Balozi Mpungwe: Adui wa maendeleo ya Tanzania ni Watanzania wenyewe

Balozi Ami Mpungwe

Muktasari:

Anataja watu kuwa na ubinafsi, rushwa na kukosekana kwa uwazi katika matumizi ya rasilimali hasa madini

Miaka zaidi ya 10 iliyopita ilishawahi kuvuma habari kuwa Balozi Ami Mpungwe ‘ameuza nchi kwa wawekezaji.’ Maneno hayo hayakutoka hewani.

Sehemu kubwa ya wananchi walikuwa wakimhusisha na mchakato wa ubinafsishaji uliokuwa ukiendelea miaka 1990 na 2000 wakati wa mpango wa kuboresha uchumi kupitia mfumo wa kiliberali.

Mpungwe akiwa balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Botswana, Namibia na Lesotho kati ya mwaka 1994 hadi 2000 alifanikisha kuwaleta wawekezaji nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo madini kutoka Afrika Kusini ambao kwa bahati mbaya baadhi ya wananchi walishindwa kutambua umuhimu wao.

Pamoja na ukosoaji huo, Balozi Mpungwe hajutii hata kidogo uamuzi wake. Anafurahia kazi yake aliyoifanya hata kama wataendelea kumkosoa kwa yaliyotokea miaka ya nyuma.

“Wanasema niliuza nchi sijui bei gani. Najivunia nilifanya vyema, sijali hata waseme maneno gani,”anasema Mpungwe.

“Mimi leo nataka aje balozi mwingine alete wawekezaji wengi kuliko mimi wachangie ukuaji wa uzalishaji, aongeze ajira na kuleta viwanda.”

Mpungwe ambaye ni mfanyabiashara maarufu nchini, anasema wawekezaji hao aliowaleta walikuja kuwekeza kwenye mashirika yaliyobinafsishwa ambayo hakuhusika nayo moja kwa moja zaidi ya tume ya ubinafsishaji mashirika ya umma (PPRSC) iliyokuwa chini ya ofisi ya Rais.

Anasema tume hiyo ilikuwa ina uongozi wake hivyo lilikuwa ni jambo la ajabu kuendelea kumwingiza kwenye jambo ambalo hausiki nalo moja kwa moja.

“Balozi ni tarishi tu anayetumwa. Nilitumwa kuhamasisha wawekezaji waje. Hicho ndicho nilichofanya na nilifanya vyema katika kiwango kikubwa,” anasema.

Anasema alistaafu akiwa na miaka 48 na ingekuwa utendaji wake mbovu isingekuwa tabu kuondoka serikalini, lakini ilichukua muda mrefu kuruhusiwa na Rais kumkubalia astaafu katika umri mdogo.

Adui wa maendeleo ya Watanzania

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, kigogo huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, anasema adui wa maendeleo ya “Watanzania ni Watanzania wenyewe.”

Hata baada ya kurejea nchini mwaka 2000, kazi za Balozi Mpungwe zilizoendelea, zilizidi kukosolewa hasa baada ya kujitosa kwenye usimamizi wa biashara ya madini.

Tangu mwaka huo, Mpungwe alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya TanzaniteOne Ltd ambayo alisaidia uanzishwaji na uendelezwaji wake.

Habari za Tanzanite zinampa machungu balozi Mpungwe na hadi leo anashukuru kuwa nje ya biashara hiyo.

Anasema vurugu zilizoibuka Mirerani zilikuwa ni matokeo ya kusimamia misingi ya utawala bora katika mashirika kwa kuimarisha uwazi, uwajibikaji na siyo vinginevyo.

Anasema jambo linalomuumiza zaidi kwa sasa ni Tanzania kuwa nchi pekee inayozalisha Tanzanite, lakini hakuna kiwanda cha uzalishaji madini hayo kwa sababu ya maslahi ya watu wachache.

“Kama wazalishaji pekee wa Tanzanite, Tanzania tulitakiwa tuwe chanzo cha bei ya madini hayo lakini tumegeuka wapokeaji wa bei zinazotoka nje nchi ambao hawazalishi,” anasema balozi Mpungwe.

Katika maelezo yake, anasema hadi sasa hakuna takwimu za uhakika juu ya kiwango halisi cha uzalishaji madini hayo, kinachouzwa na mapato kwa Taifa kutokana na baadhi ya kampuni zinazohusika kuficha taarifa kwa makusudi.

Huku akitumia mifano mbalimbali ya utawala ikiwamo kuweka hadharani takwimu zao, Mpungwe anasema kuwa kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya watu kuwakalia kooni na kuonekana wameuza nchi.

Uwazi katika madini

Suala la uwazi na rushwa katika sekta ya madini limezidi kuirudisha nyuma Tanzania katika medani za utawala bora, huku ripoti ya Transparency International ya mwaka jana ikionyesha inashika nafasi 117 ulimwenguni nafasi mbili zaidi juu kutoka ile ya mwaka 2014.

Mpungwe ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Richland Resources iliyokuwa ikimiliki TanzaniteOne, anasema hata makaburu aliokuwa akihusishwa nao walikuwa na umiliki wa asilimia moja na sehemu kubwa ilikuwa ikimilikiwa na taasisi ikiwamo mifuko ya hifadhi ya jamii ya Uingereza.

Suala la uwazi katika sekta ya madini limekuwa mwiba nchini na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Rais John Magufuli aliahidi kupambana na wawekezaji wanaokwepa kubainisha viwango halisi vya madini, mapato na fedha wanazochangia serikalini.

Anasema ana furaha kwa sasa kwa kuwa hayupo kwenye biashara ya Tanzanite anayoona ingemtoa macho kwa kuwa utaratibu wa kurasimisha sekta hiyo kwa kutangaza kila jiwe la madini lililotoka, ulionekana kuwa dhambi kwa baadhi ya wafanyabiashara ndani ya nchi.

“Dhambi kubwa tuliyofanya ni kurasimisha hii sekta kwa kulipa kodi, kutunza mazingira, kutoa ajira na kuweka rekodi ya kila tunachopata.

“Tulionekana nuksi hatufai. Kuna mfumo upo gizani kwenye sekta ya madini wenye nguvu. Hilo ndiyo jipu kweli nadhani ni tezi kabisa,” anasema balozi huyo ambaye ameshika nafasi za uongozi katika bodi mbalimbali za mashirika na kampuni nje na ndani ya nchi.

Balozi Mpungwe aliyewahi kuwa mtumishi wa umma kabla ya kustaafu na kuingia kwenye biashara, anaeleza kuwa kwa rasilimali zilizopo Tanzania hakuna sababu ya nchi kuendelea kuwa maskini.

Idadi ya watu takriban 50 milioni, mifugo na utalii, kwa mujibu wa balozi huyo, ni utajiri tosha unaoweza kuifanya nchi kuwa katika ngazi za juu za maendeleo.

“Leo hii Tanzania tuna takriban asilimia 30 ya maji ya baridi ulimwenguni, lakini bado wananchi wake wanatembea umbali mrefu wakisaka maji vijijini na majini…kote hakuna ahueni,” anasema.

Balozi Mpungwe anabainisha kuwa ushiriki wa kikanda wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ni mtaji mkubwa wa soko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.

Hoja ya mwanadiplomasia huyo kwa sasa inazidi kuwa na mashiko kutokana mfumo wa kidiplomasia kuhama kutoka ule wa kisiasa pekee hadi kwenda kwenye mrengo wa kiuchumi.

Katika hilo, Mpungwe anasema Serikali haina budi kuimarisha safu yake ya wataalamu katika balozi zake ulimwenguni kwa kuwaweka wenye uelewa mkubwa wa masuala ya biashara na uchumi.