Baada ya kutamba Bongo Fleva, ahamishia majeshi kanisani

Muktasari:

  • Hali hiyo ndiyo iliyomkuta mwimbaji wa muziki wa injili, Natasha Lisimo wakati alipokuwa akirekodi wimbo wa Shukrani.

Dar es Salaam. Umeshawahi kukutana na mtu akimshukuru Mungu huku akibubujikwa machozi kutokana na matendo makuu aliyomtendea?

Hali hiyo ndiyo iliyomkuta mwimbaji wa muziki wa injili, Natasha Lisimo wakati alipokuwa akirekodi wimbo wa Shukrani.

“Huwa siamini kama leo hii na mimi nipo hivi nilivyo, niliambiwa mengi, nilitukanwa na kudharauliwa lakini Mungu amenipa heshima. Hii ndiyo sababu ya shukrani zangu kwake,” anasema.

Kinachompa nguvu mwanadada huyo ni namna ambavyo hakati tamaa hata wakati anapokutana na mambo magumu.

“Ujue kukata tamaa ni adui mkubwa wa mafanikio ya mtu, hata wakati ninapopitia magumu huwa siamini kama nitashindwa, huwa napiga goti kumuomba Mungu,” anasema.

“Mimi ni mama wa watoto wawili, nimeokoka nampenda Yesu na nimeolewa.”

Akielezea historia yake, Natasha anasema aliamua kujifunza muziki katika Nyumba ya Vipaji maarufu THT ili awe kati ya waimbaji mahiri wenye uwezo wa kuitumia sauti vilivyo.

“Pale THT nilisoma kwa mwaka mmoja na nusu hivi kabla ya kuhitimu na ninashukuru Mungu nilinolewa na ninaweza kuimba vyovyote vile,” anasema.

Anasema wimbo wake wa kwanza uliomtambulisha ni ule uliokuwa unaitwa ‘Maumivu Niache’ huku akiutumia jina lake la Khadijanito.

Anasema alipata matamasha mengi na wakati akiendelea muziki aliamua kuolewa.

Natasha anasema mumewe alikuwa akimuunga mkono kwenye kazi zake nyingine za muziki za Si Ulisema, Sina Maringo na baadaye aliamua kuanza kuimba muziki wa injili.

“Unajua mume wangu siku zote anasikiliza muziki wa Injili kwa hiyo hata nikiimba nilikuwa naona akiwatumia watu nyimbo za Injili kwa hiyo nikaona ni vizuri nami niimbe hizo,” anasema.

Anasema 2016 alipata ujauzito wa mtoto wake wa pili na kwamba ni kipindi ambacho alipitia magumu ikiwamo kuugua kiasi cha kukaa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

Natasha anasema mapafu yake yalijaa maji na figo zilishindwa kufanya kazi huku akikaukiwa na damu.

“Baada ya kuombewa na kuinuka kitandani pale Muhimbili kulinifanya sasa niwe na maamuzi kabisa ya kumtumikia Mungu kwa hiyo nimeamua toka moyoni kabisa na kwa nguvu zangu zote na bila kujali familia yangu watasemaje,” anasema Natasha.

“Kwa wiki mbili nilitumia mashine na nilikuwa na hali mbaya mno, hata huu wimbo wa Shukrani nilipousikia niliona unanifaa sana, kuna kipindi watu walisema nilifulia ndio maana nikakimbilia wokovu.”

Anasema haogopi mawe ya wanaompiga kwa sababu ya kubadili imani akiamini ni njia yake ya kuingia kwenye mafanikio.

Mwanamuziki huyo wa injili anaeleza kuwa mpango wake siku za usoni ni kuendelea kumtumikia Mungu kwa nguvu zaidi katika muziki akiamini atafika mbali.

Juni mwaka huu anatarajia kuachia video yake ambayo inaitwa ‘Ufunguo’ aliyomshirikisha Bagagiste Bukuku.