Alianza akiwa karani, akastaafu akiwa daktari bingwa wa watoto

Muktasari:

  • Kuna wakati wasikilizaji wakiwamo wanafunzi wakike wa shule za msingi na Sekondari walipiga makofi ya shangwe, wakaguna na wakati mwingine kuhuzunika pamoja na wasimuliaji hasa walipoelezea nyakati ngumu walizopitia.

Kila aliyekuwepo kwenye kijiwe cha simulizi za wanawake waliofikia ndoto zao za maisha yao na kuwa mfano wa kuigwa kwenye jamii, alitulia kwa makini kusikiliza.

Kuna wakati wasikilizaji wakiwamo wanafunzi wakike wa shule za msingi na Sekondari walipiga makofi ya shangwe, wakaguna na wakati mwingine kuhuzunika pamoja na wasimuliaji hasa walipoelezea nyakati ngumu walizopitia.

Simulizi ya daktari wa kwanza mwanamke hapa nchini, Profesa Ester Mwaikambo ni kati ya zile zilizovutia hisia za watu wengi.

Licha ya changamoto lukuki ambazo leo zinakatisha ndoto za maisha ya wanafunzi wengi wa kike, Profesa Mwaikambo ambaye pia amekuwa mhadhiri wa elimu ya juu alipenya.

Alianza kazi kama karani lakini sasa anastaafu akiwa Daktari Bingwa wa Watoto na mwanamke wa kwanza kuwa daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mwaka 1969.

“Usiruhusu changamoto zikuangushe, zitumie hizo kufikia ndoto za mafanikio yako,” anasema.

Tamasha la 14 la jinsia lililoendeshwa na Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) lilitumia nafasi hiyo kuwafunda wanafunzi na vijana hasa wa kike kujitambua na kuweka malengo ya kufikia ndoto zao.

“Kwa nini ukubali kuishia njiani? Kwa nini uogope masomo ya sayansi? Unawezaje kudanganywa na chipsi wakati anayekununulia naye analipiwa ada na mzazi wake kama wewe? Sikuruhusu yeyote akatishe ndoto zangu. Usiruhusu pia,” anasema Mwaikambo.

Nafasi ya kujua wakongwe hao waliwezaje kupambana na changamoto na hatimaye kutimiza ndoto zao kimaisha, ilikuwa darasa tosha ya kuona wataweza hata iwaje.

Kwa sababu ndiye aliyefungua pazia la wanawake madaktari nchini, TGNP walimpatia Tuzo ya Heshima ya Jinsia iliyokabidhiwa kwake na Makamu wa Rais Samia Suluhu.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi anasema katika mazingira ambayo wanafunzi wengine wa kike walishindwa kupambana nayo, Profesa Mwaikambo aliweza.

Licha ya umri wke wa miaka 75, Profesa Mwaikambo anajivunia kuonekana kijana.

“ “Nafanya kazi kwenye taasisi za elimu ya juu kwa sababu natamani kuona wasichana wanasoma sayansi na teknolojia wanafikia malengo yao.”

Kiuhalisia sayansi na teknolojia ina matumaini ya kutimiza ndoto za wengi kwa sababu licha ya urahisi wa kupata kazi, inawezesha kujiajiri.

Hakusoma sayasi

“Mama yangu alifariki na kutuachia mtoto akinyonya. Ilibidi dada yetu mkubwa aache shule kutulea. Huu ulikuwa mtihani wangu wa kwanza,” anasema.

Kwa kuwa alijua ukombozi wa maisha na familia yao ni elimu, hakukata tamaa. Alifanya vizuri darasani na kufaulu masomo ya darasa la nne na baadae la nane.

Katika mazingira magumu, alihitimu darasa la 12 wakati huo katika shule ya Ashira kisha kujiunga Tabora alikohitimu kidato cha nne.

“Sikufanya vizuri hivyo ikabidi nisome ukarani nikijifunza kuchapa, hati ya mkono na hii imenisaidia sana,” anasema. Hiyo inadhihirisha kwamba, ipo nafasi ya kufanya vizuri hata mtu anaposhindwa hatua moja.

“Nilifanya kazi kwenye ofisi ambayo bosi alikuwa akiniita kwa kugonga gonga na hata kupiga kelele kwa kengele. Nilikuwa nashtuka kweli kwel,” anasema na kuongeza;

“Sikukaa hata miezi sita na niliona biashara hiyo ngumu sitaiweza. Sikuwa na hata miaka 20 na wakati huo, uhuru ulikuwa ndio unakaribia,”.

Kiuhalisia,Profea Mwaikambo hakusoma masomo ya sayansi akiwa sekondari.

Aachana na ukarani

Mwanamke huyo msomi anasema aliona wazi kwamba kazi hiyo sio yake. Aliamua kuachana nayo baada ya kuona nafasi ya kwenda kusoma akilenga kubadili kazi yake ya ukarani.

“Nilipata East African Airways, nikaacha kazi masaa 24 ili niende nchini Urusi kusomea masuala ua uhudumu wa ndege,” anasema.

Anakumbusha kwamba, kitendo cha kumuona mama yake akifa polepole kwa ugonjwa ambao baadae aligundua ni saratani kilimpa mzigo moyoni mwake wa kujua sababu.

Japo hakujua anataka kusomea udaktari, alihisi lazima asomee kitu kitakachompa majibu ya tatizo lililomuondoa duniani mama yake.

“Sikuwahi kujua kama nataka kuwa daktari ila moyo wangu uliapa kwamba lazima nisome sana nilijue tatizo la mama,”anasema.

Hamu ya udaktari yamjia

Akiwa nchini Urusi, alijifunza lugha ya kirusi kwa mwaka mmoja lakini hakutaka tena kuendelea na masomo ya uhudumu wa ndege yaliyompeleka.

Anasema aliamua kusomea udaktari hivyo akataka kujua sifa za kujiunga na kozi hiyo.

Kiuhalisia hakuwa na sifa kwa sababu hakuwa kusoma masomo ya sayansi.

Kukosa kwake sifa kulimfanya arudie masomo ya sekondari lakini alisoma kwa miaka miwili tu.

Akiwa na umri wa miaka 33 aliajiriwa Muhimbili akiwa daktari wa kwanza mwanamke.

“Kuna wakati wagonjwa waliniita kwa jina la nesi na nikienda kuwasikiliza wananiambia niwaitie daktari. Niliwajibu hakuna shida lakini kwa kuwa nilishajua niliwahudumia. Ilikuwa ajabu mwanamke kuwa daktari,”anasema.

Dk Mwaikambo anasema aliweza hayo yote kwa sababu moja tu, alijitambua na kuthubutu.

Mtihani mwingine

Mtihani wa pili kwake ni wakati akiwa chuo. Anasema wakati anaendelea na masomo yake aliolewa japo alikuwa bado nchini urusi.

“Nilirudi Tanzania nikafunga ndoa na kwenda kuendelea na masomo na mume wangu tulikutana urusi,” anasema.

Anasema alipomaliza masomo yake na kurudi nyumbani alishangaa kuona mumewe ameoa mke mwingine.

“Hilo pia halikuniondoa kwenye ndoto zangu, niliendelea na maisha nikimuheshimu. Maisha yaliendelea,” anasema.

Mtihani mwingine

Profesa Mwaikambo anasema kuna wakati tafiti zake hazikupokelewa kwa madai ni mbaya kutokana tu na uanamke.

“Nililazimika kuipeleka mwenyewe kwa wasimamizi wakubwa. Maajabu nilipopeleka ikawa the ‘best’,”anasema.

Tuzo zake

Profesa Mwaikambo hakumbuki idadi ya tuzo alizopo kwa sababu ni nyingi.

Miongoni mwa hizo ni ile ya Havard African Distinguish Lectures Award 2009, Martine Luther King alipopewa mwaka 2012 nchini Marekani na Women Achievement Award (2009).