Ahadi ya Sh50 milioni kila kijiji isisubiri 2020

Muktasari:

  • Machi 2016 Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC), lilitangaza kuwa Serikali imetenga Sh800 bilioni kwenye bajeti yake ili kuanza utekelezaji huo. NEEC ilirudia tena tangazo lake hilo Septemba 2016 kuwa fedha hizo zitaanza kutolewa mapema mwaka 2017.

        Mwaka 2015 CCM iliahidi kuwa iwapo ingeshinda Uchaguzi Mkuu, ingetekeleza programu maalumu ya kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji ili fedha hizo zitumike kuchochea maendeleo ya watu wa vijiji hivyo. Jambo hili halikuwa wazo baya, lakini tulitahadharisha kuwa CCM isingeweza kulitekeleza kwa ufanisi.

Machi 2016 Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC), lilitangaza kuwa Serikali imetenga Sh800 bilioni kwenye bajeti yake ili kuanza utekelezaji huo. NEEC ilirudia tena tangazo lake hilo Septemba 2016 kuwa fedha hizo zitaanza kutolewa mapema mwaka 2017.

Mpaka sasa hakuna kijiji ambacho kimepata hata senti tano ya mkoloni.

Katika kugonga msumari wa mwisho kwenye jeneza, majuzi Rais Magufuli akiwa Mwanza ametamka rasmi kuwa yeye hana hizo fedha na kwamba anasafisha kwanza ili aweze kuzipata. Kwa hiyo CCM imetoa ahadi isiyotekelezeka. Ni dhahiri kuwa wamewahadaa wananchi. Lakini duru nyingine zinaonyesha kuwa CCM inataka kulifanya jambo hili mwaka 2019/2020, si kwa lengo la kuchochea maendeleo ya watu, bali kwa lengo la kutapanya fedha ili kupata kura.

Rai yetu ni kuwa, kama lengo ni kuinua maisha ya watu, programu hii ilipaswa kutekelezwa sasa, ili itumike kuchochea uchumi wa wananchi wa vijijini nchini.

Sisi ACT Wazalendo tunakubaliana na wazo hili, japo uzoefu wa miaka iliyopita unatuonyesha kuwa CCM haina uwezo, maarifa na njia nzuri za kutekeleza mipango na programu za namna hii. Pia ni lengo letu kupitia makala hii kutoa njia nzuri mbadala ya utekelezaji wa programu hii.

ACT Wazalendo ingefanya nini?

Sisi tuliwaahidi kwenye ilani yetu mwaka 2015 kuwa iwapo tungechaguliwa na kushika madaraka tungetekeleza sera ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wote nchi nzima. Hifadhi ya jamii ni mfumo wa kuweka akiba kwa muda mrefu na kupata mafao kama vile fao la matibabu, fao la uzazi, fao la mikopo ya ujasiriamali, fao la bei na fao la ukame.

Mafao ya muda mrefu ni pensheni ambapo mwanachama wa hifadhi ya jamii hulipwa baada ya kupoteza nguvu za kufanya kazi. Tungetekeleza wazo hili zuri la Sh50 milioni kila kijiji kwa kutumia ahadi yetu hii ya hifadhi ya jamii kwa wote.

Tanzania ina jumla ya vijiji 15,000. Jumla ya Sh750 bilioni zingehitajika kutekeleza ahadi ya Sh50 milioni kila kijiji. Kwenye ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2015 tulipendekeza mfumo wa akiba wa Serikali kuchangia sehemu na mwananchi kuchangia sehemu iliyosalia.

Katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo sisi ACT Wazalendo tunaiongoza, tunatekeleza wazo hili kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF), ambapo mwananchi anachangia asimilia 50 kwenye hifadhi ya jamii na Manispaa inachangia asilimia 50 iliyobakia.

Iwapo Serikali ingetumia mfumo huu ingeweza kuwa na Skimu ya Hifadhi ya Jamii yenye jumla ya Sh1.5 trilioni kwa yenyewe kumchangia kila mwananchi anayeingia Sh10,000 na mwananchi kuchangia Sh10,000 iliyobaki kila mwezi.

Kwa Sh750 bilioni za Serikali, watu 6,250,000 wangeweza kulipiwa na kuingizwa kwenye hifadhi ya jamii kwa wao kuchangia nusu tu ya michango ya kila mwezi.

Idadi hii ni wastani wa watu 400 kila kijiji na Mitaa kwa maeneo ya mijini. Watu hawa wanakuwa kwenye chama cha msingi cha ushirika kwa madhumuni haya. Na wote, pamoja na wategemezi wao watano kila mmoja angekuwa anapata bima ya afya na mikopo ya ujasiriamali ilhali akiba yao ipo palepale.

Katika vijiji na mitaa mingi nchini tatizo la huduma za afya lingekwisha kabisa, wananchi mngeweza kutibiwa kwa bima na wajibu wa Serikali ungebaki kwenye kushirikiana nanyi kujenga vituo vya afya na zahanati tu. Kwa wafugaji, skimu hii ingekuwa ni mkombozi mkubwa, vikundi vya ushirika vya wafugaji vingeweza kupata mikopo pamoja na kujengewa uwezo wa kuanzisha ranchi ndogondogo za ufugaji na kuondoa kabisa tatizo la kuhamahama na mifugo, huku ukame ukitokea wanalipwa fidia kutokana na fao la ukame kwa mifugo.

Skimu hii ingewakomboa wakulima pia, ambao ni asilimia 75 ya Watanzania wote vijijini, karibu robo tatu ya wananchi wote. Kwanza ingetoa urahisi kwa mikopo kupitia vyama vya ushirika, ingechangia uanzishwaji wa viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na uwepo wa fao la bei ungewahakikishia uhakika wa soko na fidia iwapo bei ya mazao yao ingeporomoka.

Jambo muhimu zaidi, kwa mfumo huu, Serikali itaweza kuwa na Watanzania milioni 36 wenye bima ya afya, ndoto ya bima ya afya kwa wote ingetimia.

Programu hii ingefanyika kwa miaka mitano tu mfululizo basi wananchi wangeweza kufikia uwezo wa kujilipia wenyewe akiba kwa asilimia 100 na kuukuza Mfuko wa Skimu hii mpaka kufikia jumla ya Sh7.5 trilioni.

Jambo hilo pia lingeweza kukuza uchumi kutokana na uwekezaji wake kwenye maeneo yanayohusu wananchi wa chini na kwenye miradi yenye masilahi kwa Taifa, ukijengwa utaratibu utakaofanya maamuzi ya kiuwekezaji kuamuliwa na bodi huru ya wadhamini yenye uwakilishi wa wananchi waliomo kwenye Skimu hiyo.

Hivyo kuifanya skimu hii shirikishi na iliyo wazi kwenye uendeshaji wake, ili kuziba mianya ya maamuzi mabaya pamoja na rushwa na ufisadi.

Faida ya yote haya isingekuwa kwa wananchi, Serikali nayo ingefaidika, kwani fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii huwekezwa kwenye miradi ya Serikali kupitia hati fungani na hata uwekezaji wa moja kwa moja kwenye miradi mikubwa kama ya kilimo, mifugo na viwanda vya kuongeza thamani za mazao ya kilimo na mifugo.

Skimu hii pia ingesaidia kuongeza uwezo wa uwekaji wa akiba katika nchi yetu, kwa sasa uwiano wa uwekaji wa akiba nchini ni asilimia 16 tu ya Pato la Taifa, wakati kwa muundo wa uchumi wetu tulipaswa kufikia hata asilimia 30 tu, nchi kama China wamefikia asilimia 50. Kuwa na akiba ndani ya nchi kutaongeza uwezo wa uwekezaji utokanao na fedha za ndani nchini.

Lakini pia Serikali ingetumia fedha kidogo kwenye bajeti ya afya kwani zaidi ya nusu ya wananchi wangekuwa na Bima ya Afya kupitia skimu hii, na uchumi wa nchi yetu usingesinyaa kama ilivyo sasa kwa sababu mikopo ya ujasiriamali na kwa vikundi vya ushirika wa wakulima na wafugaji kupitia mifuko hii ya hifadhi ya jamii ingeongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi na kuchochea uzalishaji wa mali.

Ni jambo la kushangaza kuwa Serikali inasema haina fedha za kutekeleza ahadi yake yenyewe. Utekelezaji wa Sh50 milioni kila Kijiji kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii ingeifanya Serikali iwe na fedha zaidi za kutekeleza miradi yake.

Hivi majuzi Serikali imekwenda kukopa Sh1 trilioni kwenye benki moja kwa riba kubwa ili kutekeleza miradi yake, ingekuwa imetekeleza hifadhi ya jamii isingehitaji kwenda huko nje kukopa kwani ingekopa fedha hizo ndani na malipo ya riba yangebaki ndani na kurudi kwa wananchi kupitia bima ya Afya, uwekezaji kwenye kilimo, mifugo na viwanda, pamoja na mikopo kwa Wajasiriamali.

Tungeweza kuupanua uchumi wa nchi yetu kupitia hifadhi ya jamii, ni bahati mbaya kuwa CCM hawayafanyi haya.

Kila wakati nasema Serikali ya CCM inasumbuliwa na ukosefu wa maarifa, si dhamira. Sina mashaka na dhamira yake bali maarifa ya kuchambua matatizo ya nchi yetu na kuyatatua.

Katika nchi yeyote ya Kidemokrasia, nakisi ya maarifa hutatuliwa kwa mijadala. Serikali ya Awamu ya Tano haitaki mijadala, haitaki mawazo mapya ambayo yangewasaidia kuongeza maarifa.

Ndio maana uchumi unaporomoka, na wananchi wanalia na hali mbaya lakini mawazo mazuri ya kutatua hali hiyo kama haya, hayasikiki, kwa sababu haki na uhuru wa kujieleza vinaminywa.

ACT Wazalendo pamoja na mazingira haya ya kuminywa kwa nafasi ya kutoa mawazo mbadala, bado tunaendelea kutimiza wajibu wetu kwa Taifa kwa kuhakikisha tunakosoa na kushauri juu ya sera mbadala. Suala la kusikia na kutekeleza litabaki kwa Serikali.

Zitto Kabwe, ambaye ameandika haya, ni Kiongozi wa ACT Wazalendo.