Afrika kuwa nchi moja bado kizungumkuti

Muktasari:

Vuguvugu hilo lilianza kama harakati ya kiutamaduni na baadaye likaendelezwa kuwa zla kisiasa kwa lengo la kuunganisha nchi huru za Afrika baada kuondoka kwa ukoloni ili kutengeneza nchi moja yenye Serikali na dola moja.

Kwa miongo sita kumekuwa na vuguvugu la kuamsha Uafrika na kuwaunganisha Waafrika kote duniani na kuwaweka pamoja ili waweze kutambua utu na thamani yao na kushirikiana kujiletea maendeleo.

Vuguvugu hilo lilianza kama harakati ya kiutamaduni na baadaye likaendelezwa kuwa zla kisiasa kwa lengo la kuunganisha nchi huru za Afrika baada kuondoka kwa ukoloni ili kutengeneza nchi moja yenye Serikali na dola moja.

Wazo hilo lilianza kipindi cha mapambano ya kupigania haki za Waafrika kote duniani ambayo yaliungwa mkono na wanaharakati maarufu wa Marekani kama vile Marcus Garvey na William Du Bois. Kwa Afrika viongozi wanaoweza kutambuliwa haraka kwa dhana hii ni Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana na Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania.

Mkutano wa kwanza wa wanaharakati hawa wa uafrika, ulifanyikia Accra Ghana mara tu baada ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1957. Mwaka 1958 Nkrumah alitoa wazo la kuunda umoja wa nchi huru za Afrika. Baada ya mazungumzo marefu, wazo hilo lilikubaliwa na viongozi wa nchi huru za Afrika akiwemo Nyerere. Hivyo umoja wa Afrika OAU ambao sasa unaitwa AU uliundwa mwaka 1963 nchini Ethiopia.

Pamoja na umoja huo, Nyerere na Nkrumah walifikiri zaidi ni kwa vipi bara la Afrika lingeweza kuungana na kuwa nchi moja, wazo ambalo hadi leo ingawa halijazaa matunda lakini bado lingalipo.

Msimamo wa Nkrumah

Nkrumah na wenzake kutoka nchi za Mali, Nigeria na Guinea walitaka kuharakishwa kwa Afrika kama nchi moja, tofauti na hapo waliona ni kupoteza muda. Waliona kuwa kuundwa taifa moja la Afrika kusingezifanya nchi husika zikose uhuru, bali kungesaidia kuleta muungano baina ya Waafrika wenyewe.

Kwa mtazamo wake, Nkrumah aliona tatizo la kuwa na tamaduni tofauti halikustahili kukwamisha harakati za kuunda taifa la Afrika na kuwa kuendelea kuchelewa kungetoa nafasi kwa wakoloni kurudi kuitawala Afrika kwa urahisi.

Katika moja ya matamshi yake anasema umoja ulikuwa njia pekee ya kuwazuia wakoloni kutawala tena.

Anabainisha kuwa matatizo mengine baina ya nchi na nchi yangeendelea kutatuliwa huku muungano ukiwa umeshaundwa.

“Muungano wa Afrika utajenga nchi huru na imara yenye kusimamia maamuzi yake kuhusu uzalishaji katika kilimo,” anasema katika moja ya matamshi yake.

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Msimamo wa Nyerere

Nyerere alitaka hatua za kuunda nchi moja ya Afrika zisiharakishwe. Nyerere alitoa mawazo ambayo aliona yasingeruhusu muungano wa haraka alioutaka Nkrumah.

Alisema kila nchi inayo haki ya kutengeneza uchumi na siasa yake ili kuifanya nchi hiyo kutambulika kwa lugha na tamaduni zake.

“Ni vigumu kuwaunganisha watu wenye tamaduni tofauti, lazima kwanza tofauti hizo za kitamaduni ziondolewe, jambo hilo linahitaji muda,” anasema Nyerere.

Pia Mwalimu alibainisha kuwa matatizo yanayozikumba nchi za Afrika, kama umaskini, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ujinga, magonjwa ni kikwazo kikubwa katika uundaji wa umoja huo.

Kutokana na hali hiyo anabainisha kuwa suala la kuziunganisha nchi kadhaa wa kadhaa kama hatua mojawapo ya kuelekea kuunda Afrika moja, ndipo zikaundwa jumuiya kama SADC, Ecowas, Comesa na EAC.

Tumekwama wapi

Wazo hilo ambalo lilitolewa wa wazee hao bado lipo katika fikra za baadhi ya Waafrika, hasa wasomi wanaoamini kwamba jambo hilo linawezekana. Hata hivyo wapo wengine wanaoona ugumu katika utekelezaji wake.

Wakati wa kongamano la tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika kwa siku tatu katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wasomi mbalimbali walijadili kwa kina juu ya mawazo hayo ya waasisi wa nchi za Afrika.

Kongamano hilo la kitaaluma lililoanzishwa na UDSM kwa lengo la kufufua mawazo ya Mwalimu Nyerere yanayozikwa na wachache wasiokuwa na mapenzi mema na Tanzania na Afrika, mada kuu mwaka huu ilikuwa ni “Nafasi ya wanasiasa ya wanasiasa katika kuanguka na kuinuka kwa maendeleo ya Afrika.

Wanasiasa walaumiwa

Katika kongamano hilo wanasiasa wa Afrika walitupiwa lawama kwa kushindwa kufanya mageuzi ya kimtazamo ambayo yangeweza kuendeleza nchi zao na bara zima kwa ujumla, badala yake wanakumbatia wahisani ambao wanafanya mambo mengi kwa masilahi ya mataifa yao, na hivyo kukwamisha muungano.

Mwanakigoda wa mwaka huu ambaye ni mwanasiasa na mwanadiplomasia kutoka Senegal, Profesa Abdoulaye Bathily anasema endapo Afrika itaungana na kuwa na dola moja itakuwa ni ukomo wa changamoto zinazolikabili bara hilo sasa ambazo ni magonjwa, ukosefu wa ajira na ukimbizi ambao unasababishwa na migogoro katika baadhi mataifa.

“Afrika imekosa viongozi wenye mtazamo chanya kwa ajili maendeleo ya Afrika ya leo na ya baadaye. Hayo yote ni kwa sababu viongozi waasisi hawaenziwi kwa matendo yao na maandiko waliyoyaacha. Wao waliungwa mkono na kufanikiwa katika ukombozi kwa kuwa walikuwa na mtazamo wa kuona ni kitu gani umma unataka,” anasema Profesa Bathily.

Anasema Afrika haiwezi kuendelea bila kuungana na kuwa na nguvu moja, kuangalia ni mambo gani yana manufaa ya muda mrefu kwa Waafrika na si kila kiongozi kuangalia maslahi ya nchi yake pekee.

Profesa Bathily anaongeza kuwa Waafrika wanapaswa kuwa ndiyo washiriki wakuu wa kujenga uchumi wao kwa pamoja.

“Afrika ya sasa ni utengano, kila nchi ina wabia wake lakini ukweli ni kwamba wabia kutoka nje hawawezi kuwaletea maendeleo Waafrika. Ndiyo maana Afrika inaendelea kuwa bara la kuzalisha malighafi na bidhaa zinazalishwa kwingine. Hata mashamba yanayolimwa na wawekezaji wa mataifa mengine ni kwa ajili ya manufaa yao na si chakula kwa Waafrika,” anasema Profesa Bathily.

Anabainisha kuwa nchi za bara la Asia zimeendelea kutokana na viwanda, biashara na kilimo ambavyo vimetoa ajira kwa raia wake lakini Afrika hata katika ujenzi wa miundombinu yoyote watalaam wote wanatoka katika mataifa ya watu badala ya kuendeleza watu wa ndani ili kuwa na taifa la watu wenye ujuzi.

“Afrika ina watu zaidi ya bilioni moja lakini ili iweze kuendelea ni lazima mataifa yake yawe pamoja. Tangu kupata uhuru ni zaidi ya miongo minne sasa lakini bado kuna mkuwamo katika maendeleo yake kwa sababu hakuna muungano halisi kwa mataifa yanayounda bara hilo,” anasema Bathily.

Hoja ya muungano wa Afrika kwa maendeleo yake inaungwa mkono na Mwanasheria nguli, Profesa Patrick Lumumba kutoka Kenya. Katika kongamano hilo, alizungumzia mada ndogo iliyohusu siasa safi barani Afrika.

Anasema Waafrika wanapaswa kujiamini na kushikamana na kutakatisha siasa zao huku viongozi wakitanguliza masilahi ya wananchi wao mbele kwa ajili ya maendeleo ya Waafrika wote.

“Nchi zetu haziwezi kuendelea kwa bajeti zinazotegemea wahisani, ni lazima kuvipenda vitu vyetu na kuvithamini, mkwamo wa maendeleo uliopo unatokana siasa chafu miongoni mwa viongozi wa mataifa yetu, ni vizuri kuiga mfano wa Namibia na Angola,” anasema Lumumba.

Anasema kuna namna ambavyo Afrika inaweza kutoka katika mkwamo wa kimaendeleo ni kwa kuungana kwa kuwa na fedha moja, hati moja ya kusafiria na kushirikiana katika miundombinu.

“Kuna umuhimu wa kuwa na treni ya umeme inayotoka Cairo, Misri hadi Pretoria, Afrika ya Kusini. Kila ukanda ufanye ubobezi katika kuzalisha kitu fulani, kwa mfano nchi ya Congo ikafanywa kuwa chanzo cha nishati, sehemu nyingine chakula na maeneo mengine kufanya jambo jingine kulingana na mazingara na uwezo wake ili mradi kuiinua Afrika kwa pamoja,” alisema Profesa Lumumba.

Changamoto za utekelezaji

Mhadhiri mstaafu wa masuala ya maendeleo ya jamii wa UDSM, Profesa Ophelia Mascarenhas anasema jambo la muungano wa Afrika lina ugumu wake kwa sababu kila nchi ina mtazamo wake na matatizo yake.

“Kwa mfano leo kuna ambao wanataka kuendelea kupokea msaada kutoka kwa wahisani wao, kuna ambao wanafanya mapinduzi ya viwanda. Kila kiongozi wa nchi atakuwa na vipaumbele vyake ambavyo kwa upande wake ataona vina masilahi kwa taifa lake,” alisema Mascarenhas.

Mhadhiri wa Elimu wa UDSM, Profesa Herme Mosha anasema katika muungano huo changamoto ni hofu ya demokrasia ya kweli katika kupatikana kwa viongozi wa kuongoza dola nyingine ambazo kimsingi zina aina ya maisha na tamaduni tofauti.

“Historia iwe kigezo muhimu kwa sababu ndiyo silaha kuu ya jadi. Sisi Tanzania katika demokrasia tayari tumefanikiwa, viongozi wetu wakimaliza muda wao wanang’atuka bila kubembelezwa wala kutumia nguvu lakini je wote watakuwa wa namna hiyo? Au kutakuwa na uchu wa madaraka,” anahoji Profesa Mosha kisha akacheka kidogo.

Anasema mahali pekee ambapo Afrika inaweza kuungana ni katika nyanja ya uchumi kwa kuwa ni mfumo wa pamoja wa uzalishaji mali kwa ajili ya mataifa yote kwa kuangalia kila ukanda unaweza kuzalisha kitu gani.

Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wakiwamo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaonyesha dhamira nzuri katika kuimarisha umoja wao.

“Jumuiya zikijiimarisha na kuonyesha mafanikio mazuri, muungano wa bara zima utakuwa ni rahisi kufanikiwa,” anasema.

Mhadhiri mwingine ni Richard Mbunda anasema wanaoamini kuwa Afrika inaweza kuungana sasa wanapaka mafuta tu, lakini uhalisia wake ni mgumu kwa sababu nchi zote hazipo katika msitari mmoja.

“Nchi hazipo sawa kiuchumi, thamani ya fedha, uwezo wa kuzalisha. Ni vigumu sana nchi kuungana zikiwa hazilingani kiuchumi ila ni rahisi endapo maendeleo yake katika nyanja tofauti yanalingana,” anasema Mbunda.