MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Athari ya Mwalimu Nyerere na Karume katika Kiswahili

Muktasari:

  • Hii inatokana na misimamo, sera, sheria na miongozo mbalimbali wanayoiweka. Ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania tunaoushuhudia leo hii ni matokeo ya jitihada za viongozi waasisi wa Taifa hili.

Viongozi mbalimbali hususan wa kisiasa, wana mchango mkubwa katika kustawi au kuporomoka kwa utamaduni wa jamii.

Hii inatokana na misimamo, sera, sheria na miongozo mbalimbali wanayoiweka. Ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania tunaoushuhudia leo hii ni matokeo ya jitihada za viongozi waasisi wa Taifa hili.

Tukiwa katika mwezi wa kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, miongoni mwa mengi aliyoyafanya, suala la kuweka misingi imara ya Kiswahili kamwe halitasahaulika. Pamoja naye ni kiongozi mwasisi-mwenza Sheikh Abeid Amani Karume.

Ikumbukwe kwamba nchi nyingi za Kiafrika ambazo zilitawaliwa na wageni, ziliathirika vikubwa kiutamaduni hususan katika kipengele cha lugha.

Aidha, urithi ulioachwa na wakoloni pamoja na wageni hao umekuwa kama kilevi ambacho athari yake huonekana hata leo hii.

Mathalani, zipo baadhi ya nchi ambazo wageni hao wameacha lugha zao zikitumika na wenyeji walioachiwa lugha hizo, huzionea fahari na kuzikumbatia hata kubeza jitihada zifanywazo kuzienzi lugha za Kiafrika.

Historia ya Tanzania kwa upande wa lugha ni tofauti kidogo. Hii ni kwa sababu ya misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume, kama viongozi Tanzania.

Kiswahili ndiyo lugha iliyotumika kuyaunganisha makabila zaidi ya 120 katika harakati za kudai uhuru. Hata hivyo, Kiswahili kiliendelea kuenziwa na waasisi hao kwa kukipa nafasi muhimu kitaifa baada ya uhuru.

Nchini Uganda kwa mfano, Kiswahili kilijengewa dhana tofauti hivyo kutopewa kiapaumbele. Kiingereza kinakumbatiwa na kuchukuliwa kama lugha azizi mpaka leo hii.

Aidha, baadhi ya nchi za Kiafrika lugha zake za taifa ni zile zilizoachwa na wakoloni.

Tanzania hurejelewa kama kitovu cha Kiswahili duniani kwa sababu ya misingi iliyowekwa na Nyerere na Karume.

Viongozi hawa walifanya hivyo wakizingatia kwamba nchi haina budi kuwa na utamaduni wake yenyewe. Utamaduni unahusisha mambo mbalimbali, moja kati ya hayo ni lugha. Nyerere na Karume kwa kulitambua hilo, waliweka mkazo na uzito mkubwa katika utamaduni.

Yapo mambo mengi yaliyofanywa na waasisi hawa na hata kuifanya lugha ya Kiswahili leo hii iwe na sura iliyonayo.

Miongoni mwa hayo ni: Mwalimu Nyerere kuanzisha sera ya lugha ambayo haikuwa katika maandishi iliyotoa dira kwamba; ‘Kiswahili ni lugha ya Taifa na mojawapo ya lugha rasmi za Tanzania, na Kiingereza ni lugha kuu ya kigeni na lugha rasmi ya pili Tanzania.

Profesa Mugyabuso Mulokozi anatanabahisha kuwa, sera hii ilitekelezwa kwa vitendo na hatua kadhaa zilichukuliwa kutokana nayo.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kukitangaza Kiswahili kuwa lugha ya Taifa (1962); kuanzishwa kwa Wizara ya Utamaduni (1962); TUKI (1964); Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (1964); Bakita (1967); Kiswahili lugha ya kufundishia shule ya msingi (1968); Elimu ya Msingi kwa Wote (1972); Elimu ya Watu Wazima (1972-1985) na hatua nyingine nyingi.

Profesa Mulokozi anasema; “Matokeo ya sera hizi ni ukuaji wa lugha yenyewe ya Kiswahili kutokana na matumizi mapya na mapana zaidi. Kwa mfano, maneno mapya ya siasa na utawala kama vile kata, tarafa, ujamaa... yaliibuka.”

Aidha, anaongeza kuwa, maneno kama sayansi na teknolojia, elimu, uchumi na mengineyo yaliibuka na kupanuka kimatumizi.

Viongozi waige mfano wa Nyerere na Karume katika kukiendeleza Kiswahili kutokana na nafasi zao. Nasi raia tuzienzi jitihada za waasisi hawa kwa kukitendea haki Kiswahili.