Aibu yao, wameumbuka!

Muktasari:

Unaweza kusema wameumbuka. Walidhani Cameroon itakuwa ileile, kumbe miaka hailingani. Ajabu yake, wengine wanasema hawajutii kukosa fainali hizo.

Unaweza kusema wameumbuka. Walidhani Cameroon itakuwa ileile, kumbe miaka hailingani. Ajabu yake, wengine wanasema hawajutii kukosa fainali hizo.

 

Kocha Broos

Kocha wa Cameroon, Hugo Broos alifanya kazi ya ziada kuwaita kikosini, lakini wakamdengulia na kusema kuwa hawawezi kujiunga na timu ya Cameroon kwa kuwa wana majukumu ya klabu.

Wachezaji nane wa Cameroon waligoma kujiunga na timu ambao ni Joel Matip, Allan Nyom, Eric Maxim Choupo-Moting, Guy N’Dy Assembe, Maxime Poundje, Andre Onana, Andre-Frank Zambo Anguissa na Ibrahim Amadou.

Pamoja na kudhoofisha timu, lakini Indomitable Lions ilifanya kazi bila wao na walicheza fainali kwa ari kubwa.

 

El Hadj Diouf

Mshambuliaji wa zamani wa Senegal, El Hadji Diouf aliiambia BBC World Service kwamba, mchezaji kama Matip na Nyom watajutia kiburi chao kugomea kuitumikia Cameroon, wanatakiwa wasikilize wimbo wa Bob Marley, Buffalo Soldier.

“Siwaelewi kabisa watu wanaokataa kujiunga na timu zao za Taifa,” alisema Diouf.

Alisema, “Na kama Bob Marley anavyosema: ‘If you don’t know where you come from, you don’t know where to go. (Kama hujui unakotoka, hujui wapi pa kwenda.

“Ni wazi hata kama hawako wazi, lakini watajilaumu hata kimoyomoyo. Baada ya kumaliza soka utafanya nini au utakwenda wapi? Utabakia Ulaya? Kufanya nini? Ni ngumu kwa Mwafrika, unaweza kuwa kocha mzuri Afrika, lakini huwezi kupewa ufundishe hata PSG (Paris Saint-Germain), Barcelona, Liverpool, au Manchester United. Ndiyo maana ninasema kwa wao wote: Usidharau taifa lako, kwa kuwa maisha yako ya baadaye ni Afrika.”

Katika fainali za 2002, Diouf alikuwa roho ya Senegal ‘Simba wa Teranga’ aliongoza timu hadi fainali, lakini walifungwa na Cameroon katika penalti. Diouf alikuwa mmoja wa wachezaji watatu waliokosa penalti.

 

Roger Milla

Diouf aliungwa mkono na mkongwe Roger Milla, aliyeiongoza Cameroon katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990 wakati ilipoifunga Argentina na kutolewa na England dakika za nyongeza.

Akizungumza baada ya kutwaa ubingwa, Milla alisema: “Wakati Matip na wenzake wanagomea timu, waliopo wakafanya vizuri, lazima wajutie.”

 

Nyom onyesha jeuri

Nyom (28) beki wa timu hiyo, anasema hajutii uamuzi wake wa kugomea timu ya taifa kwa kuwa mpango wake ni kujitengenezea mazingira West Midlands na katika kikosi cha Tony Pulis.

Cameroon ilikataa kumpa kibali Nyom na kumwondoa katika kikosi cha wachezaji 23 na hadi Fifa kuingilia kati na hiyo ilisababisha Pulis kumwacha katika mechi na Derby County na Tottenham Hotspur.

“Sijutii,” Nyom aliiambia BBC World Service. “Wametwaa ubingwa au hawakutwaa hakunibadilishii chochote katika maisha yangu. Hata kama ningekuwepo. Sijutii chochote katika hili.”

Hata hivyo, Nyom anasema yuko tayari kujiunga na Cameroon kama watakuwa wanamhitaji, licha ya kusema kuwa aliamua kubaki Albion. “Nimesikia kocha anasemasema, anasema nini,” alisema Nyom na kuongeza: “Muulizeni na anafahamu kwa nini mimi sikuwapo na nini kimetokea.”

 

Mapokeza ya kufa mtu

Wachezaji wa Cameroon walipata mapokezi ya kitaifa baada ya kuwasili na kombe lao, yaliyoongozwa na Rais Paul Biya.

Wachezaji wa Indomitable Lions walilikabidhi Kombe la Rais Biya katika hafla iliyofanyika Unity Palace na baadaye wachezaji walizunguka kwa gari la wazi kwenye mitaa ya Yaounde wakiwa na kombe lao.

Wachezaji wa Cameroon walipewa medali ya Rais, ambaye alisema ushindi wa timu yao lazima ushangiliwe na kila mmoja.

Baada ya sherehe hizo, mke wa Rais, Chantal Biya alipiga picha na wachezaji wa timu hiyo huku akitumia simu ya kipa, Fabrice Ondoa kupiga naye ‘selfie’.

Ushindi wa Cameroon umemaliza kiu ya miaka 15 ya kushiriki fainali hizo bila mafanikio. Cameroon ndiye mwenyeji wa fainali za 2019.

 

 

Salamu za Rais

Rais Biya aliwapongeza vijana wake kwa ushindi ambao alisema ulishangiliwa kutoka Kaskazini hadi Kusini na Mashariki hadi Magharibi katika mikoa yote 10 ya Cameroon na ni kama wameshinda vita dhidi ya Boko Haram.

Rais alisema timu ya wanawake, Lionesses wameweka rekodi lakini Lions wamefanya kweli. Wanaume wamefanya kazi kubwa kwa kuilaza moja ya timu kali Afrika.

“Umoja wenu ndiyo mafanikio, mmefanya kazi kubwa ya kudumisha umoja wa taifa na ndiyo ulioleta mafanikio. Kila Mcameroon anajivunia mafanikio yenu,” alisema.

Rais alitoa salamu za pekee kwa kocha Hugo Broos kwa kutengeneza ari ya ushindi kwa wachezaji. Aliwapongeza Wagabon kwa kuandaa fainali zilizofana.

Aliwatakiwa kila la kheri wachezaji waendelee kuliletea sifa taifa.

Baada ya hotuba yake iliyochukua dakika nane, aliwavika kila mmoja Medali ya Rais wa Jamhuri ya Cameroon kwa wachezaji na benchi la ufundi.