Alama 11 za mpenzi mwenye mchepuko

Muktasari:

  • Kutokuwa mwaminifu hapa namaanisha hali ya mpenzi mmoja kuwa na mahusiano yasiyo rasmi na mpenzi au wapenzi wengine pembeni au mchepuko kwa lugha ya kisasa

Kila mmoja atakubaliana na mimi kwamba uhusiano baina ya wapendanao ulikusudiwa kuwa ya upendo, maelewano, kuaminiana na urafiki wa hali ya juu. Kwa bahati mbaya hali halisi siyo hiyo katika mahusiano ya wengi. Wengi wetu wameumizwa kwa mpenzi mmoja au mara nyingine wote kutokuwa waaminifu katika mahusiano yao.

Kutokuwa mwaminifu hapa namaanisha hali ya mpenzi mmoja kuwa na mahusiano yasiyo rasmi na mpenzi au wapenzi wengine pembeni au mchepuko kwa lugha ya kisasa

Japo jambo hili hufanyika kwa siri sana kwa kuogopa kuharibu mahusiano mtu aliyonayo, wako baadhi ambao wamegundulika na mahusiano yakaathirika kwa kiasi kikubwa na wengine yalikufa kabisa.

Wako ambao wameweza kuhimili machungu ya kugundua hali ya wapenzi wao kutokuwa waaminifu lakini pia wako ambao imewashinda kabisa kuwa wavumilivu, wako ambao hali hii imewaletea shida kihisia, kisaikolojia na hata kiafya.

Kwa bahati mbaya wengi wetu hatuzijui hata dalili au alama zozote za kutujulisha mabadiliko waliyonayo wapenzi wetu ili basi walao tuanze mapema kufanya uchunguzi au kupeana tahadhari kabla makubwa na machungu zaidi hayajatokea.

Zifuatazo nia alama zitakazokusaidia kuwa macho mara utakapoona mazingira ya kufanana nazo yanatokea katika uhusiano yenu, alama hizi nimezikusanya katika mazungumzo na baadhi ya watu niliowahi kusaidiana nao kutatua matatizo ya mahusiano yao na pia nikazihakikisha kupitia kusoma vitabu mbalimbali, kwa hiyo nina uhakika zitakusaidia kuona uhalisi wa mambo, na yamkini utaona baadhi ya alama ambazo umeshawahi kuzihisi au kuzishuhudia katika mahusiano yako.

Kuongezeka ghafla kwa hali ya kujipenda

Yawezekana mpenzi wako alikuwa amezoea kuvaa kawaida, hapa simaanishi kutopendeza, na wewe ulikuwa umemzoea katika hali fulani ya mavazi au mitindo mara ghafla anabadilika nakuwa mtanashati zaidi, ana badilisha mavazi, anapenda mavazi ya gharama, labda alikuwa hatumii manukato lakini ghafla anaanza kupenda manukato tena ya gharama, anakuwa mtu wa kujijali zaidi ya kawaida yake kiasi ambacho hukumzoea. Katika hali hii jaribu kuwa macho zaidi kufahamu nini kilicho sababisha mabadiliko ya ghafla kiasi hicho.

Kuanza kuchelewa kutoka kazini mara kwa mara

Sio kwamba kila mtu anapochelewa kutoka kazini basi anakuwa sio mwaminifu, lakini zaidi ya asilimia 75 ya ambao wamekuwa na mahusiano nje wamekuwa wakitoa visingizio vinavyohusiana na kazi, vikao, mikutano na safari za kikazi, yamkini wewe ni shahidi wa hili.

Unaweza kukuta mtu alikuwa anafanya kazi hiyo muda mrefu tu tangia muanze mapenzi yenu, mara ghafla hali inabadilika, sikuhizi anachelewa sana kurudi nyumbani, na anaporudi unaweza kutegemea utamwona amechoka kimwili na hata kiakili kwa majukumu ya kazi kuhusiana na asili ya kazi anayoifanya lakini unakuta mtu wala haonyeshi kuchoka, ana furaha kama kawaida.

Hali hii inapojitokeza mara kwa mara usichelewe kufungua macho na kudadisi mazingira maana yamkini ni kweli amepata kazi ya ziada ila siyo ile ya ajira unayoijua wewe.

Kupenda kutembea na mipira ya kinga “condoms”

Inashangaza mara nyingine kusikia mpenzi mmoja ana tabia ya kubeba kondomu kwenye pochi yake au mfukoni kwa kisingizio kuwa anajali, cha kushangaza zaidi unakuta yuko katika mahusiano na mkewe au mumewe. Yamkini ni kweli kunakujali na labda katika mahusiano yenu hili sio la kushtua kwa sababu mnajali afya zenu au mnatumia kondomu kwa sababu zaidi ya moja, lakini inakuwaje pale unapogundua kuwa ile kondomu uliyokuwa unaiona haipo tena na yamkini wewe hukuhusika katika kuitumia.

Mazingira tatanishi ya simu

Inawezekana mpenzi wako sio mtu wa kupokea simu au kupiga simu sana, na hivi ndiyo ulivyomzoea, mara ghafla simu zinaanza kumiminika mpaka mida ya usiku. Yamkini pia alikuwa yuko huru hata simu yake inapolia waweza ichukua na kumpatia lakini ghafla anakuwa na hofu kubwa na kuificha simu yake, nimeongea na wengine ambao wanakwenda na simu hadi bafuni isije ikasikika. Wengine wameanza kuondoa milio katika simu zao wakati haikuwa kawaida yao, wako ambao simu zao zikipigwa hawawezi kuzipokea na kuongea kwa uhuru kama kawaida, ataondoka na kujitenga pembeni akijifanya anaongea kiuaminifu kabisa lakini mtu uliyempenda na ukamzoea unaweza kugundua uhalisi wa anachokiongea kwenye simu na jinsia ya anayeongea naye kwa kumuangalia usoni tu. Yamkini mpenzi wako amepigiwa simu na kwa sababu hakuwepo karibu ukaipokea, na mara mpigaji wa simu anapogundua aliyepokea sio mwenye simu anakata simu hiyo ghafla, au ghafla unagundua kila simu inayopigwa kwenye simu ya mpenzi wako haionyeshi namba au haionyeshi jina. Mazingira kama haya yanapozidi basi jaribu kuchukua hatua, yawezekana kuna mvamizi tayari katika mahusiano yenu.

Itaendelea......