Bajeti ijayo inahitaji sera za kodi za kupanua uchumi

Muktasari:

  • Ni muhimu kwa wananchi kufuatilia mijadala hii kwa sababu inawahusu moja kwa moja. Pamoja na mambo mengine, bajeti ya Serikali ni mkakati wa makusanyo na matumizi ya fedha za walipa kodi ambao ni wananchi. Inahusu maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali.

Kati ya Aprili na Juni ya kila mwaka nchini huwa ni muda wa mjadala wa bajeti. Pamoja na mambo mengine, Bunge linakaa na kujadili bajeti za wizara mbalimbali kabla ya bajeti kuu kusomwa na kuanza kutumika mwaka mpya wa fedha unapoanza kila Julai Mosi.

Ni muhimu kwa wananchi kufuatilia mijadala hii kwa sababu inawahusu moja kwa moja. Pamoja na mambo mengine, bajeti ya Serikali ni mkakati wa makusanyo na matumizi ya fedha za walipa kodi ambao ni wananchi. Inahusu maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali.

Ni muhimu kuelewa kwa ujumla wake ni mambo gani hujitokeza katika mijadala ya bajeti zetu. Wananchi wanapaswa kufahamu vipaumbele vilivyopo kwa mwaka wa fedha unaofuata na namna vitakavyotekelezwa. Katika makala haya msisitizo unawekwa katika sera za kikodi za kupanua uchumi kwenye bajeti ijayo.

Bajeti

Katika lugha rahisi, bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi kwa kipindi au shughuli fulani maalumu. Bajeti ya Serikali ni makadirio ya mapato na matumizi ya; kwa mwaka wa fedha ambao kwa Tanzania huanza rasmi Julai.

Serikali huwasilisha makadirio ya mapato yake kwa kuonyesha fedha zitakazotoka katika vyanzo mbalimbali kama vile kodi, tozo, ushuru, mikopo na misaada kutoka kwa wahisani wa maendeleo.

Pia, huonyesha fedha hizi zitatumika katika maeneo gani kugharamia bidhaa na huduma za umma. Sera za kikodi ni muhimu katika bajeti kama itakavyofafanuliwa kwenye makala haya.

Kodi

Bajeti ya Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine nyingi, hugharamiwa kwa vyanzo mbalimbali vya fedha. Hivi ni pamoja na vile vya ndani na vya nje ya nchi. Vyanzo vya nje ni mikopo na misaada kutoka sehemu na wadau mbalimbali.

Vyanzo vya ndani vya fedha za bajeti ni pamoja na vya kikodi na visivyo vya kikodi. Vyanzo vya kikodi hutokana na kodi mbalimbali zinazotozwa. Kodi hizi ni pamoja na ile ya Ongezeko la Thamani (Vat), ambayo ni asilimia 18 ya thamani ya bidhaa na huduma husika.

Nyingine ni kodi ya zuio inayotozwa katika muktadha tofauti ikiwamo ushauri elekezi. Wataalamu wa ndani hulipa asilimia tano ya mkataba na wa nje hulipa asilimia 15. Kodi nyingine ni ya mapato ya kampuni ambayo ni asilimia 30. Zipo kodi nyingi nyingine katika bidhaa na huduma.

Sera ya kodi

Licha ya mambo mengine, mapato ya kodi huongozwa na sera kwa bajeti husika. Sera hizi hutajwa na waziri wa fedha katika mwongozo wa bajeti na hata pale anaposoma bajeti kuu.

Kama ilivyo kwa sera nyingine, sera za kodi hutoa mwongozo wa nini kifanyike kwa mwaka na bajeti husika. Lengo la sera za kodi ni kuonyesha mwelekeo, matamanio, mipango, malengo na njia ambayo Serikali itakusanya fedha kutoka katika vyanzo vya kodi kwa mwaka husika wa fedha.

Sera za kodi huweza kuwa na sura na athari kadhaa kutegemeana na nia ya Serikali na hali halisi ya uchumi. Sera za kodi huweza kuchochea kupanua uchumi au kuufanya usinyae kulingana na vile vitakavyotungwa na kutumika ndani ya muda huo. Yote haya hutegemea sera gani Serikali imeamua kuzitumia.

Sera za kupanua uchumi

Sera za kodi za kupanua uchumi hulenga kuleta ahueni kwa walipa kodi. Sera hizi huchochea shughuli za uchumi za uzalishaji bidhaa na huduma. Hizi ni sera zenye kodi chache, au viwango vya chini vya kodi au yote mawili.

Maana yake, ni kuwa fedha nyingi zaidi huachwa mikononi mwa walipakodi ambao ni kampuni, taasisi na mtu mmoja mmoja. Fedha nyingi zaidi zinapobaki mikononi hupaswa kuchochea shughuli za uchumi na biashara.

Kwa kampuni kwa mfano, kodi ndogo baada ya faida hubakiza fedha nyingi zaidi inayoweza kutumika kwenye maeneo mengine ya kipaumbele kwa taasisi husika. Fedha hizi huweza kuwekezwa kwenye miradi mipya au kupanua iliyopo.

Kwa upande wa wananchi, kodi inapokuwa ndogo maana yake wanabakiwa na fedha zaidi ambazo huwezesha matumizi, akiba na pengine uwekezaji. Kodi ndogo inapowezesha matumizi zaidi, huchochea uwekezaji, ajira, kipato, mauzo na hatimaye ustawi zaidi wa uchumi.

Sera za kubana uchumi

Kinyume cha kupanua ni kubana uchumi. Sera za kikodi za kubana uchumi huwa na kodi nyingi na viwango vya juu. Utitiri wa kodi na viwango vya juu vya kodi siyo afya kwa uchocheaji wa uchumi na biashara.

Kodi nyingi na viwango vikubwa vinavyotozwa kwa walipaji hupunguza uwezo na utayari wa kampuni kuwekeza, kuzalisha na kuajiri. Hivyo, kuwa changamoto kwa walio katika biashara kupanua shughuli zao na wanaotaka kuanzisha biashara mpya.

Kodi nyingi zenye viwango vikubwa hupunguza utayari na uwezo wa wananchi kutumia bidhaa na huduma, kuweka akiba hata kuwekeza. Hivyo sera za kodi za kubana uchumi au kwa kukusudia au kwa kutokusudia huathiri ustawi wa uchumi.

Sera pana za kodi

Kwa kutizama mazingira ya kiuchumi na biashara kwa miaka ya karibuni hasa mwaka 2016/17, sera za kupanua uchumi zitakuwa rafiki zaidi dhidi ya zile za kubana uchumi nchini.

Tupo katika hali ambayo biashara zimekuwa zikisuasua kwa sababu kadhaa wa kadhaa. Kwa baadhi ya sekta, hasara imekuwa kubwa, faida imepungua, biashara zimefungwa, biashara zimeshindwa kulipa madeni katika taasisi za fedha, upatikanaji wa mikopo umekuwa tatizo na mitaji imekata katika baadhi ya biashara.

Kwa kaya na mtu mmoja mmoja gharama za maisha zimepanda na ugumu wa kulipa bidhaa na huduma ni dhahiri. Katika mazingira ya namna hii kitaalamu mwitikio wa kisera hasa za kodi ni kuwa na sera za kupanua badala ya kubana uchumi.

Changamoto

Pamoja na mahitaji ya wazi ya kuwa na sera za kupanua uchumi, changamoto kadhaa zitajitokeza. Sera hizi huweza kupunguza mapato kwa muda mfupi na wa kati. Hii ni changamoto kwa kuzingatia Serikali inataka kugharamia bidhaa na huduma nyingi za umma.

Pia, wanasiasa wanataka kuonekana wakitimiza ahadi walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi. Pamoja na changamoto hizi, ukweli ni kwamba sera za kupanua uchumi katika bajeti ya 2017/18 zitaimarisha uchumi na biashara kuliko zile za kubana.