Baada ya fitna za FDL, Ligi Kuu kuna haya

Muktasari:

  • Msimu ujao zitashuka timu mbili na kupanda sita ambazo zitatimiza timu ishiriki zitakazokuwepo katika ligi tofauti na msimu huu ambao una timu kumi na sita na kwa maana hiyo mechi za ligi zitaongezeka.

Kama ulikuwa haujui nakukumbusha tu mzunguko wa pili wa lala salama wa Ligi Daraja la Kwanza ulishanza kitambo na timu mbili za juu katika kila kundi zitapanda Ligi Kuu msimu ujao wa 2018-19.

Msimu ujao zitashuka timu mbili na kupanda sita ambazo zitatimiza timu ishiriki zitakazokuwepo katika ligi tofauti na msimu huu ambao una timu kumi na sita na kwa maana hiyo mechi za ligi zitaongezeka.

Wakati ligi ikiendelea, kumekuwa na fitna mbalimbali, ambazo ama zinatengenezwa au ni uamuzi wa mtu anaamua inakuwa hivyo kuhakikisha timu fulani inafika.

Spoti Mikiki linawakumbusha tu, viongozi, wachezaji, wapenzi na mashabiki ambao timu zao zitapata nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu, wakumbuke kuna mambo ambayo lazima watakutana nayo na wanatakiwa kukabiliana nayo hivyo wakipiga fitna wajue kujipanga.

Timu bora

Katika kila msimu, lazima kutakuwa na timu ambayo itakuwa bora kama msimu huu ni wazi kwamba Simba ndio timu bora kutokana na kikosi chao jinsi kilivyo licha ya kuwa na changamoto za hapa na pale ambazo klabu yoyote lazima ikubali kukutana nazo.

Hapa ndio nawakumbusha kuwa katika timu ambazo zitapata bahati ya kupanda Ligi Kuu wajue kuna mnyama.

Pia zinatakiwa kujipanga na kuwa timu bora kama ilivyo Singida United kwa sasa au Mbeya City ilivyopanda Ligi Kuu msimu wa 2013-14.

Pia kuna timu kama Yanga, Azam ambazo hazifanyi makosa kwa timu ndogondogo na wanaopanda wajipange wanaweza kupigwa mabao hata zaidi ya matatu hadi saba.

Kama wakishindwa kuwa miongoni mwa timu bora watakuja Ligi Kuu kama kushanga na kupita tu kwani watakuwa timu ya kugawa pointi na kurudi walipotoka yaani Ligi Daraja la Kwanza.

Vikosi vya thamani

Timu za Daraja la Kwanza zinaweza kuwa na vikosi vya Sh6milioni au hata Sh10milioni, huwezi kukuta timu ambayo inatoka Ligi Daraja la Kwanza kuwa na kikosi kilichokuwa na thamani kubwa.

Singida United imepanda ikichechemea, lakini wadhamini wamewabeba na kuleta ushindani haswa kwa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam.

Singida United wamejipanga vya kutosha na wana wadhamini ambao watasaidia kuendesha timu yao bila shaka.

Timu zitakazopanda Ligi Kuu lazima zikutane na vikosi vyenye thamani na wachezaji wenye majina makubwa kama Emmanuel Okwi, Obrey Chirwa, Aishi Manula, Ibrahim Ajib au Himid Mao.

Mchezaji mmoja mkali

Ukiangalia katika timu zote zilizokuwa katika Ligi Kuu ambazo zinafanya vizuri lazima zitakuwa na mchezaji mmoja au zaidi ambao ndio unaweza kusema nyota wa timu kwani anatoa mchango mkubwa wa kuisaidia timu.

Wapo wengi lakini kwa ufupi Yanga kuna Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa, Simba Shiza Kichuya na Okwi, Azam Mbaraka Yusuf na Himid Mao, Tanzania Prison kuna Mohammed Rashid na Mbeya City kuna Eliud Ambokile.

Hao ni baadhi ya wachezaji ambao wanafanya vizuri katika timu zao sasa nawakumbusha tu kuwa kama timu za Daraja la Kwanza zinakuja huku tayari zije zimeshajiandaa kisaikolojia kuwa zinatakiwa kuja kupambana na wachezaji wakali na tayari wako juu katika anga za soka hasa Ligi Kuu Bara.

Gharama za usafiri

Timu za Daraja la Kwanza zinapanda kwa mbwembwe lakini ligi ikichanganya si jambo la kushangaza kusikia wamekwama katika sekta ya uchumu.

Matatizo hayo ya kiuchumi yanaweza kuwa kushindwa kulipa mishahara na posho wachezaji na kushindwa hata kusafirisha timu kutoka mkoa waliokuwepo kwenda mkoa mwingine na tumeshasikia baadhi ya timu msimu uliopita kukwama katika usafiri.

Nawakumbusha tu, zinatakiwa kujipanga mapema kutafuta kusaka wafadhili kama vipi kuwapa basi ili wawe na uhakika wa safari kama ilivyo kwa Singida, Mbao, Mtibwa, Mbeya City, Yanga, Simba na klabu nyingine kuwa na gari la uhakika la kusafiria muda wowote kwenda mahala popote ambako mtakuwa mnacheza mechi ya ligi au FA.

Waamuzi

Si jambo la kushangaza katika Ligi Daraja la Kwanza kusikia mwamuzi kachezea kichapo kisa kachezesha vibaya au mwamuzi kuamuru maamuzi ambayo hayakuwa sahihi ili kufaidisha timu fulani kupata matokeo.

Jambo hili katika Ligi Kuu halifanyiki waziwazi kama ilivyo huko katika Daraja la Kwanza ila nachukua jukumu la kuwakumbusha haya mambo huku napo yapo pia ingawa si mara kwa mara ila manatakiwa kuchukua tahadhari na kijipanga.

Kuna penalti, kuna magoli ya offside, kuna wakati bao tamu lakini linakataliwa. Huku hakuna kuhamaki, unatuli tu kama mgonjwa anapopigwa sindano.

Zomeazomea

Simba, Yanga ndio klabu zenye mashabiki wengi kwa sasa hapa nchini na wala si jambo la kushangaza kuona mnacheza na timu hizo moja ya mchezaji wenu ambaye anacheza vizuri akawa anazomewa katika Uwanja wa Taifa, Uhuru na hata kiwanja chenu cha nyumbani.

Nawakumbusha huku kuna zomea zomea ya mashabiki ambayo watakumbana nayo

wachezaji na makocha na kama mkishindwa kuvumilia mnaweza kujikuta mnashindwa kuhimili na kurudi mlipotoka lakini vinginevyo timu itafanya vizuri kama Mbao, Singida na hata Azam walipopanda Ligi Kuu 2008.

Jamvi la wageni

Si kitu cha kushangaza kuona timu ilikuwa kinara Ligi Daraja la Kwanza na kucheza msimu mmoja tu Ligi Kuu na kurudi walipotoka na hii yote kutokana na kutojipanga katika maandalizi ya michuano hiyo.

Katika misimu kadhaa, tumewahi kuona timu zinapanda Ligi Kuu lakini zinashindwa kuleta ushindani na inakuwa timu ya kugawa tu pointi katika kila mechi na mwisho wa msimu kujikuta katika zile timu tatu ambazo zinashuka.

Timu itakayobahatika kupanda Ligi Kuu, inatakiwa kukaza buti na kama ikishindwa kufanya hivyo timu yenu itakuwa ya kugawa pointi tu na kuitwa jamvi la wageni.