ELIMU NA MALEZI : Athari ya ufundishaji wa kukaririsha wanafunzi

Muktasari:

Mwalimu alirudia maneno hayo hayo kuweka msisitizo, kisha akatafsiri kwa Kiswahili. Alisema, ‘maana yake kuna kitu kidogo kisichoonekana kwa macho kwenye miili yetu kinachofanya tuishi. Mmeelewa?’ Kwa kweli hatukuwa na namna nyingine zaidi ya ‘kuelewa’ na tukaitikia, ‘ndiyo!’

Nakumbuka siku ya kwanza kusikia neno ‘cell’ nikiwa kidato cha kwanza haikuwa kazi rahisi kupata picha kamili. Mwalimu wetu aliandika ubaoni, ‘cell is a basic unit of life.’ Niliduwaa. Sikujua anamaanisha nini zaidi ya kutazama kamusi kujua maana ya maneno aliyoyatumia.

Mwalimu alirudia maneno hayo hayo kuweka msisitizo, kisha akatafsiri kwa Kiswahili. Alisema, ‘maana yake kuna kitu kidogo kisichoonekana kwa macho kwenye miili yetu kinachofanya tuishi. Mmeelewa?’ Kwa kweli hatukuwa na namna nyingine zaidi ya ‘kuelewa’ na tukaitikia, ‘ndiyo!’

Mwalimu alifurahi na akatupa muda tunakili sentensi hiyo kwenye madaftari yetu. Tulifanya hivyo ingawa ni wazi hatukuwa tukielewa anazungumzia nini.

Kazi iliyofuata ilikuwa ni kukariri sentensi hiyo bila kuelewa ina maana gani. Tulifikiri kukumbuka ndio kuelewa.

Mtihani ulipokuja tulijibu vile vile bila kukosea na mwalimu alitupa alama za juu kwa kurudia kile kile alichokuwa ametukaririsha. Lakini ukweli ni kwamba hatukuwa tumeelewa ‘tulichomeza.’

Changamoto ya ufundishaji

Huu ni mfano wa namna ufundishaji unavyochangia kwa kiasi kikubwa kufanya maarifa yanayokusudiwa na mtalaa yakose maana kwenye maisha halisi ya wanafunzi. Tunasoma vitu vingi tusivyoviona kwenye maisha yetu ya kila siku. Matokeo yake tunaishia kukumbuka na kufaulu mitihani kwa kiwango cha juu lakini thamani yetu kimaarifa ikibaki vile vile.

Tunamaliza shule lakini hatujui tunawezaje kutumia maarifa hayo kubadilisha maisha yetu kwa sababu ukweli ni kwamba, hatuoni uhusiano wa wazi kati ya kile tulichojifunza shuleni na maisha ya kila siku. Ikiwa tunataka kubadili hali ya mambo, mahali pa kuanzia ni kuwekeza kwenye maandalizi madhubuti ya walimu. Kama nilivyoeleza kwenye makala yaliyopita, mwalimu ndiye anayebeba dhima ya elimu. Bila mwalimu aliyeandaliwa vema, hatuwezi kuona matunda ya sera nzuri za elimu, mitalaa mizuri, madarasa bora na hata vifaa bora vya ujifunzaji na ufundishaji. Mwalimu aliyeandaliwa vema na kufuzu kazi ya kutafsiri mtalaa katika maisha ya mwanafunzi, anaweza kuibua na kuchochea udadisi kwa mwanafunzi wake.

Jitihada za wadau

Katika makala yaliyopita, tulitumia mfano wa mradi wa Next Generation Leaning (NGL) unaotekelezwa na Shirika la Opportunity Education Foundation kujifunza namna mwalimu anavyoweza kuifanya kazi yake kwa ufanisi.

Tuliona kanuni mbili. Kwanza, anahitaji kumfanya mwanafunzi aone namna gani kile anachofundishwa darasani kinagusa maisha yake ya kawaida. Kujua uhusiano uliopo kati ya maudhui anayojifunza na maisha yake, kunamfanya athamini maudhui husika na hivyo kuwa na ari ya kujifunza.

Pili, mwalimu anahitaji kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu maudhui anayojifunza. Kanuni hii inamsaidia mwanafunzi kupunguza utegemezi kwa mwalimu na hivyo kujenga ari ya kujiamini kuwa anaweza kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji.

Kukuza ujuzi

Kanuni ya tatu ni kumtarajia mwanafunzi kutumia maarifa yake kujitengenezea ujuzi. Mwanafunzi wa NGL si tu anahitajika kujibu maswali ya kufikirisha, bali kuonyesha ujuzi mahususi. Mathalani, baada ya mwanafunzi kujifunza namna mimea inavyotengeneza sukari kwa kutumia mwanga wa jua, lazima aonyeshe anavyoweza kutumia maarifa hayo kutatua changamoto anazokabiliana nazo katika mazingira yake.

Hali halisi katika shule zetu ni tofauti. Mwalimu humtarajia mwanafunzi kukusanya na kukariri maarifa. Kipimo cha ujifunzaji ni kwa kiwango gani mwanafunzi huyu anajua kutoa maelezo sahihi ya nadharia za kitaaluma.

Mwanafunzi anayesoma mada ya Uchafuzi wa Mazingira, kwa mfano, anatarajiwa kukusanya, kukariri na kuelewa maelezo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira. Mwanafunzi huyu mwenye taarifa nyingi kuhusu uchafuzi wa mazingira bado anaweza kuvumilia kuishi na takataka zilizo karibu na makazi yake bila wasiwasi. Kwa mtindo huu, uelewa wa uchafuzi wa mazingira haujaweza kumsaidia kuona tatizo na kulitatua. Kwa mwanafunzi huyu uchafuzi wa mazingira ni ‘mambo ya shule’ yasiyohusiana na maisha yake halisi ambayo hata hivyo yanaweza kumsaidia kufaulu mitihani yake vizuri.

Katika zama hizi za ukuaji wa mawasiliano, maarifa ya kila namna yanaweza kupatikana. Mtu yeyote mwenye ujuzi wa namna ya kutumia mtandao wa intaneti anaweza kutafuta na kupata chochote anachotaka kujifunza.

Kuendelea kusisitiza kwenye kumbukumbu ya maarifa kimsingi si kumtendea haki mwanafunzi. Maarifa hayapaswi kuwa lengo la elimu. Tunahitaji kuongeza thamani kwa kwenda mbele ya maarifa.

Badala ya mwalimu kumjazia mwanafunzi maelezo mengi, anahitaji kulenga katika kukuza uwezo wake kwa kutumia maarifa anayoyapata katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazomkabili.

Uwezo huu unaitwa ujuzi. Mtu mwenye ujuzi anaweza kufanya vitu vinavyoonekana kama ushahidi kuwa amejifunza maudhui fulani.

Kwa mfano, katika kufundisha mada ya uchafuzi wa mazingira, mwalimu asiishie kumjaza mwanafunzi nadharia na maelezo mengi yanayohusiana na uchafuzi.

Badala yake, aende hatua moja mbele kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuona matatizo yanayofanana na kile anachojifunza na kujaribu kutafuta majibu yanayolingana na kiwango chake cha uelewa. Huko ndiko kutumia maarifa kujipatia ujuzi, kanuni muhimu ya mradi wa NGL.

Mwalimu wa NGL, kwa mfano, mbali na kuhakikisha mwanafunzi anahusianisha kile anachojifunza na maisha yake, anatarajiwa kukuza ujuzi wa mwanafunzi kwa kufundisha katika namna inayochochea utafutaji wa majibu.

Ufanisi wa somo unapimwa kwa namna mwanafunzi anavyoweza kutazama nje ya darasa na kubaini matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa kutumia maarifa aliyonayo.

Mwanafunzi ashirikiane na wenzake

Tunafahamu wanafunzi hutofautiana uwezo. Wapo wenye uelewa mkubwa wa mambo kuliko wengine. Kadhalika, kila mwanafunzi ana namna yake bora zaidi ya kujifunza. Wapo kwa mfano, wanaojifunza kwa kusikia, wengine kwa kutazama, wengine kwa kufanya. Kwa kuzingatia ukweli huo, mradi wa NGL unayo kanuni ya nne inayomtaka mwalimu kumwezesha mwanafunzi kujifunza akishirikiana na wenzake.

Kupitia majadiliano, mwanafunzi anapata nafasi ya kusikiliza uzoefu na uelewa wa wenzake ambao unaweza kuwa tofauti na wa kwake.

Pia, kwa kuwa majadiliano haya yanafanyika katika mazungumzo ya kawaida na marafiki, mwanafunzi anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufurahia kile anachokisoma.Ingawa walimu wetu wamekuwa wakifundishwa mbinu hii ya kuwashirikisha wanafunzi katika ujifunzaji, mara nyingi utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi.

ITAENDELEA