Anguko la Mugabe, nguvu ya mwanamke na siasa za Afrika

Mwanaume hajawahi kuwa salama mbele ya mwanamke mwenye kutaka kutimiza lengo lake. Pamoja na yote bado wanaume hujiamini kuwa wao ndiyo wenye nguvu, akili na ujasiri wa kutenda, kisha huwadharau wanawake kwamba ni dhaifu, waoga na stahili yao ni kutawaliwa tu.

Ni jeuri hiyo ya kujidanganya waliyonayo wanaume, ndiyo ilimfanya gwiji wa muziki wa Soul, James Brown, mwaka 1966 kutoa wimbo “It’s a Man’s Man’s Man’s World”, akimaanisha kuwa dunia ni ya mwanaume.

Katika wimbo huo ambao Brown aliimba na Betty Newsome, waliimba kuwa magari, treni, barabara, umeme, ndege na kila kitu vimeletwa na mwanaume. Hata hivyo, wanaimba kwamba dunia haiwezi kuwa tamu kwa mwanaume bila uwepo wa mwanamke.

Tangu Kabla ya Kristo (BC), dunia imekuwa ikishuhudia nguvu ya mwanamke inavyoweza kumwingiza mwanaume kitanzini akijiona na kwa ridhaa yake. Samson na nguvu zake zisizomithilika, alikuwa laini kwa Delila licha ya kuonywa na wazazi wake, mwisho akatobolewa macho na kugeuzwa kipofu.

Rais wa 29 wa Marekani, Warren Harding kabla ya kushika madaraka alikuwa amekata tamaa ya kupata tiketi ya kuwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Republican, hivyo aliandika barua ya kujitoa. Mkewe, Florence Harding aliichana barua hiyo kisha akamwambia mumewe: “Mume wangu hapaswi kuwa mtu wa kukata tamaa na kujitoa kwenye mbio.”

Haitoshi, Florence alitumia ujanja wake wa kucheza na vyombo vya habari kuwachafua wagombea wengine ili kumpa sifa mume wake ambaye alikuwa hafikiriwi hata kati ya watatu wenye nafasi ya kupitishwa na chama.

Ni mpango huo uliofanikisha wagombea waliokuwa na nafasi kubwa kuondolewa kwa kashfa ya matumizi makubwa ya fedha kwenye uchaguzi. Mwisho Harding alipitishwa na chama kisha akachaguliwa kuwa Rais wa 29 wa Marekani.

Tuendelee; baada ya Harding kushinda urais, Florence alikuwa kila kitu mpaka ikaripotiwa na vyombo vya habari kuwa nchi ilikuwa inaendeshwa na mke wa Rais. Mwisho Harding alifariki ghafla kwa kifo kinachoaminika kuwa alipewa sumu na Florence, kisha mwanamke huyo akapiga marufuku mwili wa Harding kuchunguzwa.

Tukio la Zimbabwe

Grace Mugabe ni mke wa Rais aliyewekwa kuzuizini nyumbani kwake, Robert Mugabe. Grace alijaribu kupita njia iliyomgharimu Rais wa 10 wa Ufilipino, Ferdinand Marcos na kung’olewa madarakani. Mke wa Marcos, Imelda Marcos baada ya kuona mume wake amedhoofu kiafya, alianza kuchukua hatua za kumrithi.

Imaendelea uk 26

Hata katika kifo cha aliyekuwa kiongozi wa upinzani Ufilipino, Ninoy Aquino alitajwa Imelda kuhusika, ikielezwa lengo lilikuwa kumaliza nguvu za watu wenye uwezekano wa kumrithi Marcos ili kujitengenezea nafasi ya kuwa Rais baada ya mume wake.

Jitihada za Imelda ambazo zilikwenda pamoja na kumtia ‘upofu’ Marcos kung’ang’ania madaraka hata baada ya kushindwa mwaka 1986, huku afya yake ikiwa dhaifu, ndiyo sababu ya kiongozi huyo kupinduliwa kwa aibu na wananchi.

Imelda aliota mapembe mpaka akajiona ndiye msemaji wa Serikali. Akawa mtapanya pesa za umma na aliishi maisha ya kifahari mpaka kuogopwa. Wakati mumewe anapinduliwa, alikutwa na jozi za viatu zaidi ya 2,700.

Kama Imelda, Grace naye akataka kumrithi Mugabe ili naye atamkwe Rais. Kasi ya Grace kujichomeka kwenye chama na kugombana na wasaidizi wa mume wake ilipanda kwa kiasi cha kumwogopesha kila mtu. Mugabe hakumdhibiti mkewe, akamwacha atende atakavyo.

Kama Imelda, Grace akashutumiwa kwa kuishi kifahari na kujilimbikizia mali nyingi, huku kiasi kikubwa akiwa amekificha Malaysia. Kama Imelda alivyosababisha Marcos achukiwe na wananchi, Grace amekuwa sababu ya Mugabe kuonekana hafai wakati alikuwa kiongozi lulu kwa Wazimbabwe na Afrika kwa jumla.

Kama Imelda alivyotumia mwanya wa udhaifu wa afya ya Marcos kutaka kurithi urais wa Ufilipino, Grace naye aliutumia uzee wa Mugabe kujiandalia mazingira ya kujisimika uraisi. Ni jitihada hizo ambazo zilimfanya aguse pabaya na kusababisha mumewe awekwe kando.

Kwa yaliyomkuta Mugabe kama Marcos kupitia wake zao, Grace na Imelda, ujumbe ni mmoja tu; tamaa huwa na matokeo mabaya. Wanawake hao waliona kuishia kuitwa wake wa rais haivutii mpaka wawe marais kamili.

Anguko la Mugabe

Novemba 6, mwaka huu, sinema ya anguko la Mugabe ilianza alipomwondoa kazini aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Emmerson Mnangagwa kwa kile kilichoelezwa ni kutengeneza mipango miovu dhidi ya Serikali.

Hata hivyo, ukweli ambao ulikuwa dhahiri ni kuwa kuondolewa kwa Mnangagwa ilikuwa kumwandalia nafasi Grace kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, ikiwa ni hatua iliyokosa soni kuelekea kumpa urais wa nchi hiyo baada ya mumewe.

Mnangagwa aliondolewa si kwa bahati mbaya au kwamba alionewa, la! Ilikuwa inafahamika kuwa Mnangagwa naye alikuwa anajiandaa kuchukua mikoba ya Mugabe ambaye alishaonekana kuwa yupo ukingoni kiumri.

Hatua ya Mugabe, 93, kumwondoa Mnangagwa iliwachukiza wengi, ikionekana kuwepo na hali ya kuifanya Serikali ya Zimbabwe na mamlaka ya utawala wa nchi kuwa mali ya familia. Mzozo ukaanza ndani ya chama tawala, Zanu-PF.

Mnangagwa baada ya kuona usalama wake upo shakani, alikimbilia Afrika Kusini. Novemba 8, mwaka huu, Mugabe na Grace kupitia Zanu-PF walifanya mkutano wa hadhara jijini Harare na kumnanga Mnangagwa. Mugabe alisema, Mnangagwa alitaka kupita njia ya mkato kurithi urais.

Mugabe alisema Mnangagwa alifanya kosa kama la Joice Mujuru kutaka kupita njia ya mkato kuwa Rais. Mujuru alikuwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe kwa miaka 10 kabla ya Mugabe kumuondoa mwaka 2014. Mugabe alimtuhumu Mnangagwa pia kwa kumwendea kwa waganga wa kienyeji.

Grace acheka mamba

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, ni mpigania uhuru shupavu wa Zimbabwe. Ni mmoja wa watu wachache ambao wamekula vizuri mkate wa nchi kama sehemu ya wapigania uhuru. Ni mwanajeshi na jasusi aliyepewa mafunzo Zimbabwe na China.

Kumfananisha Mnangagwa na Mujuru lilikuwa kosa kubwa kufanywa na Mugabe pamoja na Grace. Uzuri ni kuwa Mugabe alimfahamu kwa undani Mnangagwa kwa sababu amekulia kwenye mfumo chini ya utawala wake na alishamtumia kutekeleza mipango mingi ya kijasusi.

Mnangagwa ni wa jamii ya Karanga ambayo ni kundi dogo kwenye kabila la Washona. Wakaranga huamini mamba ni mnyama mwenye nguvu kubwa kiroho, hiyo ndiyo sababu kwa jina la utani la Mnangagwa huitwa mamba na wafuasi wake kisiasa hujiita Lacoste kwa sababu mavazi ya kampuni hiyo huwa nembo ya mamba.

Hivyo, mkutano wa Mugabe na Grace kupitia Zanu-PF ambao agenda yake ilikuwa kumnanga Mnangagwa, tafsiri yake ilikuwa kucheka mamba kabla ya kuvuka mto, maana Mnangagwa ni mamba. Kilichotokea Grace na Mugabe wamemezwa na mamba.

Mnangagwa ni mwenye ushawishi mkubwa ndani ya mfumo wa usalama na Jeshi la Zimbabwe. Zaidi, Mnangagwa ni rafiki hasa wa Mkuu wa Jeshi la Zimbabwe, Constantino Chiwenga ambaye kwanza alimuonya Mugabe kuhusu vitendo vyake kisha Novemba 15, mwaka huu akamweka kizuizini.

Hata sasa, Mnangagwa ndiye inaaminika atakuwa Rais wa mpito, kwa hiyo yeye ndiye mshindi wa mtifuano wa kuwania kumrithi Mugabe. Zaidi Grace amemponza mumewe na familia yake kwa tamaa zake za kumuona mume mzee hivyo kumpelekesha bila tahadhari.

Anguko la Mugabe na Afrika

Aprili 2011, Laurent Gbagbo alitiwa nguvuni baada ya kugoma kuachia madaraka baada ya kushindwa na Alassane Ouattara nchini Ivory Coast. Alikutwa amejificha na mkewe, Simone Gbagbo, wakiongopeana kuwa wangevuka.

Kama Gbagbo na Simone, ndivyo Mugabe na Grace walifikia tamati. Hii ni shule kuwa hakuna mamlaka ya nchi yenye hatimiliki ya familia. Tatizo viongozi wengi Afrika wanajisahau mno, matokeo yake Afrika ndiyo bara linaloongoza katika Karne ya 21, viongozi wake kung’olewa kwa lazima.

Uganda, Yoweri Museveni kwa utawala wake wa miaka 31, haoni kama imetosha kupumzika. Hivi karibuni Kanisa lilijitokeza na kueleza kuwa inaonekana Museveni hajafikisha umri alionao sasa, ili apate kukidhi masharti ya Katiba na kugombea tena urais kwenye uchaguzi ujao. Hili lilifanyika nje ya mpango ya kubadili Katiba kufuta ukomo wa umri unataka kufanywa na Bunge la Uganda.

Kama Mugabe na Grace, Museveni naye ameona Serikali ya Uganda ni kama mali ya familia yake, kwani mwaka jana alimteua mkewe, Janet Museveni kuwa Waziri wa Elimu, wizara ambayo bajeti yake ni kubwa mno, vilevile mtoto wake, Muhoozi Kainerugaba amempandisha madaraja jeshini hadi Meja Jenerali, kisha akamteua kuwa mshauri wa Rais.

Katika kuonyesha kuwa Museveni ameamua Uganda iwe mali ya familia yake, taarifa zipo dhahiri kuwa anamwandaa Kainerugaba kuwa Rais wa Uganda baada yake. Sawa na Muammar Gaddafi baada ya kuitawala Libya kwa miaka 42, akawa anamwandaa mwanaye, Saif Al-Islam kuwa mrithi wake. Hiyo ndiyo Afrika.

Kitabia viongozi wengi wa Afrika ama hufanana au huigana, ni kama wake wa watawala ambao wametokea kuwaponza waume zao, nao ni hulka sawa. Huongea mpaka kuharibu. Grace alitamba kuwa Wazimbabwe wangemchagua Mugabe aendelee kutawala hata akiwa kitandani hajiwezi kwa uzee.

Mke wa Mfalme Louis XVI, Marie Antoinette, mwaka 1793 alikuwa sababu ya mume wake kupinduliwa na wananchi kwa sababu ya kuwajibu wananchi wenye njaa kwa dharau. Wananchi wanazunguka jumba la Mfalme kudai hawana hata mikate ya kula, yeye akasema: “Kama hawana mikate wakale keki.”

Hufanana sana, Marie Antoinette alikuwa mpenda starehe na mtapanya pesa kama Grace ndiyo maana Zimbabwe akaitwa Grace Gucci, sawa na Imelda Marcos aliyeitwa Kleptocrat, yaani tajiri mwizi wa mali za umma.

Mwanazuoni wa Kenya, Profesa Patrick Lumumba amekuwa akisema kuwa Mugabe alipokuwa na mke wake wa kwanza, Sally Hayfron, ambaye ni mpigania uhuru mwenzake, alikuwa kiongozi bora mno, Sally alipokufa mwaka 1992 na Grace kuingia kwenye maisha ya Mugabe kila kitu kilibadilika.