Badili mtazamo wako kuhusu eneo lako la kazi

Muktasari:

Labda tuangalie mfano wa mwisho! Je umewahi kuona muuza duka amekaa nje akisoma gazeti au akiongea na jamaa zake na mteja anapofika anaanza kumuuliza “unataka nini” angali akiwa nje ya duka bado. Mara nyingine unakuta amekamatwa na maongezi matamu ambayo wenzake wasio na kazi wanaamua kuja kuyaongelea katika eneo lake la kazi, au yamkini sio maongezi bali ni mchezo fulani kama vile bao, karata, draft au pooltable na anaona shida kabisa kuacha mtiririko wa mchezo aende kumhudumia mteja.

Je, umewahi kuona wafanyakazi kuanza wikiendi mapema na kuchelewa kumaliza? Zamani ukisikia wikiendi ilimaanisha Jumamosi na Jumapili, siku zilipokwenda ikaanza kusheherekewa kuanzia Ijumaa jioni, taratibu sikuhizi inaanza kuhamia Alhamisi. Kibaya zaidi nipale cherekochereko za wikiendi hususani kwa wanywaji zinapowafanya kuwadhaifu kwa majukumu ya jumatatu kazini. Wewe nishahidi mara ngapi Jumatatu tunakuta ofisi za watu zimechelewa kufunguliwa kisa jamaa hajafika mapema na sababu kuu ni “hangover” vijihisia vya kilevilevi baada ya kunywa siku iliyopita. Au wengine unawakuta ofisini lakini anavyokuangalia unajua kabisa anahitaji kupumzika na mara nyingine hata harufu ya ofisi inatosha kukwambia kuwa lipo tatizo sehemu.

Labda tuangalie mfano wa mwisho! Je umewahi kuona muuza duka amekaa nje akisoma gazeti au akiongea na jamaa zake na mteja anapofika anaanza kumuuliza “unataka nini” angali akiwa nje ya duka bado. Mara nyingine unakuta amekamatwa na maongezi matamu ambayo wenzake wasio na kazi wanaamua kuja kuyaongelea katika eneo lake la kazi, au yamkini sio maongezi bali ni mchezo fulani kama vile bao, karata, draft au pooltable na anaona shida kabisa kuacha mtiririko wa mchezo aende kumhudumia mteja.

Hizi na nyingine nyingi ni baadhi ya tabia zinazoonekana katika maeneo yetu ya kazi na ambazo ni vigumu sana kuzisikia kwa wenzetu wa nchi zilizo endelea.

Swali ni je? Umeshapata muda wa kufikiri ni muda wa thamani kiasi gani unapotezwa na wafanyakazi kizembe? Je, umeshawahi kufikiri faida ya muda uliopotea au unaopotea katika mtazamo wa kifedha? Umeshawahi kuwaza jinsi ambavyo kwa tabia hizi itatuchukua maelfu ya miaka tukiota mafanikio ambayo hatutakaa tuyaone?

Kama umewahi kuyawaza haya na je, unajiweka katika nafasi gani katika kujaribu kuleta mabadiliko?

Tunamaanisha nini katika suala zima la maadili ya kazi? Hapa tunaangalia jinsi nzima ya utendaji, mahusiano yetu na waanyakazi wenzetu, wafanyabiashara wenzetu, wajasiriamali wenzetu, na mahusiano yetu na wateja au wale wanaopokea huduma zetu.

Yapo maadili na kanuni mbalimbali za kiutendaji kutofautiana na maeneo ya kazi, baadhi ya maadili hayo ni kama vile;

•Kuweka mazingira ya kufanyiakazi safi na salama kwa ajili yako wewe mfanyakazi mwenyewe na kwa ajili ya wafanyakazi wengine. Kuna wengine sehemu anakofanyia kazi anapajua na kupaweza peke yake, kwa jinsi palivyo kaakaa hata asipokuwepo yeye hakuna atakayeweza kufanya kitu katika meza yake. Hii siyo sawa na siyo maadili mazuri.

•Kuwaheshimu na kuwachukulia vyema wafanyakazi wenzako na wewe binafsi.

•Kutoa maslahi sawa na ya haki kwa mpokea huduma yeyote. Epuka dhuluma.

•Kushughulikia mambo yote yanayohusu biashara yako au kazi yako kwa ukweli, uwazi na uaminifu. Bahati mbaya hali imebadilika sana siku hizi, ukiwa mwaminifu sana makazini watu wanakushangaa, wanakuona kituko. Kwenye suala la kuyalinda na kuyaheshimu maadili lazima kukubali kuonekana kituko. Kumbuka ni kwa faida yako pia.

Baadhi ya Maadili yanayomlenga mfanyakazi

•Fika katika eneo la kazi kwa muda muafaka (mapema) na pia utoke kwa muda muafaka.

•Fanya kila kinachoihusu ajira yako au kampuni yako katika kila sekunde unayokuwa katika eneno la kazi, usihamishie ya nyumbani au mtaani kazini.

• Tunza mali na vitu vingine vya ofisi au kampuni kwa uangalifu mkubwa na kwa kuvipenda kama vile ni vyako. Hapa tunaweza kuona siri ya magari ya serikali au makampuni ya uma kuwa juu ya mawe au yaliyo choka.

•Heshimu kampuni au ofisi yako kwa kuwa mwaminifu na mkweli, mtu awaye yeyote asikuhofie chochote katika nafasi yako. Mfano kusiwepo mazingira ya rushwa au upendeleo katika eneo lako.

Maadili ni suala la uchaguzi binafsi na kwa hiyo, jinsi maadili ya sehemu ya kazi yanavyochukuliwa au kufuatwa inategemea sana na jinsi maadili binafsi aliyonayo mfanyakazi au mfanyabiashara. Kama tuna maadili yetu binafsi na tunayaheshimu na kuyafuata inakuwa rahisi kuyafuata pia maadili ya kazi tunazozifanya.

Ni ngumu kufuata utaratibu uliowekewa au mliowekeana wakati hata ule wa maisha yako binafsi unakushinda. Mtazamo mkubwa wa ulimwengu wa leo kuhusiana na maadili ya kazi ni kwamba, kosa kubwa unaloweza kufanya katika utendaji wa yote yasiyo haki katika eneo la kazi ni kukamatwa.

Utasikia watu wakisema “ameshikwa kizembe sana” wakimaanisha “ameiba kizembe” angeweza kuiba kistaarabu. Juhudi kubwa sasa imewekwa katika kuzishtukia na kuzigundua mbinu za mwajiri au bosi au mashirika ya uchunguzi kama vile Takukuru na wakaguzi wa mahesabu, na kutafuta mianya ya kuwakwepa. Ni vema tukafahamu maishani kuwa maendeleo na mafanikio yetu binafsi yanaakisiwa na maadili ya kiutendaji tuliyonayo katika maeneo yetu ya kazi. Kumbuka Mabadiliko ya kweli huanzia kwa mtu binafsi