BURIANI KAMANDA NDESAMBURO

Marehemu Mzee Philemon Ndesamburo wakati wa uhai wake 

Muktasari:

Wa kwanza ni ule wa Mzee Mohamed Nyanga Makani alimaarufu Bob Makani mwaka 2012 ambaye alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa Chadema na baadaye mwenyekiti wa chama na hivi majuzi tu Mzee Philemon Ndesamburo kwa lakabu (a.k.a) Ndesapesa.

Tangu nilipojiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo mwaka 2011 nimeshuhudia misiba miwili mikubwa ya waasisi wa Chadema.

Wa kwanza ni ule wa Mzee Mohamed Nyanga Makani alimaarufu Bob Makani mwaka 2012 ambaye alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa Chadema na baadaye mwenyekiti wa chama na hivi majuzi tu Mzee Philemon Ndesamburo kwa lakabu (a.k.a) Ndesapesa.

Wakati Bob Makani anafariki dunia nilikuwa nimetingwa sana na kuendesha kesi ya uchaguzi kati ya Joseph Mwandu Kashindye wa Chadema dhidi ya Dk Kafumu Dalali mbele ya Jaji Mary Shangali katika Mahakama Kuu pale Nzega mkoani Tabora kwa hiyo nilishindwa kumuandikia tanzia licha ya kutamani mno kufanya hivyo. Nikaambulia kumzika tu pale Kishapu mkoani Shinyanga.

Nilisikitika mno kushindwa kumuandikia tanzia kwa vile nilikuwa karibu naye sana kitaaluma, kabila na misimamo na mitazamo yetu ya siasa za upinzani. Na yeye ndiye alikuwa na mchango mkubwa mno hatimaye kunishawishi nijiunge na Chadema.

Safari hii nimepata wasaa wa kushiriki kikamilifu katika mazishi na kuandika tanzia ya mzee wetu Kamanda Ndesapesa aliyefariki ghafla kazini kwake Moshi Mei 31.

Lakini nachelea kurejea mazuri mengi yaliyosemwa kuhusu kiongozi huyu shupavu wa Chadema hususan siku ya kumuaga rasmi katika uwanja wa Manispaaa ya Moshi pale Majengo Juni 5.

Wasemaji hao ni pamoja na muasisi mkuu wa Chadema, Edwin Mtei, Mwenyekiti Freeman Mbowe, mbunge wa Moshi Mjini, Jaffari Michael, Meya wa Moshi na rafiki yake wa takribani miaka 60, mzee Manase.

Wote walieleza mchango wake mkubwa kwa Chadema na wananchi wa Moshi ambao aliwatumikia kama mbunge wao kwa miaka 15 mfululizo.

Na siku hiyo jioni pale nyumbani kwa mzee Ndesapesa, Tundu Lissu alisawiri vyema mchango wake bungeni na kuwataka vijana waige mfano wake.

Kwa hiyo, basi nijikite kuelezea mambo adimu niliyojifunza kutoka kwa mzee wetu mara chache tulipokutana na yaliyojiri wakati wa mazishi yake.

Nilikutana na mzee Ndesamburo mara ya kwanza siku chache tu baada ya kujiunga Chadema pale Makao Makuu, Mtaa wa Ufipa Dar es Salaam. (Sehemu ileile ambapo paliwekwa kitabu cha maombolezo ya kifo chake).

Kwa ucheshi alinitakia mema katika Chadema na kuniomba niende Moshi kusaidia kuendesha kesi za kisiasa zilizokuwapo wakati ule. Lakini namkumbuka zaidi kwa kauli yake aliyoitoa katika Retreat, Hoteli ya Protea pale Aishi Machame Moshi mwaka 2014.

Ndesamburo alisema kuwa yuko tayari kutumia utajiri wake wote, ikibidi hata kuuza kuku wake wa mwisho kuleta ukombozi wa wanyonge wa Tanzania.

Kauli hiyo ikanikumbusha ya msomi maarufu wa siasa Karl Max aliyesema mapambano dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji duniani yataongozwa na wasomi na wenye mali ambao watajitoa muhanga ili kutimiza azma hiyo.

Sababu wao wanaongozwa si na tamaa ya kipato, bali uchungu wa kuwakomboa kapuku wasaka tonge. Na Waislamu wanajua vyema kuwa akhera wasomi wataulizwa na Mwenyenzi Mungu kuwa elimu yao waliitumiaje na matajiri nao wataulizwa mali yao waliitumiaje duniani.

Naamini Kamanda Ndesapesa alitumia vipawa vyake vyote viwili kwa uadilifu mkubwa kwa manufaa ya wanyonge wa Tanzania hususan Moshi.

Msiba ulivyopaswa kufanyika

Sasa nigeukie matukio muhimu yaliyojiri katika msiba wa mzee Ndesapesa ambayo yanahitaji tafakuri.

Mengine yameshaelezwa kama vile jeuri ya viongozi wa Serikali ya CCM kukataa mwili wa Mzee Ndesapesa kuagwa katika Uwanja mashuhuri wa Mashujaa. Au uwakilishi dhaifu wa CCM katika msiba huo kama ambavyo Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alivyoelezea vizuri sana.

Basi nianzie na msafara kutoka hospitali ya KCMC kuchukua mwili wa marehemu Ndesapesa saa nne asubuhi tarehe 5 Juni 2017 kuelekea Uwanja wa Majengo kwenda kuagwa. Njia nzima zaidi ya kilomita tano ilizingirwa na watu wengi wa rika mbalimbali waliosimama kwa huzuni kumuaga. Wako walioonyesha vidole viwili alama mashuhuri ya Chadema na wengine walisimama tu wameduwaa. Wengine walitembea kwa kwa mguu hadi uwanjani Majengo.

Lakini polisi walikera kwa kutokea mara kwa mara huku wakiwa na silaha za kivita kama vile bunduki za AK 47 na SMG kana kwamba ulikuwa msafara wa shari.

Pale uwanjani Majengo maandalizi ya kumuaga marehemu Ndesapesa yalikuwa mazuri. Uwanja ulikuwa mkubwa. Kulijengwa jukwaa kubwa zuri kwa ajili ya viongozi wakuu wa Chadema na Serikali pamoja na wa kiroho.

Pia kulikuwa na mahema makubwa zaidi ya ishirini kuwahifadhi waombolezaji na jua au mvua. Ukiachia vitimbwi vya polisi, kulikuwa na utulivu mkubwa mno. Kulipigwa mwimbo wa kumuaga Hayati Ndesapesa uliotungwa na msanii stadi wa Chadema, Kotide.

Wimbo huo ulifanya baadhi ya waombolezaji kuangua vilio kimya kimya na wengine kwa sauti kuu. Daima nimekariri kuwa siasa na sanaa hususan nyimbo ni sawa na mkono wa kulia na kushoto.

Kwa mfano Tanu na Mzee Mwinamila au CCM na Kapteni Komba. Napendekeza Chadema izingatie jambo hili. Kotide na wenzake waenziwe na kupewa fursa.

Nimemwelekeza Katibu wa Kanda ya Magharibi ya Chadema, Generali Kaduma afanye hivyo kwa kuutumia ustadi mkubwa wa Kamanda Elisha na wenzake katika uimbaji kama nilivyoshuhudia katika ziara zangu kule Sikonge, Tabora.

Viongozi wa kiroho walitoa mahubiri na mawaidha maridhawa. Kulikuwa na Sheikh Mwakilishi wa Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) Moshi, Sheikh Rajabu Katimba wa Jumuiya ya Waislam Tanzania na Askofu Josephat Gwajima.

Viongozi wote wakuu wa Chadema walikuwepo yaani muasisi wa chama mzee Mtei, Mwenyekiti Mbowe na Makamu wake Profesa Abdallah Saffari (Bara) na Issa Mohamed (Zanzibar).

Pia alikuwepo Katibu Mkuu Dk Vincent Mashinji na manaibu wake, John Mnyika na Salim Mwalimu. Aidha alikuwapo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Arcado Ntagazwa, Mjumbe wa Kamati Kuu na mshauri Mkuu wa Siasa wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na wajumbe wengine wa Kamati Kuu.

Vilevile alikuwapo James Mbatia Sheikh (Mb) Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, mwakilishi wa CUF na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Siku ya maziko ya Mzee Ndesamburo tarehe 6 Juni 2017 kulijaa simanzi kubwa! Msafara uliondoka nyumbani kwake asubuhi saa nne kuelekea Kanisa la Kulutheri Kiboroloni takriban kilometa tatu kutoka nyumbani kwake. Umati ulikuwa mkubwa mno!

Ndani ya kanisa waliingia viongozi wote wa kitaifa wa Chadema, James Mbatia na Hashim Rungwe aliyewahi kugombea urais mara mbili kwa tiketi ya chama chake.

Baadaye alifika Kipi Warioba, mkuu wa Wilaya ya Moshi, mbunge wa zamani wa Rombo, Basili Mramba na Wiliam Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi. Kuvutio kikubwa kilikuwa hotuba madhubuti ya Askofu Shoo dhidi ya viongozi dharimu.

Alisema wataishia kuwadanganya wanadamu sio Mungu. Waombolezaji walipita mbele ya jeneza lililofunguliwa. Baadhi yao walianguka kwa uchungu baada ya kuona sura ya Ndesapesa, yote kudhihirisha upendo wao kwake kutokana na mengi mazuri aliyoyafanya. Hatimaye mhisani wao mkuu alikuwa amewatoka.

Baada ya sala ya kanisani safari ilianza tena hadi nyumbani kwa marehemu. Mzee Ndesapesa alizikwa katika bustani kubwa na nzuri nyumbani kwake. Niliketi hatua kama nne tu karibu na kaburi lake, mkabala kabisa na yule sahibu yake wa miaka mingi, Mzee Manase.

Wakati wote wa maziko huzuni ilitamalaki na kuzidi pale jeneza lake liliposhushwa kaburini kukamilisha safari yake ya duniani. Mtoto wa kwanza wa Mzee Ndesapesa na Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya alizimia na kumwangukia mumewe Dk Owenya.

Baadhi ya wajukuu waliangua kilio. Mmoja, msichana wa miaka takriban minane alibembelezwa na Mbunge wa Viti Maalum Kunti Yusufu akilia kwa kwikwi. Ilikuwa huzuni isiyomithilika.

Mwenyezi Mungu anasema, “Baadhi yenu mko hai wakati mmekufa na wengine mmekufa wakati mko hai.” Waja vema hawafi kutokana na matendo yao mazuri kwa wanadamu. Kwangu mimi mzee Ndesapesa anaungana na wapinzani na wanamageuzi madhubuti nchini kama vile hayati Joseph Kasella Buntu na Bob Makani.

Kazi kubwa ni kumuenzi Ndesapesa kwa matendo sio maneno matupu! Amenena Mwenyezi Mungu, “Sote ni waja wa Mungu na kwake tutarejea.” Chambilecho Wakristo, “Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.”

Buriani Kamanda Ndesamburo.

Profesa Abdallah Safari ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa (Bara)