Atakayefanya mambo haya atabamba mwaka 2017

Muktasari:

Bila shaka mwaka huu haujabadilisha malengo ya wasanii na kiu ya mashabiki; bado wasanii watakuwa wamepania kufanya makubwa zaidi na kubamba kuzidi ilivyokuwa mwaka jana.

Mwaka 2016 ulikuwa bab kubwa kwa upande wa burudani huku muziki hasa wa Bongo Fleva ukionekana kutawala tasnia ya muziki.

Bila shaka mwaka huu haujabadilisha malengo ya wasanii na kiu ya mashabiki; bado wasanii watakuwa wamepania kufanya makubwa zaidi na kubamba kuzidi ilivyokuwa mwaka jana.

Ili kufanikisha hilo, wasanii wa Bongo Fleva ni lazima wazingatie mambo manne muhimu.

Kolabo nje Afrika

Masikio ya mashabiki yameshasikia ngoma nyingi ambazo wasanii wetu wamefanya na wenzao kutoka nje ya Tanzania lakini ndani ya Afrika; kwa mwaka 2016 pekee tumeisikia sauti ya wasanii kama Chidnma, P Square na Spicy kutoka Nigeria; Mafikizolo, Dj Maphorisa na A.K.A kutoka Afrika Kusini na wengine wengi.

Kwa mwaka huu 2017, kolabo na wasanii wa Afrika hazitawashtua sana mashabiki kwa sababu imekuwa ni jambo la kawaida, hivyo inabidi wasanii wajipange kwa ajili ya kolabo za nje ya Afrika; kolabo za wasanii hasa wa Marekani walio kwenye chati itakuwa ni bora zaidi.

Kuishi midomoni mwa watu

Watakaofanikiwa kuwa mada katika mitandao ya kijamii na katika mazungumzo ya kawaida ya mashabiki watabamba zaidi kwa mwaka huu 2017, hivyo ni lazima wasanii wanaofikiria kutamba wajipange katika hili.

Vitu kama skendo za hapa na pale, bifu za mlengo chanya ni miongoni mwa njia ambazo msanii anaweza kuzitumia kuishi vinywani mwa mashabiki. Pia, kuwa na mawasiliano na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, matumizi bora ya mitandao ya kijamii yatamfanya msanii kuwa karibu na mashabiki hivyo kuwapa kila sababu ya kumzungumzia na kufanya aendelee kubamba.

Ubunifu wa ‘mbingu ya saba’

Haina shaka kabisa kwamba umakini wa mashabiki unaweza kuhamia kwa wasanii watakouthubutu kuja na ubunifu wa hali ya juu; ubunifu ambao utapelekea masikio ya kila shabiki yasikie kitu cha tofauti chenye kuashiria maendeleo.

Hii ni sawa na kusema kwamba wasanii watakaopata nguvu watakuwa ni wale watakaoachia ngoma zenye mashairi yalioyoandikwa tofauti na ilivyozoeleka, ngoma zenye melodi za tofauti, midundo tofauti, video za aina tofauti na siyo utofauti tu, bali tofauti yenye ubunifu mkubwa zaidi.

Kukuza ‘brand’ na kuiwekea msimamo

Kwa mwaka 2016 wasanii wengi waliboronga katika hili; wengi hawakuwa wakifahamu thamani yao halisi. Hawakuwa wakifahamu kwamba msanii ni ofisi inayotembea na kwamba kila ofisi inahitaji kutunzwa na kulinda hadhi yake.

Vitu kama kufanya shoo za ovyo ovyo zenye malipo kiduchu yasiyoendana na hadhi, msanii kuishi maisha ya kawaida, kuonekana kila mahali bila mpangilio maalumu, kutojijengea mwonekano wa kisanii viliwaangusha wengi.

Sasa kama msanii atataka kupata nguvu ya kisanii mwaka 2017 ni lazima ajue namna ya kukuza ‘brand’ yake na aiwekee misimamo. Kwa mfano, kama anaamua kuwa malipo yake kwa ajili ya shoo ni kiasi fulani basi asimamie hilo siyo kulegalega na kukubali kuendeshwa na mteja asiyethamini kazi ngumu anayoifanya msanii.