Aibu kwa wanafunzi waliosoma Shule ya Msingi Katerero

Mmoja wa wahitimu wa Shule ya Msingi Katerero, Ali Mufuruki akizungumza na wadau wa shule. Mufuruki ndiye aliyefanikisha shule hiyo kupata msaada wa umeme.

Muktasari:

  • Tangu wakati huo imekuwa chimbuko la wasomi wanaolitumikia Taifa kwa njia tofauti.

Shule ya Msingi Katerero iliyopo Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, ilianzishwa mwaka 1958 kabla ya uhuru wa Tanganyika.

Tangu wakati huo imekuwa chimbuko la wasomi wanaolitumikia Taifa kwa njia tofauti.

Kama zilivyo baadhi ya shule nyingine nyingi hapa nchini zilizotelekezwa, huku zikiwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya wanafunzi wao wa zamani,shule ya msingi Katerero nayo inaingia kwenye mkondo huo.

Miundombinu mibovu ya majengo na ukosefu wa huduma muhimu kwa ajili ya wanafunzi na walimu, haibebi taswira halisi kwa shule ya kihistoria ambayo ni chimbuko la wasomi na watu ambao msingi wao wa kupiga hatua ulianzia hapa.

Kitabu kimoja darasani

Suala la upungufu wa vitabu vya kiada na ziada unaonekana katika shule nyingi za msingi hapa nchini ingawa suala hilo limezidi kiwango katika shule hii ambayo wanafunzi wa darasa la saba wanatumia kitabu kimoja cha Kiingereza.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye pia anafundisha somo hilo, Denisia Mutungi anasema kitabu kinatumika kwa zamu na wanafikiria jinsi ya kupata njia mbadala ili kuwasaidia wanafunzi kuondokana na adha hiyo.

Kama sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo anasema kuwa tayari ameazima vitabu viwili kutoka shule nyingine ambavyo wanafunzi watalazimika kuvitumia kwa makundi wakati taratibu nyingine zikiendelea.

‘’Nilikuta kitabu kimoja cha lugha ya Kiingereza ambacho nakitumia hili ni darasa la mitihani na kumbuka haturuhusiwi kununua vitabu. Nimeazima vitabu vingine viwili na wanavitumia wakiwa kwenye makundi’’anasema Mutungi.

Pia mwalimu huyo anasema kuwa upungufu wa vitabu unawajengea mwelekeo mbaya wanafunzi watakaoendelea na masomo ya sekondari, kwa kuwa hawakujengewa msingi mzuri tangu shule za msingi.

Aidha, anasema kuwa suala la upungufu wa vitabu unajionyesha takribani katika madarasa yote ya shule hiyo, jambo linalowapa changamoto kubwa walimu na wanafunzi katika utekelezaji wa majukumu yao ndani na nje ya darasa.

Anaamini kuwa shule hiyo wamepita wanafunzi wengi baadhi yao wakiwa ni wahadhiri katika vyuo vikuu hapa nchini, na kuwa wakiunganisha nguvu wanaweza kusaidia ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zilizopo.

Hakuna maktaba

Pamoja na ukongwe wake wa zaidi ya miaka 50 tangu kuwepo kwake, shule hii haina maktaba kwa ajili ya wanafunzi 550 na walimu 12 ambao wangeweza kuitumia kitaaluma.

Kundi hili kubwa la wanafunzi halina matarajio ya kufanya maadalizi yao ya masomo na kujisomea vitabu vya kiada na ziada, wakiwa kwenye jengo la maktaba kwa kuwa halipo.

Yajitahidi kitaaluma

Pamoja na walimu kufanya kazi katika mazingira yaliyozungukwa na changamoto lukuki, bado wanafunzi 38 waliomaliza darasa la saba mwaka 2017 wamechaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza kati ya 39 waliohitimu.

Ndoto za wanafunzi

Baadhi ya wanafunzi tayari wana ndoto kubwa katika safari yao ya masomo.Wengine wanatamani kufika hadi vyuo vikuu kama wengine waliopitia kaika shule hii ambayo sasa ina miundombinu dhaifu.

Mwanafunzi wa darasa la saba Devotha Leonard anasema matarajio yake ni kuwa daktari wa binadamu, ingawa hadi anapoelekea kuhitimu hakuwahi kuona kompyuta na kuitumia zaidi ya kufundishwa kwa nadharia darasani.

Kwa upande wake Elpidius Venant anayesoma darasa la sita analipenda somo la Tehama na anatamani kuwa rubani. Hata hivyo, anasikitika kuwa mambo yote wanafundishwa kinadharia kwa kuwa shuleni hakuna vifaa vya masomo husika.

Walilia umeme

Ni wazi kuwa ndoto za wanafunzi na matarajio ya walimu hayawezi kufikiwa kwa kuwa shule haina miundombinu ya umeme na baadhi ya vifaa vya kielektroniki vinahitaji nishati hiyo ili vitumike kufundishia.

Mwalimu Naziru Suleiman anasema kuwa uhakika wa umeme kwenye vyumba vya madarasa utarahisisha ufundishaji wa somo la Tehama na kuchochea ubunifu wa wanafunzi katika masomo yao.

Mwenyeki wa kijiji cha Kanazi ilipo shule ya Katerero Haruna Swalehe, anashauri wadau hasa wanafunzi waliosomea hapo wajitokeze kuboresha mazingira ya shule hiyo ili liwe eneo bora kielimu la kujivunia.

Mobisol wajitokeza

Kampuni ya umeme wa jua ya Mobisol imejitokeza kutatua sehemu ya changamoto nyingi zinazoikabili shule hii kwa kuanza na uwekaji wa mitambo sita ya umeme wa jua kwenye nyumba za walimu.

Mmoja wa wahitimu katika shule hiyo Ali Mufuruki aliyefanikisha upatikanaji wa nishati hiyo, anasema uboreshaji wa mazingira ya walimu ulianza na ukarabati wa nyumba.

Anasema matarajio yake kama mwanafunzi wa zamani wa shule hiyo ni kuifanya kuwa ya mfano kwa kuwa na mazingira bora kwa walimu na wanafunzi na mipango ya baadaye ni kuwezesha upatikanaji wa intaneti kwa ajili ya somo la Tehama.

Meneja wa Mobisol kanda ya ziwa, Nkora Nkoranigwa anasema msaada huo ni sehemu ya mradi wa kuboresha mazingira ya walimu wa shule hiyo na unalenga kufikisha umeme wa jua katika ofisi za walimu na vyumba vya madarasa.