Akili nyingi mwisho wake uchizi

Muktasari:

Katika wakati huo kuku, samaki, nyama, mayai na maziwa zikawa bidhaa za anasa. Mtu aliyebeba mfuko wa matunda alipewa pole kwa maana kama hakuwa mgonjwa basi aliuguza. Wakati huo soda, bia na sigara hazikupata hata nafasi ya kuitwa bidhaa.

Kisa cha Tanzania kuitwa “Bongo” kipo wazi kabisa. Miaka ya 1980 baada ya vita vya Kagera, hali ya uchumi ilikuwa mbaya sana kiasi cha wananchi kutakiwa kufunga mikanda kwa muda wa miezi kumi na minane. Unga, mchele. Sukari, mafuta na sabuni zilikuwa bidhaa adimu zilizopatikana kwa mgawo katika maduka ya kaya.

Katika wakati huo kuku, samaki, nyama, mayai na maziwa zikawa bidhaa za anasa. Mtu aliyebeba mfuko wa matunda alipewa pole kwa maana kama hakuwa mgonjwa basi aliuguza. Wakati huo soda, bia na sigara hazikupata hata nafasi ya kuitwa bidhaa.

Mishahara mitupu haikuweza kukidhi mahitaji mama ya familia ya watoto wawili. Kizazi kilishagubikwa na maadui njaa na umasikini, na kulikuwa na hatari ya kuwa na kizazi kijacho kitakachotawaliwa na maadui hao ukijumlisha yule mbaya zaidi, adui ujinga.

Kwa nia njema kabisa Watanzania walilazimika kutafuta njia mbadala za kujikwamua. Waajiriwa waliongeza kulima bustani za mboga na kujenga magenge ya kuuza nyanya na vitunguu ili kuongeza tija. Siku za mapumziko ya mwisho wa juma na sikukuu zilitumika zaidi kwa shughuli za kujiajiri.

Hata hivyo vyuma havikulegea.

Vijana waliokuwa wakisubiri ajira za serikali na wale waliojiajiri wakabuni ya kwao. Waliwatazama wenzao waliotoka masomoni ng’ambo walivyo na ahueni ya maisha. walipowahoji wao walisema walikuwa wakijiongeza kwa vibarua vya kusafisha vyoo na kufagia barabara.

Majanki wakajiuliza kwa nini na wao wasiende huko kuhemea ili kuwasaidia wazazi majukumu ya familia. Lakini kwenda kulihitaji hati ya kusafiria iliyotolewa kwa mkono wa Umoja wa Vijana wa CCM, na nauli ambayo ilipaswa kutajwa kwa tahadhari kubwa kwani anayeombwa anaweza kupandwa na shinikizo la damu.

Katika kundi la vijana walioisaka fursa hiyo walikuwamo wale wenzangu na mie wasiosikia la muadhini wala la mnadi sala. Hawa walijiita “magangwe” ambao ukosefu wa bidhaa ilikuwa ni fursa moja kwao. Walijenga mtandao wa kupata na kuuza bidhaa adimu kwa mwendo wa kuruka au kulangua. Magangwe waliamua kudandia meli na kujificha katika kona zake. Kwa mujibu wa baadhi yao, wengine walijichimbia kwenye bomba la moshi na kuibuka katikati ya safari. Walikubali kuwa watumwa kama ada ya safari na wakafikishwa ughaibuni.

Huko nako walikuwa watumwa waliofanya kazi zote zilizokataliwa na wazawa, wakapata fedha na kuwanunulia wazazi na wadogo zao mahitaji. Ndio wakati tulioanza kuona “viwalo” vya “Jeans” na “raba mtoni” kwa wingi. Wengine waliweza kabisa kuinua ustawi wa familia zao. Na ni wakati huu ambao kauli mbiu ya “TZ akili kumkichwa” yaani “Tanzania mtaishi kwa akili vichwani mwenu” ilithibitika. Elimu ya darasani na kazi za kuajiriwa zisingeweza kukubeba katika maisha yako ya kila siku. Tanzania ikawa Bongo.

Lakini wakati mwingine akili nyingi hushusha maarifa. Vijana waliokwenda baadaye walianza kushindana anasa. Walishindana kurudi nyumbani na magari ya kifahari kama Buick, Cadillac na Ferrari. Wakawa wakitambiana utajiri kwenye kumbi za starehe.

Lakini walikuja kuharibu pale walipokuja kuwatambia Mawaziri waliokuja na Land Rover 109 kwenye sherehe za Kitaifa pale Uwanja wa Taifa. Magari yote ya mtumba yalipigwa marufuku ili kuwanusuru vijana walioelekea kuambukizwa kansa ya “Bongo akili kumichwa”.

Ubongo wa mtu anayewaza sana unaweza kuwasha taa kwa jinsi unavyofua umeme. Lakini ubongo wa Mtanzania wa wakati ule bila shaka ungeweza kuwasha mashine ya kusaga nafaka! Wenyewe walisema mbumbumbu anayeweza kuishi Tanzania hakuwa na tofauti na msomi mwenye digirii ya chuo kikuu.

Kwa kawaida binadamu ni wabunifu na wanaoweza kuyamudu mazingira yao. Lakini wabongo ukizingatia “waya” ulivyowasugua walikuwa wabunifu “plus”. Shida humfunza mtu mambo mengi sawasawa na vile anavyopambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Narudia kusema kuwa akili nyingi ni ukichaa kwa sababu Wabongo waliacha kubuni maendeleo na kuanza kutiana ujinga. Kwa mbali inafanana na mabaharia walivyoacha kuhudumia familia na kuanza kupiga misele. Mara wabunifu wakaanza kuchezea mita za umeme, namba za luku na kadhalika.

Wakaona haitoshi. Ni ukweli usiopingika kuwa maisha ya mwanadamu wa leo yanategemea kompyuta na simu za viganjani. Sanjari na hilo, tunategemea mitandao ya kijamii kupashana habari. Wajanja wakaamua kucheza na akili za watu mitandaoni. Utaona kichwa kisemacho: “Mkuu wa Mkoa abambwa uchochoroni”.

Kwa vile michezo ya kompyuta inaweza kumhamisha Mswahili kutoka Tandale hadi Hollywood. Utaona picha ya mheshimiwa akiwa kati ya machangudoa. Ukibonyeza kwa maana ya kutaka kuona kile kilichotukia unajikuta umefungua wimbo wa msanii mchanga anayelalamikia kuporwa mke. Na inaeleweka kuwa kila unapofungua ukurasa hata kama hukukusudia basi huwa unamchangia mwenyewe hela ya kubadilisha mboga. Juzi kati ndo nikasikia kubwa kuliko nyingi. Watu sasa wanaamua kuwafundisha uhuni binti zetu kwa kuwawekea nyenzo kwenye simu zao. Unampigia binti yako anakujibu kuwa yuko msibani. Na kweli unasikia sauti za vilio na kwaya za maombolezo. Lakini kumbe anakuwa amekusetia tu ili usigundue kuwa yupo klabu akila vichwa kama konda! Haki ya Mungu hizi akili nyingi zitatumaliza…