Asilimia 71 ya wanawake wanaotumia dawa za kulevya wana VVU

Muktasari:

  • Ni sehemu ya simulizi ya kusisimua ya msichana Diana James (23), anayeishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) ambaye pia ni mwathirika wa dawa za kulevya.
  • Kuna wakati alilazimika kuuza mwili wake ilimradi tu apate fedha za kumudu gharama ya dawa za kulevya na kutibu hali ya uhitaji iliyomkabili kwa wakati huo.

“Kwa sababu kaka yangu alikuwa akitumia dawa za kulevya, haikuwa kazi ngumu kujifunza. Nilipofikisha umri wa miaka 20 nilikuwa siwezi kuishi bila kuvuta, nilifanya lolote niwezalo ilimradi nitulize kiu kali iliyonipata, matokeo yake ni kilio na mateso makubwa! najuta, ”

Ni sehemu ya simulizi ya kusisimua ya msichana Diana James (23), anayeishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) ambaye pia ni mwathirika wa dawa za kulevya.

Kuna wakati alilazimika kuuza mwili wake ilimradi tu apate fedha za kumudu gharama ya dawa za kulevya na kutibu hali ya uhitaji iliyomkabili kwa wakati huo.

Wakati mwingine, alilazimika kuiba fedha nyumbani kwao na kwa yeyote atakayejisahau jambo lililohatarisha zaidi maisha yake.

Imefikia hatua hajiwezi, mwili wake umeshadhoofika.

Hana tena uwezo wa kuuza mwili wake ili apate dawa za kulevya zinazozidi kupanda bei kutokana na oparesheni ya kupambana na dawa hizo inayoendelea.

“Nimekonda, nimedhoofika sana, sina uwezo wa kujiuza tena….nimeharibika kupita kiasi. Nilichoamua ni kumrudia Mungu wangu naamini yeye anayo kauli yangu ya mwisho. Kwake kuna msamaha,” anasema Diana.

Haikuwa kazi ngumu kwake kujifunza kutumia dawa za kulevya kutokana na mazingira aliyokulia.

Hata hivyo imekuwa kazi ngumu kuacha, japo kwa sasa hushinda ila bado kuna wakati akipata hamu kali ya dawa hizo, huwa analazimika kuzitafuta na akikosa basi huwa anatumia pombe kali kama ‘viloba’, walau kiu hiyo imalizike.

Sio Diana peke yake, wapo wasichana wengi waliojikuta kwenye wakati mgumu kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa sababu dawa hizo zimeshawazoea hawawezi tena kuacha na badala yake wanalazimika kufanya vitendo vinavyo hatarisha afya zao ili wapate fedha na kumudu mahitaji ya miili yao.

Mwanamke mwingine, Aisha Juma (28) sio jina halisi anasema miaka mitano imepita tangu apate maambukizi ya Ukimwi.

Anasema msongo wa mawazo na makundi rika ndio yaliyochangia kujiingiza kwenye matumizi ya dawa hizo ambazo hadi sasa hajaweza kuacha.

“Siwezi kujiuza kwa sababu naumwa, na kibaya zaidi mwili umedhoofika hivyo nimebaki kuteseka,”anasema.

Daktari Bingwa Mwandamizi wa Tiba na Afya ya Akili, Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Frank Masao anasema ni rahisi zaidi kwa mtumiaji wa dawa za kulevya kupata mambukizi ya Virusi vya Ukimwi, magonjwa mengine ya zinaa na kukumbwa na magonjwa nyemelezi.

Akielezea Ukimwi na magonjwa ya zinaa kwa wanawake, Dk Masano alisema mtumiaji anapokosa fedha za kununulia dawa huwa analazimika kutumia njia yoyote ikiwamo kujiuza mwili wake, ili tu apate dawa za kulevya.

Anasema mtu anayetumia dawa za kulevya kama Heroin na Cocain hazipatikani kwa urahisi, ni gharama sasa kwa mwanamke ambaye dawa hizo zimemzoea.

“Mtumiaji mzoefu huwa anatumia kete 10 hadi 20 kwa siku, na wakati huo kete moja inauzwa Sh3,000 hadi 5,000. Hivyo hujikuta anatumia 60,000 fedha ambayo wakati mwingine anakosa. Ikifikia hatua hiyo hapo hulazimika kufanya chochote apate pesa na ndipo hatari inapokuja,” anasema.

“Njia mbadala ya mwanamke kupata fedha ni kwenda kuuza mwili wake, kwa hiyo athari ya kwanza huwa inaanzia hapo,”anasema Dk Masao.

Akitoa takwimu, Dk Masao anasema utafiti walioufanya mwaka 2004, walibaini kuwa watu wanaotumia dawa hizo kwa njia ya kujidunga, maambukizi ya Ukimwi yalikuwa asilimia 42.

Lakini wanawake maambukizi ya Virusi vya Ukimwi yalikuwa ni asilimia 62.

“Ukiangalia takwimu za mwanzoni mwa miaka ya 2010, katika utafiti wetu wa Kinondoni, Dar es Salaam tuligundua asilimia 51 ya watu wanaojichoma heroin wanamaambukizi ya Virusi vya Ukimwi, lakini kati yao wanawake walikuwa ni asilimia 71,” anasema.

Anasema katika utafiti huo pia waligundua kwamba maambukizi ya homa ya Ini aina C ilikuwa ni asilimia 83.

Dk Masano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Watoa huduma za Afya ya Akili Tanzania (Mehata) anasema ikiwa mtumiaji huyo hatapata kilevi huwa anakutwa na ‘Arosto’ ambayo ni hamu kali yenye kuambatana na maumivu makali kwenye mwili wake.

Anabainisha kuwa kila dawa ya kulevya huwa na ‘arosto’ya aina yake lakini mtu mwenye Arosto ya Heroin huanza kupiga miayo, kutoka kamasi, machozi, kuharisha, kukosa hamu ya kula, tumbo kuuma, hofu isiyo ya lazima, hapati usingizi, hatulii sehemu moja, anakosa amani na huwa na hamu ya kilevi hicho kupindukia.

Anasema kwa kawaida ikiwa mtu atakutwa na hali hiyo huwa analazimika kutafuta dawa. Na dawa pekee kwa wakati huo ni kilevi.

“Sasa wakati anapotaka kilevi hicho na hakipo kwa mwanamke sasa huwa inabidi hata ajiuze. Hapo ndipo wanaume hulazimika kufanya uhalifun kama kuiba mchana, kupora, kutapeli ili tu wapate fedha. Ili kuzipata lazima uwe na fedha ya kutosha,”anasema.

Anasema kwa mtumiaji huwa anatumia muda mwingi kutafuta fedha kwa ajili ya dawa za kulevya na sio kufanya kazi za maendeleo.

Anataja maradhi yanayowasumbua zaidi kuwa ni ya ngozi, vidonda hasa kwenye maeneo wanayojidunga, majipu na mwisho wa siku hupoteza viungo vya na wengine hufariki dunia ikiwa hawatapata matibabu.

Pia huwa hawana muda wa kula kwa sababu fedha wanayoipata huwa wanaitumia kununua dawa za kulevya, na hiyo ndiyo sababu inayowafanya watumiaji wa dawa za kulevya kudhoofika miili yao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Mhagama anasema njia pekee ya kuwalinda watoto wa kike kutojiingiza kwenye madawa hayo ni malezi yenye maadili.

“Tuwaepushe watoto wetu kwa kuwalea vyema. Kama mzazi mlevi jua mwanao atajiingiza huko sasa kama tunaipenda jamii yetu, tuwalee ipasavyo,”anasema.

Anashauri elimu kuendelea kutolea huku akisisitiza Serikali na wadau wengine kuendeleza vita dhidi ya dawa za kulevya.