Tuesday, October 24, 2017

Anna : Hata sijui nilivyofaulu darasa la saba!

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

“Nikuulize swali mwenyewe. Hivi kwani mimi nilifauluje? Najiulizaga kila siku ila hata sipati jibu, sijui nilifauluje”.

Achana na makosa ya kisarufi ya maneno nilifauluje (nilifaulu vipi) na naulizaga (nauliza), kimsingi, swali lenyewe halikuwa rahisi kulijibu.

Ni swali aliloniuliza Anna Matonya (16), ambaye alipaswa kuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Magaga iliyopo wilayani Bahi katika Mkoa wa Dodoma.

Imepita takriban miezi miwili tangu aamue kuacha shule, anataka kufahamu namna alivyoweza kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana baada ya kuhitimu katika Shule ya Msingi Chifutuka.

Hatua yake ya kuamua kuacha masomo inatokana na madai yake kwamba akiwa shuleni hakuwa akielewa chochote darasani.

Siyo kwamba hajui kusoma na kuandika, La hasha! isipokuwa analalamika aliwezaje kufaulu darasa la saba kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kuyamudu masomo.

Lakini akiwa sekondari mzigo ukazidi kumwelemea hasa pale lugha ya Kiingereza ilipokuwa ikitumika kufundishia. Anasema haelewi.

Anasema anaumizwa kushika mkia katika matokeo ya mitihani yake na kusababisha kupewa adhabu huku akichekwa na wanafunzi wenzake.

“Afadhali shule ya msingi nilijifunza kwa Kiswahili na sio sekondari, maana nikienda darasani siambulii kitu,”anasema na kuongeza:

“Kila siku nakuwa wa mwisho, walimu wakifundisha sielewi hata kidogo. Wakiongea Kiingereza ndio kabisa kama napotea, ndio maana nimeamua kukimbia shule”.

Anna anasisitiza kwamba haelewi ilikuwaje jina lake likawa miongoni mwa majina 31 ya wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka huu.

“Tupo 31 darasani, kila tukifanya mitihani nakuwa wa mwisho na kuchapwa viboko, kwa hiyo sitaki tena kusoma bora nimsaidie mama kazi za nyumbani,” anasema.

Anasema amejitahidi kusoma kwa bidii ili walau aendane na wenzake, lakini bado aliambulia nafasi ya mwisho jambo lililomkatisha tamaa ya kuendelea na masomo.

Anasimulia kwamba alijaribu kuwaambia wazazi wake kuhusu mwenendo wake kielimu, lakini hawakumwelewa na badala yake walimsihi aendelee na shule kwa kuwa ndio msingi pekee wa maisha yake.

“Hakuna aliyenisikiliza, baba na mama wote wanataka niendelee kusoma sekondari, sasa nitasomaje wakati sielewi chochote? Mimi sitaenda tena ila ningekuwa naelewa ningeendelea,”anasema na kuongeza:

“Nilienda porini, sikuogopa chochote kwa sababu nimechoka kuchekwa kwa kuwa wa mwisho darasani”.

Muundo wa mtihani wakosolewa

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifutuka, Daniel Mchomvu anasema muundo wa maswali ya kuchagua unaotumika sasa katika mtihani wa taifa wa darasa la saba, ndio unaosababisha wanafunzi wengi wasio na uwezo kufaulu akiwamo Anna.

“Unaweza kumkuta mtoto anabuni jibu na kufaulu, ndio maana wanaokwenda sekondari wengi hawana uwezo kama binti huyu amejikuta haendani na wenzake,”anasema.

Wadau mbalimbali wa elimu wanasema mabadiliko ya muundo wa mtihani huo, ndio unaosababisha kuwapo kwa wanafunzi wanaochaguliwa sekondari huku baadhi wakiwa hawajui stadi za msingi za kusoma na kuandika.

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati nchini (MAT/CHAHITA, Dk Said Sima anasema, Serikali ifanyie kazi maoni ya wadau ya kubadilisha mfumo huo kwa sababu unaua taaluma ikiwamo somo la Hisabati kwa sababu wengi wanaofaulu hawana uwezo.

Mchambuzi wa masuala ya elimu, Frank John anasema kilichosababisha mfumo huo kuanza kutumika ni matumizi ya mashine wakati wa kusahihisha. Ni mfumo uliowekwa makusudi kwa ajili ya kurahisisha kazi ya usahihishaji

Anasema: “Ni mfumo mbaya usiomuandaa mtoto. Hii ni hatari kwa Taifa.’’

Hata hivyo, Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Bahi, Hassan Mohamed anatetea muundo wa mitihani hiyo kwamba haina ubaya wowote. “Asiyejua kusoma na kuandika hawezi kujibu. Nchi zaidi ya 13 zinatumia utaratibu huu kwa hiyo sio muundo mbaya,”anasema.

Wazazi wasononeka

Akiwa miongoni mwa wanafunzi wasichana waliopangiwa vyumba mtaani katika kijiji cha Magaga, wazazi wake wanasema wamekuwa wakimpatia binti yao mahitaji yote.

“Mwanangu ananisikitisha sana, huyu ndiye niliyemtegemea walau, nilijua akisoma atawasaidia wadogo zake lakini ndio kama unavyosikia,” anasema baba yake Julius Matonya, mkazi wa kijiji cha Chikopelo.

Ilimlazimu Matonya kuwaomba walimu, viongozi wa serikali ya kijiji na majirani zake waongee na binti yake ili aendelee na masomo lakini haikuwezekana.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifutuka, Gasper Mhembano anakiri kushiriki katika kumashwishi Anna aendelee na masomo, lakini anasema ushauri wake pia uligonga mwamba kwani alikataa kata kata.

Baada ya kuona analazimishwa kuendelea na masomo, Anna aliamua kukimbilia porini ambako alikaa huko siku mbili kuepuka karaha ya kutakiwa aende shule.

Wapita njia ndio waliomuona Anna akiwa amejilaza porini. Walimfuata na kumbembeleza arudi nyumbani, akakubali.

Mama mzazi wa Anna, Peris Matonya anasema jamii inayowazunguka iliamini kwamba binti yake huyo ameacha masomo ili aolewe na kwamba alipotoroka wengi walidhani kwamba amekimbilia kwa wanaume.

Hata hivyo Anna mwenyewe anasema: “Sitaki kuolewa mimi ila pia sitaki shule maana sielewi darasani”.

Mama huyo anasema kazi pekee anayoweza kuifanya mwanawe baada ya kuacha masomo ni kupika pombe. “Mimi napika pombe kama unavyoniona, amerudi nyumbani hakuna namna atanisaidia hii kazi tu,”anasema.

Kwa upande wake, Anna anaona bora akasome shule ya fundi, lakini wazazi wake wanasema kwa sasa hawana fedha za kumsomesha kwa kuwa waliwekeza kwenye elimu yake ya sekondari hivyo asubiri hadi watakapopata fedha.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Daudi Gingi anasema sio Anna peke yake, baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaopelekwa baada ya kufaulu huwa hawana uwezo.

Matonya anakiri kuwa maendeleo ya binti yake shule ya msingi hayakuwa mazuri, lakini matokeo ya kufaulu mtihani wa darasa la saba yalimtia moyo kwamba huenda alibadilika.

“Nilijua atafeli kwa sababu alikuwa anapata 10 au 20…alipofaulu nilimshukuru Mungu nikawekeza akili zangu kwenye shule yake matokeo yake anatuambia kwamba haelewi,”anasema.

Necta yatoa neno

Ofisa mitihani mwandamizi wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Yustine Balyuha anasema mfumo huo unapitiwa upya ili kuona namna ya kuubadilisha.

“Tunapitia upya kuona namna tunavyoweza kubadili mfumo huu, japo sio rahisi kwa mtoto asiyejua kufaulu kama inavyosemekana,”alisema katika mkutano wa wadau wa hesabu uliofanyika hivi karibuni.

-->