Afrika ina la kujifunza kutoka Ethiopia

Muktasari:

  • Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere amewahi kutuonya kuilinda amani, umoja, mshikamano na utangamano wa taifa huku akisisitiza kuwa nchi ambazo hazina amani kwa sasa ziliwahi pia kuwa nchi zenye amani, mshikamano, umoja na uzalendo. Mwalimu alisisitiza, vitu hivyo vikipotezwa kwa sababu yoyote ile Taifa linalohusika linaweza kuingia matatizoni kirahisi.

Wiki hii Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn amejiuzulu wadhifa wake. Hailemariam Desalegn ambaye pia ni Mwenyekiti wa Muungano wa vyama vinavyotawala Ethiopia, ameeleza kuwa machafuko na migogoro ya kisiasa ambayo inaikumba nchi yake na kupelekea watu wengi kukimbia makazi yao au na kuuawa, ni moja ya sababu zilizomfanya achukue uamuzi wa kukaa pembeni.

Akizungumza kupitia Televisheni ya Taifa hilo mchana Alhamisi, kiongozi huyo ameeleza “...kujiuzulu kwangu ni sehemu ya jitihada za lazima za kuiruhusu nchi ifanye mabadiliko yanayohitajiwa na wananchi na ambayo yataleta amani ya kudumu na demokrasia ya kweli kwa wananchi wa Ethiopia” Kwa wale wasiofahamu, demokrasia ya Ethiopia kwa muda mrefu imekuwa na viashiria sawia na hali halisi ya kidemokrasia katika nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania. Mazingira ya Ethiopia yanafanana na nchi nyingi za bara letu, hivyo zinaweza kujifunza kwake.

Nasaha za wahenga

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere amewahi kutuonya kuilinda amani, umoja, mshikamano na utangamano wa taifa huku akisisitiza kuwa nchi ambazo hazina amani kwa sasa ziliwahi pia kuwa nchi zenye amani, mshikamano, umoja na uzalendo. Mwalimu alisisitiza, vitu hivyo vikipotezwa kwa sababu yoyote ile Taifa linalohusika linaweza kuingia matatizoni kirahisi.

Ili kuendeleza taifa lenye mshikamano, utulivu, umoja, udugu, uzalendo na sifa nyingine nyingi – Mwalimu Nyerere alitaka kuwa tujenge mifumo ambayo kila mwananchi atapata haki na azione zinatendeka, mwalimu alieleza, haki ndiyo msingi wa amani.

Mahali popote penye amani ya kudumu, haki zinapoanza kuvunjwa na kupuuzwa mahali hapo huweza kutumbukia kwenye machafuko, vita ya wenyewe kwa wenyewe na mauaji yasiyokwisha. Haki kuu za raia zinapovunjwa zinaweza kuonekana kwa vitendo, mathalani kwa sababu nchi zote duniani kazi yake ya kwanza ni kulinda maisha na mali za raia, inapotokea katika nchi yoyote ile maisha ya raia yanapotea kirahisi au yanapotezwa kienyeji tu, mahali hapo kuna uvunjifu wa haki na hali hiyo ikiendekezwa huleta balaa kubwa sana.

Tusisubiri kuzima moto

Kwa miaka mingi sana raia wa Ethipia wamevumilia kuminywa na kudhitibiwa na dola. Wamebaniwa uhuru wa habari, uhuru wa vyama vya siasa ukaota mbawa na wanasiasa wanaoikosoa serikali, wakapotea, wakakimbia nchi, na au wakashtakiwa na kufungwa kwa makosa ya kutungwa. Haya yote yanatokea mahali pengi hasa Afrika.

Manung’uniko ya wananchi wa Ethiopia ndiyo yamepelekea kuwepo kwa machafuko yasiyokwisha tangu mwaka 2014. Hivi karibuni katika juhudi za kurejesha amani, Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn aliwaachia huru wanasiasa wote kutoka magerezani, baada ya kukubali kuwa wanasiasa hao wakosoaji wa serikali wanateseka bure.

Haile Mariam ameona haitoshi na nafsi imemsuta sana, ameona ajitoe madarakani ili kupata kiongozi atakayejenga Ethiopia yenye utangamano na umoja, ukizingatia kuwa yeye binafsi

Inaendelea uk 24

Inatoka uk 23

amekuwa sehemu ya utawala ambao uliendeleza ukandamizaji tangu na kabla ya kuwa waziri mkuu.

Wakati nafsi inamsuta Hailemariam na anaamua kusimamia haki kwa kuondoka madarakani, ukweli mchungu ni kwamba raia wa Ethiopia wameshaumia sana, wamekufa mno na wamekandamizwa kweli kweli na hakuna namna ya kuwalipa - kama tujuavyo kazi ya ujenzi huchukua miaka lakini ubomoaji ni sekunde moja.

Wapambe wa watawala

Kama ilivyo kwa nchi nyingi leo, wakati wote wa ukandamizaji wa raia wa Ethiopia, wako wapambe wa serikali na dola ambao huyaishi na kuyafurahia maisha hayo ya ukandamizaji wa raia - watu wakiuawa wapambe hao wa serikali wanasema sawa, watu wakitekwa wao wanasema wamejiteka, wanasiasa wakifungwa wao husema “dola haichezewi, tena iwafunge miaka mingi zaidi, ikiwezekana milele.”

Wakati wa uongozi wa Hailemariam, wapambe hao wa dola walimsifia kweli kweli, walisifia kila anachofanya na wakapongeza kila anachokosea, hawakuweka mipaka wala akiba. Leo baada ya Mariam kujiuzulu na kukiri kuwa utawala wake umefanya makosa mengi, wapambe walewale waliokuwa wanamsifia tayari wameshaonekana kwenye TV ya taifa ya Ethiopia wakisifia uamuzi huo wa Haile.

Si Ethiopia tu, hata nchi nyingine na hata hapa kwetu, yako masuala muhimu unakuta uongozi wa nchi umeyafanya kwa haki na kizalendo. Na yako masuala mengine uongozi yanafanyika bila kutenda haki, kufuata sheria wala katiba. Athari ya wapambe wa utawala kwenye hali kama hiyo ni wao kusifia mazuri ya serikali na kusifia mabaya ya serikali, wanasifia yote.

Mfano, kiongozi wa nchi akisimama hadharani na kusema utawala wake umeminya mno demokrasia, umeua uhuru wa habari na vyombo vya habari na mengine utasikia viongozi wa chini, baadhi ya vyombo vya habari na wapambe wengine wakijimwaga mitaani kumpongeza kwa kueleza ukweli huo.

Lakini wapambe hao hao siku kiongozi huyo anapotoka madarakani watajitenga naye mita 1000. Ndivyo ilivyokuwa Ethiopia.

Tusipite njia ya Ethiopia

Kwa hiyo, yale yanayotokea katika nchi zetu za Afrika leo, yametokea Ethiopia kwa miongo kadhaa na wapambe wa watawala wakasema hayana uzito - leo, kiongozi wa utekelezaji wa madhambi hayo amejiuzulu na kuieleza dunia kuwa utawala wa chama chake na yeye mwenyewe wemetenda vibaya dhidi ya mustakabali na demokrasia ya Ethiopia - ni jambo kubwa sana.

Tunapaswa kujifunza Ethiopia, kwamba vitendo vya kikatili na kinyama vinavyotokea katika nchi zetu, si jambo la kujivunia na halikubaliki. Leo Ethiopia inavurugika na ina majeshi imara, kumbe majeshi si kila kitu, wananchi wana ukomo wa uvumilivu, na ukomo huo ukifika ni vigumu kuwadhibiti tena na kwa sababu ya maslahi ya mama nchi. Ni mwendawazimu tu ndiye anaweza kupuuza jukumu la kuipigania amani na utangamano wa nchi yake na bara zima la Afrika.

Ethiopia ilianza kuvurugika polepole, wanasiasa wakapigwa vita, shughuli za kisiasa za vyama mbadala zikapigwa marufuku, Bunge la Ethiopia likatulizwa, mahakama, majaji na mahakimu wakadhibitiwa, chanzo cha habari kwa wana wa Ethiopia kikabakizwa kuwa televisheni ya taifa hilo tu huku vyombo vingine vikifungwa, vikivurugwa, vikinyimwa leseni na kunyanyaswa na ikahakikishwa kwamba televisheni ya taifa na redio ya taifa ndivyo vinabaki ulingoni.

Fikra mbadala si dhambi

Uvunjifu wa haki za wana Ethiopia haukuishia hapo, waandishi wa habari wakateswa, wanasiasa wakafungwa, wafanyabiashara wasiounga mkono serikali wakafilisiwa, wakosoaji wa serikali wakateswa sana, wanaharakati wakatishiwa na wengine wakapotea kwenye mazingira ya kutatanisha. Mambo mengi sana yametokea Ethiopia na wananchi wakayavumilia.

Tangu mwaka 2014 wananchi wa Ethiopia wakaanza kudai haki zao zote za msingi, haki za kiuchumi, haki za kisiasa, haki za kijamii, haki zikawa haki juu ya haki. Serikali ya Ethiopia chini ya Hailemariam ikatoa matamko mengi kuonyesha kuwa wanaodai haki hizo ni makundi ya watu waliotumwa na wazungu, na mataifa ya magharibi na maadui wa serikali.

Miaka minne baadaye, Hailemariam yule yule anasimama hadharani na kukiri kuwa utawala wa nchi yake na yeye akiwa kiongozi mkuu, haujawatendea haki wananchi wa Ethiopia. Hailemariam anaomba msamaha na anajiuzulu, lakini anajiuzulu wakati mgawanyiko umekuwa mkubwa sana, Ethiopia ile iliyosimama imara na ikakataa kutawaliwa na wakoloni si hii ya leo – na waliosababisha Ethiopia ya sasa ikagawanyika na kukosa uzalendo, utu, ubinadamu na mengine ni watawala wa taifa hilo akiwemo waziri mkuu aliyeondoka.

Jinsi ya kukwepa

Nchi nyingi za Afrika zinapita kwenye wakati mgumu sana kukiwapo dalili za kuhodhi haki za msingi za raia, hali ambayo tunapaswa kuikwepa kwa nguvu kubwa.

Katika baadhi ya nchi, leo tumefikia mahali kauli za mgawanyiko, kuvunja umoja wetu, kufurahia watu wanaopotea na kutekwa, kufurahia mauaji ya raia wenzetu na vitendo vya kikatili – vimekuwa vitu vya kawaida na vilivyoanza kuzoeleka.

Leo chaguzi nyingi Afrika zinaendeshwa kwa gharama kubwa hadi ya maisha ya watu wasio na hatia kupotea. Mwalimu Nyerere kila mara alitukumbusha kuwa amani isipotunzwa hupotea na tena akihitimisha kuwa ili amani isipotee lazima kuwepo na haki.

Wanasiasa wengi husubiri hadi mambo yaharibike kabisa ndipo huchukua hatua kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Ethiopia. Amesubiri mambo yamekuwa magumu mno ndipo akachukua hatua za kurejesha utangamano, kuwaachia wafungwa wa kisiasa na hatua zingine – hata hivyo raia wa Ethiopia walishaingiwa na usugu na walishazoea vurugu. Hatua za Waziri Mkuu hazikufua dafu hadi ameamua kujiuzulu.

Funzo muhimu

Kwa kuyatazama yaliyofanyika Ethiopia, Waafrika kwa ujumla tunapata funzo kubwa kwamba tunao wajibu wa kufanyia kazi haraka mambo yanayotokea katika nchi zetu. Si jambo sahihi akiacha watu wakaendelea kufunzwa usugu, wakaanza kuona mapambano ya dola na wananchi ni jambo la kawaida.

Viongozi wa nchi hizi wasikubali kamwe misingi iliyokuwapo iendelee kuvunjwa, wasiruhusu haki za msingi za wananchi zivunjwe, wawazuie wasaidizi wao na wachukue hatua kali pale ambapo haki hizo zimevunjwa.

Pia, kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Ethiopia, viongozi wasione aibu, inapotokea wao au wasaidizi wao wamevunja misingi ya utangamano wa watu wao wajitokeze hadharani na kuomba radhi na kueleza taifa hatua wanazochukua ili makosa ambayo serikali zao zinayafanya yasiendelee.

Viongozi hao pia wajipange na kuwawajibisha wasaidizi wao ambao wanavunja Katiba na sheria, wasikubali kusubiri hadi mambo yaharibike ndipo wasimame na kuchukua hatua za juu sana wakati wanao wasaa wa kuchukua hatua za kawaida mapema.

Julius Mtatiro ni mchambuzi na mfuatiliaji wa utendaji wa serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF). Simu; +255787536759. Barua Pepe; [email protected]