BAADA YA BAO Tino: Joel Bendera alinibeba mgongoni Zambia

Muktasari:

Bendera alifariki Alhamisi iliyopita akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa nne tu tangu alipopokewa akitokea mjini Bagamoyo.

Kocha Joel Bendera ametangulia na jana Jumapili alipumzishwa katika nyumba yake ya milele wilayani Korogwe, lakini ameondoka na historia yake tamu ambayo nyota wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino anasema kama sio Bendera, Taanzania isingecheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1980.

Bendera alifariki Alhamisi iliyopita akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa nne tu tangu alipopokewa akitokea mjini Bagamoyo.

Mchezaji wa zamani wa Pan African, Peter Tino hatasauliwa kutokana na kufunga bao lililoiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini mshambuliaji huyo anasema wa kukumbukwa zaidi ni Bendera.

“Asikwambie mtu, wachezaji tulifuraji lakini bendera alifurahi zaidi tulipofunga bao la kusawazisha kwenye mechi na Zambia tena mbele ya rais wao, Kenneth Kaunda kwenye uwanja wa Ndola,” Tino anasimulia alipofuatwa na Spoti Mikiki.

“Baada ya filimbi ya mwisho, Bendera alinikimbilia na kunibeba mgongoni. Ilikuwa ni furaha ya Watanzania wachache waliokuwa pale uwanjani.”

Anasema ushindi haukuanzia uwanjani, bali maneno ya Bendera walipopokelewa ubalozini.

“Tulipofika Lusaka, timu yetu ilikwenda kumtembelea balozi kabla ya kwenda Ndola. Tukiwa pale (ubalozini) tulionyeshwa magazeti ya Zambia, rais wao akiwa ameshika funguo za gari na kutamka kwamba kila mchezaji atapewa gari na nyumba kama wataifunga Tanzania,” anasema.

“Yale maneno yalimuumiza mno Bendera. Alituambia, ninyi hamjaahidiwa chochote, lakini ninyi ndiyo mnatakiwa mtoe zawadi kwa Watanzania. Msitumike kama mgongo wa watu kupewa nyumba na gari. Bendera alizungumza kwa ujasiri mno na maneno yake yalitusisimua na tuliwaahidi kufia uwanjani.

“Kwenye mechi ilikuwa hakuna bahati mbaya. Hadi mapumziko tulikuwa tumeshafungwa bao 1-0. Tukiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kocha mzungu alizungumza akamaliza, ikafika zamu ya Bendera sasa, alizungumza kwa hisia akasema maneno yangu ni yale yale.

“Tusikubali watu wapewe nyumba na gari kwa mgongo wetu, Serikali haijatoa ahadi yoyote kwetu, lakini sisi tutoe ahadi kwa Watanzainia, wao wanaongoza na bila shaka sasa hawana nguvu hivyo sisi twendeni tukawafunge, Bendera alipomaliza kutamka hivyo, mimi niliitikia sawaa tena kwa sauti ya juu,” anasimulia Peter Tino. “Wakati tunacheza, pale Uwanjani kulikuwa na Watanzania kama 30 hivi au 40 ambao walikuwa wakitushangilia mwanzo mwisho kwani kitendo cha kufungwa bao moja hadi mapumziko wao waliona cha kishujaa kwetu kwani walijua tutapigwa nne au tano hadi mapumziko.

“Baada ya bao letu mpira ukaisha kwa sare ya bao 1-1, Bendera alikuja spidi hata sikumbuki alinibebaje mgongoni. Nilijikuta niko tayari mgongo kwake huku akiimba ndoto yangu imetimiaaa! Ilikuwa ni furaha isiyopimika kwani matokeo yale yalitupeleka AFCON kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya kuibika na ushindi wa bao 1-0,” anasema.

Jinsi bao lililovyofungwa

Tino alifunga bao hilo wakati Stars iliporudiana na Zambia jijini Ndola Agosti 26,1979 wakati huo wenyeji wakijulikana kwa jina la KK Eleven, kumaanisha rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda.

Iko hivi, Taifa Stars wakati huo ikiwa chini ya Kocha, Slowmir Wolk kutoka Poland, akisaidiwa na Bendera na Ray Gama ambaye naye ni marehemu, ilikata tiketi ya kushiriki Fainali hizo za Afrika.

Katika pambano hilo la agosti 26, 1979, Taifa Stars ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili ifuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1968.

Timu hizo zilikuwa zinarudiana baada ya Stars kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika wiki mbili zilizotangulia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), bao pekee likiwa limefungwa na kiungo, Mohammed Rishard Adolph.

Katika mchezo huo wa marudiano, KK walipata bao la mapema katika mchezo huo ambalo lilidumu hadi dakika ya 85.

Dakika tano za mwisho, Peter Tino alisawazisha bao na kunyamazisha umati wa mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Ndola.

Ilipigwa kona kuelekea lango la Stars na kipa Juma Pondamali “Mensar” akaupangua kwa ngumi, ukamkuta beki wa kati, Leodegar Chilla Tenga ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Hussein Ngulungu. Kiungo huyo akamgongea Tino.

Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino aliwazidi ujanja akiwa nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia na kupiga kombora la mguu wa kulia, lililompita kipa wa Zambia aliyekuwa kikwazo, John Shileshi.

Katika mchezo huo, Tanzania iliwakilishwa na; Juma Pondamali ‘Mensar’, Leopard Tasso Mukebezi, Mohammed Kajole Machela/ Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Chilla Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein ‘Keegan’, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.

Nahodha Leodegar Tenga

Leodegar Tenga, aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka 10, aliiongoza timu hiyo uwanjani na kufanya vizuri hata kufika fainali hizo.

Akimzungumza na Spoti Mikiki Hospitali ya Lugalo wakati wa kuuaga mwili wa Bendera, Tenga anasema: “Mwalimu Bendera alikuwa na uwezo mzuri wa kuongea na wachezaji kabla na hata wakati wa mchezo.

“Tulikuwa tukijisikia furaha tukiwa naye. Kila mmoja wetu alijiona ni mwana familia, hakika hili ni pigo kwenye familia ya mpira na daima atabaki kukumbukwa kama mtu mbaye amelifanyia Taifa makubwa.”

Hata hivyo, Tenga anasema kuwa mafanikio yao hayakuja kirahisi kwani waliandaliwa kwa miaka minne kuanzia mwaka 1976.

Kiraka Adolf Rishard

Jina la timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars lilizinduliwa katika mchezo ambao Tanzania iliongozwa na Bendera, kwa mujibu wa Adolf Rishard, mchezaji mwingine aliyewahi kuwa chini ya mkufunzi huyo.

Rishard, ambaye pia alifunga bao katika mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Zambia nyumbani, anasema Bendera alikuwa ni kocha mwenye maono.

“Mimi niliitwa Stars 1976 kwenye mechi na Kenya kwa ajili ya kuzindua jina la Harambee Stars. Alikuwa pamoja na marehemu Gama mwaka 1977 hatukucheza Chalenji kutokana na vita ya Uganda, lakini mwaka 1978 tulikwenda kuweka kambi Lushoto kwa ajili ya Chalenji na 1979 tulikuwa wa tatu kwenye Chalenji Nairobi .

“Wakati huo ndio tulikuwa katika harakati za kufuzu tukiwa naye hadi 1980 kwenye AFCON. Lakini baada ya AFCON aliondoka na kocha wa Stars akawa Msomari, japo sikumbuki Bendera aliondokaje ondokaje Stars wakati ule,” anasema Rishard.

“Ninamkumbuka Bendera alikuwa na kipawa cha hamasa, alitupa hamasa sana kiasi cha kufanya vizuri mechi zetu.”

SAFARI YA KOROGWE

Bendera alifariki Desemba 6 jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Brass Kiondo ndugu yao alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kupumua ambalo lilimuanza Desemba 3 na alikuwa anatibiwa Hospitali ya Korogwe na baada ya hali yake kuimarika, akapelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi lakini hali ilibadilika ghafla hadi mauti yalipomkuta akiwa Muhimbili.

Bendera aliagwa juzi jijini Dar es Salaam na ndugu, jamaa na marafiki na wanamichezo, hasa wachezaji aliowafundisha akiwemo Tenga na Tino.

Watu wengine waliohudhuria ni pamoja na mkurugenzi wa ufundi wa TFF ambaye pia ni kocha, Salum Madadi na mtangazaji mkongwe, Tido Muhando.

Wengine ni mbunge wa Muheza, Adadi Rajab.

Bendera aliwahi kuwa mbunge wa Korogwe Mjini, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkuu wa mikoa ya Morogoro na Manyara.

Katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli Oktoba 26, Bendera alikuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa waliostaafu na nafasi yake imechukuliwa na Alexander Mnyeti aliyepandishwa kutoka kuwa mkuu wa Wilaya ya Arumeru.

Mapema baada ya kushindwa ubunge, aliteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro.