Ajabu ya Watanzania, hatuna jema!

Muktasari:

  • Maamuzi yalifanyika mwaka 1973 na hayakuwa maono au mawazo, yalikuwa maamuzi, makabrasha yote ya serikali yakaanza kusoma, Dodoma kuwa mji mkuu, bado nayakumbuka makonzi niliyopigwa nilipojibu kuwa makao makuu ni Dar es Salaam nikiwa darasa la pili. Hata google ukiiuliza inakwambia makao makuu ni Dodoma.”

Katika jukwaa moja la wasomi mtandaoni, mjadala mzito unaibuka kuhusu uamuzi wa Rais John Magufuli kutaka Serikali yake kuhamia Dodoma.

Kuna makundi matatu. Makundi mawili ungeyategemea, lakini  kundi moja lilinistajabisha. Hili ni kundi la ajabu; kundi la Watanzania.

Makundi mawili ya mwanzo ni yale ya wanaoafiki uamuzi wa mwendo kasi (wengine huuita uamuzi wa ‘kukurupuka’ au wa ‘mizuka’) wa Serikali kuhamia Dodoma haraka haraka.

Kundi hili lilitoa hoja kuwa maneno yametosha, sasa patendwe. Walisema, marais wote wanne waliopita walizungumzia Serikali kuhamia Dodoma, lakini hakukuwa na utashi wa dhati wa kisiasa wa kutekeleza uamuzi huo na hivyo wakaishia kusema tu.

Wakaendelea kutushawishi kwa kusema sasa yafaa Magufuli ambaye amekuja kutekeleza aungwe mkono maana ni takriban zaidi ya miaka 40 sasa tangu uamuzi wa kuhamia Dodoma upite.

  Hizo ndizo hoja za waliounga mkono uamuzi huo wa kuhamia Dodoma chap chap

Kundi la pili ni la wale waliosema licha ya nia nzuri ya kuhamia Dodoma, kasi hii ya uhamaji haina tija. Hawa waliitaka Serikali isikurupuke kwani mchakato huu  usipofanyika kwa uangalifu unaweza kuleta athari mbaya na wakazitaja baadhi ya athari hizo.

Ilidaiwa kuwa kwanza Serikali inafaa ijiridhishe kuwa kuna ofisi za kutosha na nyumba za makazi kwa ajili ya watumishi wanaohamia huko.

Hawa waliopinga uhamaji wa mwendo kasi pia walionya kuwa kazi hii ikifanyika kwa haraka na papara huenda  nyaraka muhimu za Serikali zikapotea. 

Pia wapo waliohoji bajeti ya kuhamia Dodoma ilitengwa au ni mwendo uleule wa Rais kuamua juu kwa juu kupeleka fedha kwenye mradi bila idhini ya Bunge.

 Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Mhandisi Paskazi Muragili, akinukuliwa katika mtandao wa IPP Media, Sh1.3 trilioni sawa na asilimia 4.4 ya bajeti yote ya mwaka huu ambayo ni Sh29.5 trilioni, zinahitajika kutekeleza mpango wa kuhamia Dodoma. 

Katika kundi hili, yaani wale walioamini kuwa kuhama fasta fasta si jambo zuri pia walisema Ilani ya chama tawala inaagiza Serikali iwe imehama katika kipindi cha miaka mitano, sasa iweje watake

kuhama ndani ya miezi kadhaa tu na pia walionyesha wasiwasi wa utayari wa balozi za nchi za nje kukubali kuhamia Dodoma kwa mtindo huu wa kuburuzana.  Hilo ni kundi la pili na hoja zao.

Kundi la Watanzania

Kundi la tatu likaja na msimamo wa kushtusha. Wao wakahoji kuhamia Dodoma kabisa. Wao wakasema sababu zilizotumika kuamua kuhamia Dodoma hazina uzito tena katika zama hizi kwa hiyo baadhi wakataka ipigwe kura mpya ya maoni ya kuamua jambo hilo ama Serikali ifute tu uamuzi huo na badala yake ibaki Dar es Salaam!

Ikumbukwe kuwa  Oktoba 1973, iliamuliwa kuhamisha makao makuu ya nchi  kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, sababu kubwa ikitajwa kuwa kijiografia mji huo upo kati ya nchi.

Iliamuliwa pia kuwa  Dar es Salaam ingebakia kuwa bandari kuu na kitovu cha biashara.

Ulikuwa ni uamuzi mgumu kiutekelezaji, kama ilivyokuja kuthibitika miongo minne baada ya kuhangaika kutekeleza uamuzi huo. 

Changamoto ya kuhamia Dodoma inatokana na mambo mawili. Kwanza ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa, maana Dar es Salaam ni jiji la maraha; na hivyo kusababisha changamoto ya pili ya kutotengwa kwa rasilimali za kutosha kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kuifanya Dodoma iwe makao makuu.

Katika wale waliokuwa wakihoji uamuzi wa kuhamia Dodoma, mmoja aliandika katika jukwaa lile la wasomi, akihoji ni vipi matumizi ya Sh1.3 trilioni  kwa ajili ya kuhamia Dodoma hayaingii katika kundi la matumizi yasiyo na tija yaliyopigwa marufuku na  Serikali ya Awamu ya Tano?

Mjumbe huyo anayehoji makao makuu kuwa Dodoma akadai ajulishwe ni vipi uwekezaji wa  Sh. trilioni 1.3 za kwenye uhamishaji wa kushtukiza wa makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma una tija gani kwa taifa?!

Kuhusu tija inayotokana na kuhamia Dodoma mimi sijui. Lakini ninachojua ni kuwa uamuzi ulipita wa kuhamia Dodoma mwaka 1973 na serikali imekuwa ikiutekeleza hata  kama ni kwa kusuasua.

Katika miaka yote ya utekelezaji haku watu hawakuhoji kuhamia Dodoma. Zaidi watu walilalamikia unyondenyonde wa Serikali wa  kutekeleza uamuzi huo.

Sasa wakati serikali imeamua kutekeleza uamuzi huo watu wanajitokeza kuhoji usahihi wa kuhamishia makao makuu Dodoma! Huu ni unafiki wa hali ya juu!

Kweli tunaweza kuhoji haraka ya  kuhamia Dodoma kwa kuhofia athari mbalimbali za kukurupuka huko,  lakini kuhoji kuhamia Dodoma na kutaka makao makuu yabaki Dar es Salaam ni miujiza ya hawa ninaowaita kwa jina jipya la ‘Wataanza nia’.

Mimi ni mmoja kati ya watu wasioafiki  methodolojia ya rais wetu ya kufanya mambo, nikiamini wakati fulani anatumia ubabe, lakini ninaposikia mambo kama haya namuelewa kwa nini rais huamua kuziba masikio na kulazimisha mambo kwa amri.

Ni kwa sababu ya watu wa aina hii, vigeugeu, leo wanasema hivi kesho vile.

Baada ya miaka yote hii ya ujenzi wa makao makuu mjini Dodoma, leo watu fulani wadai tugeuze uamuzi?  Walikuwa wapi miaka yote hii hadi wahoji uamuzi huu leo?

Hii haikubaliki, na haijalishi kama wana hoja za kuitetea Dar es Salaam kuendelea kuwa makao makuu au hawana. Uwekezaji uliofanyika Dodoma kwa miaka yote hii zaidi ya 40 ni mkubwa mno kugeuza uamuzi huo kirahisi.

Mpaka sasa haiwezekani kurudi nyuma. Mabilioni ya fedha yashatumika kujenga majengo, baadhi ya taasisi zilishahamia huko, na hata mamlaka nzima ikaundwa kusimamia ueendelezaji wa Dodoma. Tumeyavulia nguo maji, lazima tuyaoge.

Naungana na msemaji mmoja aliyehoji  kundi la wanaohoji usahihi wa makao makuu kuwa Dodoma. Mmoja aliandika: “Maamuzi yalifanyika mwaka 1973 na hayakuwa maono au mawazo, yalikuwa maamuzi, makabrasha yote ya serikali yakaanza kusoma, Dodoma kuwa mji mkuu, bado nayakumbuka makonzi niliyopigwa nilipojibu kuwa makao makuu ni Dar es Salaam nikiwa darasa la pili. Hata Google ukiiuliza inakwambia makao makuu ni Dodoma.”

Wale wanaozuka sasa kupinga Dodoma kuwa makao labda wana sababu binafsi, kama mmoja alivyodai kuwa kuna watu waliokopa kujenga hoteli Dar es Salaam na hivyo watakosa wateja na hivyo kushindwa kurejesha mikopo. Kama hili lipo, inahuzunisha lakini ukweli ni kwamba kila uamuzi utakaochukuliwa una gharama zake.

Licha ya kuwakosoa wanaopinga makao makuu kuwa Dodoma, hoja ya lile kundi linalopinga kuhama haraka  ni muhimu izingatiwe.

Ni sawa Rais alivyosema Serikali yote itakuwa imehamia Dodoma katika miaka mitano ya mwanzo ya utawala wake, lakini mawaziri wanapowaambia wafanyakazi wa wizara zao kuhamia Dodoma ndani ya wiki moja au mwezi. 

Hawa wafanyakazi wana familia, wakiwamo watoto wanaosoma. Unawahamishaje ghafla?

Kukurupuka kama walivyofanya baadhi ya mawaziri siyo sawa, lakini hatimaye Serikali lazima ihamie Dodoma.

0789201383