsi.

Miongoni mwa kampuni zilizoingia kwenye orodha ya kampuni bora 100 ni Africab Group of Companies inayotengeneza vifaa vya umeme. Kampuni hiyo inajumuisha; Kilimanjaro, inayotengeneza vifaa vya umeme; Al Hatimy Enterprises Ltd, vifaa vya usambazaji wa umeme zikiwemo nyaya, mita na mitambo ya umeme wa viwandani, sasa inadhamiria kushirikiana na Tanesco na Rea kusambaza umeme nchini.

Meneja wa utawala wa kampuni hiyo, Kunjal Gina anasema hakuna tena haja kwa Watanzania kuagiza bidhaa za umeme kutoka nje kwa sababu uzalishaji wa kiwanda hicho unakidhi mahitaji.

Hasiti kueleza furaha yake ya kufanikiwa kuingia kwenye mashindano hayo na kuwa miongoni mwa kampuni zilizokidhi viwango. Anajivunia ufanisi katika kazi na ubora wa bidhaa wanazozalisha na kuwataka Watanzania kuziamini na kuzitumia bidhaa zao ambazo ni pamoja na nyaya, swichi, mitambo ya kubadilisha umeme wa gridi ya taifa na umeme wa jenereta na vifaa vya umeme wa viwandani.

Sababu za kutumia bidhaa za ndani zipo. Kuokoa muda, zipo zinazochukua mpaka miezi mitatu kuwasili nchini wakati kampni hii inatumia wiki moja pekee kukamilisha kila kitu. Lakini malighafi za ndani ndizo zinazotumika kuzalisha bidhaa nyingi, hii inaongeza thamani ya fedha huku ikikuza uchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.

Kadri inavyoendelea kujiimarisha, Africab inajipanga kuanza kutengeneza transfoma ili kuchochea usambazaji wa umeme nchini na kuwawezesha wajasiriamali kutumia nishati hiyo kwenye viwanda watakavyovianzisha kwa gharama nafuu.

Ikiwa inategemea shaba kutoka Zambia, mippango ipo tayari kuanza uzalishaji huo mwakani na transfoma hizo zitauzwa kwa Tanesco jambo litakalopunguza ghrama za kuvuta umeme, majumbani na hata viwandani.

Kushiriki mashindano ya Top 100 ni fursa ya kujitangaza na kubainisha uwezo wako wa kushindana sokoni. Kwa udhamini wa Mwananchi Communications Limited, Bank M, Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), KPMG na Azam TV mashindano hayo yanafanyika kwa awamu ya sita mwaka huu.

Washiriki wanapewa nafasi ya kujisajili DSE kwa kujengewa uwezo kabla ya kuzitumia fursa zilizomo sokoni humo kukuza mtaji na kuwashirikisha Watanzania wengi zaidi kumiliki kampuni za hapa nchini. Hilo linaenda sanjari na kupata nafasi ya matangazo kwa gharama nafuu kutoka Mwananchi na Azam.