Ahsanteni kwa kutuamini

Muktasari:

  • Hatua hiyo ni baada ya Rais Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange kushikiliwa na vyombo vya dola kwa sababu mbalimbali.

Julai 2, 2017, Kamati ya Utendaji ya klabu ya Simba, iliwateua wajumbe wa kamati hiyo, Abdallah Salim na Iddy Kajuna kuwa wasimamizi wa majukumu ya Simba.

Hatua hiyo ni baada ya Rais Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange kushikiliwa na vyombo vya dola kwa sababu mbalimbali.

Salim amechukua nafasi hiyo ingawa Kassim Dewji ndiye alikuwa ameteuliwa, lakini alikataa kuwa hayuko tayari kutokana na majukumu yanayomkabili.

Salim maarufu ‘Try Again’ anakaimu nafasi hiyo licha ya kudaiwa kuwa Dewji amekataa kwa kuwa ana majukumu mengi ya kifamilia lakini taarifa zinaeleza, hakutaka kuanzisha migogoro kwa kuwa kuna makundi yanampinga.

“Kwanza ninawashukuru watu wote zaidi wanachama kwa kutuamini, lakini niseme kwa kifupi tu kwamba tumefanikiwa katika maeneo mbalimbali tangu tuichukue Simba na sasa mabingwa.

“Wakati tunaichukua Simba ilikuwa kipindi cha usajili, tulihangaika kuitengeneza Simba, tumefanya usajili wa wachezaji tunaoamini watatusaidia na kuipa Simba mafanikio na sasa mabingwa.

“Yako mengi ya mafanikio kwa kweli, tumefanya tamasha la Simba Day. Ilikuwa tukio la aina yake kutambulisha wachezaji wetu, tumefanya mkutano wa wananchama wa kujitambulisha lakini pia kuwaomba baraka zao kuelekea kwenye Ligi Kuu, wakatupa na mafanikio haya ni kwa ajili yao.

“Tumecheza Ngao ya Jamii, tumewafunga Yanga na tunaona ligi inamalizika na Simba kutwaa ubingwa na mechi mkononi, lakini raha zaidi kumfunga mtani.

“Yako mengi, mengi...tumefanya mabadiliko benchi la ufundi, tumebadilisha walimu sasa Simba inanolewa na Pierre Lechantre na Masudi Djuma, ilishtua mashabiki na wapenzi wa soka kumwondoa Joseph Omog na Jackson Mayanja, lakini yote ni katika kuweka sawa. Kuna mengi ya mafanikio Msimbazi.”