Ameamua kutumia mitandao kuelimisha

Pashal Masalu

Muktasari:

  • Alianza kutumia ukurasa wake aliouita #ElimikawekeendinaPaschal kama mzaha lakini sasa unasomwa na watu takribani 16,000 kwa siku.
  • “Niligundua kuwa ninaweza kutumia mitandao ya kijamii kuelimisha jamii na ikahamasika kuliko kuitumia kujifurahisha kwa kuweka vitu visivyoleta hamasa ya mabadiliko ya kifikra,” anasema.

Vijana wengi hutumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kuonyesha maisha yao binafsi na kuweka picha zisizokuwa na maadili, lakini kwa Pashal Masalu (25) ni tofauti kwani anatumia ukurasa wake wa Twitter kuelimishia jamii katika masuala mbalimbali ya kiafy na utunzaji mazingira.

Alianza kutumia ukurasa wake aliouita #ElimikawekeendinaPaschal kama mzaha lakini sasa unasomwa na watu takribani 16,000 kwa siku.

“Niligundua kuwa ninaweza kutumia mitandao ya kijamii kuelimisha jamii na ikahamasika kuliko kuitumia kujifurahisha kwa kuweka vitu visivyoleta hamasa ya mabadiliko ya kifikra,” anasema.

Pamoja hatua hiyo alibadilisha jina la ukurasa wake huo na kuupa jina jipya la #Elimikawikiend ambao hadi sasa una wafuasi 15,000.

Anasema wakati yupo kidato cha tano alikuwa anatumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuangalia mambo mbalimbali ambayo hayakuwa na manufaa kwake.

“Nilikuwa natumia muda mwingi kuangalia taarifa ambazo hazijanifunza kitu zaidi ya kuangalia picha na habari nyingi za wasanii hasa katika mtandao wa Facebook,” anasema.

Anasema tangu awe ana ukurasa wake wa Twitter amegundua kuwa mitandao ya kijamii kama itatumika vizuri inaweza kuleta mafanikio katika jamii kwani mwitikio ni mkubwa kwa watu wanaosoma habari zake anazo zisambaza kwa jamii.

“Natumiwa maoni na watu mbalimbali kuhusiana na habari ninazo zituma katika ukurasa wangu, mfano ninapotuma ujumbe unaohusu afya, wengi wanaguswa na mada niliyoijadili,” anasema.

Safari yake ya kuelimisha

Desemba 2015, Paschal alinza kusambaza habari katika ukurasa wake wa Twitter.

Anasema alianza kutuma habari za mazingira akihamsisha juu ya utunzaji.

“Ni mwaka mmoja tu tangu nimefungua ukurasa huu lakini nimepata watu takribani 15,000 kwa hiyo nimeona jinsi gani watu wanahamasika na utoaji wa elimu kwa njia ya mitandao ya kijamii,” anafafanua

Mafanikio

Anasema inamtia moyo kuona wadau takribani 15,000 wanasoma alichokiandika na kwamba anaamini azma yake ya kubadili watu kifikra inafikiwa.

Anasema: “Mafanikio siyo lazima mtu apate fedha au kitu, kukubalika kwa kile anachokifanya hata kama hakimpi fedha ni mafanikio makubwa.”

Siri ya mafanikio

Paschal anasema siri ya mafanikio yake ni kujituma na kutokata tamaa kwamba wakati anaazisha #Elimikawikiend hakutegemea angefikisha wasomaji 15,000 kwa kuwa aliona ni jambo ambalo hufanya na watu wenye hadhi fulani.

“Mara nyingi nilikuwa mbunifu na mbinu niliyoitumia na kuangalia kurasa za wenzangu wanavyoandika baada ya kuona wengi wanatuma habari za burudani, ndipo nilipoamua kuingia katika uhamasishaji wa jamii na watu wakaitikia.”

Ndoto zake hapo badae

Paschal ambaye amemaliza shahada ya masuala ya benki na fedha katika chuo cha IFM mwaka 2016 anasema ndoto yake na shirika la uhamasishaji jamii.

Wito wake kwa vijana

Anasema vijana wamezoea kazi za kuajiriwa pasipo kujua kwamba ajira sasa hivi ni ngumu.

Anasema anawashauri pia vijana kutotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kutumia lugha chafu au picha zisizo na maadili.

Paschal anaishauri serikali iwachukulie hatua wale ambao wanatumia mitandao ya kijamii vibaya.

Historia yake

Paschal ni mtoto wa tano katika familia ya watoto saba, alianza elimu yake ya msingi shule ya Solomon Mahlangu ambayo sasa inaitwa Chief Albert Ruthuli na kumaliza 2006 na alifanikiwa kujiunga elimu ya sekondari mwaka 2010 na kumaliza mwaka 2013 alijiunga na kidato cha tano mwaka 2011 na kumaliza kidato cha sita mwaka 2013 na hatimaye elimu ya chuo kikuu ambapo alimaliza mwaka 2016