Bashe: Nimekusudia kuleta mabadiliko Nzega mjini

Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe

Muktasari:

  • Historia inaonyesha kuwa mbunge huyo hana historia ya kukata tamaa na ikiwa ataamua kufanya jambo ambalo anaamini ni zuri husimamia hadi mwisho.
  • Ni mbunge aliyefanikiwa kuthibitisha kwamba anasoma makabrasha wanayopewa bungeni na anao ufahamu mpana na anajua kwa nini wananchi wa jimbo hilo wamemchagua ili awawakilishe.

Kama ukitakiwa kuwataja wabunge vijana machachari na waliofanikiwa kuonyesha uwezo wa kusimamia hoja bungeni, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe hawezi kukosekana.

Historia inaonyesha kuwa mbunge huyo hana historia ya kukata tamaa na ikiwa ataamua kufanya jambo ambalo anaamini ni zuri husimamia hadi mwisho.

Ni mbunge aliyefanikiwa kuthibitisha kwamba anasoma makabrasha wanayopewa bungeni na anao ufahamu mpana na anajua kwa nini wananchi wa jimbo hilo wamemchagua ili awawakilishe.

Uwezo wake wa kusimamia hoja vimemfanya ang’are na hivyo kuungwa mkono na wenzake.

Kwa wasiomjua, jina la mbunge huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) lilisikika zaidi wakati alipoenguliwa katika uchaguzi wa ndani ya CCM mwaka 2010, licha ya kushika nafasi ya kwanza kwenye kura za maoni.

Hakukata tamaa kwani mwaka 2015, alirusha tena karata yake kwa kuamua kugombea ubunge na safari hiyo aliibuka mshindi katika kura za maoni na baadaye jina lake kupitishwa na chama chake kisha kupigiwa kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Miongoni mwa vitu vilivyompaisha hasa wakati wa Bunge la Bajeti ni hatua yake ya kumbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa kupeleka jedwari la marekebisho la kuondoa ongezeko la kodi katika magari, bodaboda na mitumba katika Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu, Bashe anasema kipaumbele chake kikubwa jimboni ni kuboresha sekta ya elimu, afya, miundombinu, biashara na nyingine ili kukuza maendeleo ya wananchi.

Anaamini kwamba wananchi wakiwa na afya bora, elimu na miundombinu mizuri wanaweza kufanikiwa kiuchumi.

Kazi zake jimboni

Bashe ameshaanza kutekeleza ahadi zake katika sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu, afya, miundombinu na huduma nyingine muhimu za jamii ambazo wananchi wa jimbo hilo wanazihitaji.

Mara baada ya kuchaguliwa, alifanya ziara ya ghafla katika hospitali ya Nzega na kubaini upungufu mkubwa wa vifaa tiba ikiwa ni pamoja na vya kujifungulia.

Kutokana na kero alizokutana nazo, amefanikiwa kuchukua hatua kadhaa miongoni mwake ni kupiga marufuku hospitali hiyo kutoza ushuru wa Sh200 kwa wananchi wanaoegesha baiskeli zao pindi wanapoingia ndani baada ya kupewa malalamiko.

Anasema katika kipindi kifupi cha uongozi wake kwenye Jimbo la Nzega, amekamilisha ujenzi wa zahanati Kata ya Nhobola ili kuwasogezea wananchi wa kata hiyo huduma za afya.

“Wananchi walikuwa wakiteseka kupata huduma za afya, kukamilika kwa zahanati hii kutawasaidia sana,” anasema.

Anasema wapo kwenye ujenzi wa nyumba ya mganga ambayo inatarajia kukamilika wakati wowote.

Hata hivyo, anasema kuwa kupitia Wizara ya Afya jimbo hilo limepata msaada wa gari linaloongeza ufanisi katika utoaji huduma za afya kwa wananchi wake.

Anaeleza kuwa anaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya kuhakikisha kuwa kila kijiji kinapata zahanati, huku kata zikiwa na vituo vya afya.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Bashe anasema anaamini kuwa hakuna maendeleo ya kweli ikiwa wananchi hawatakuwa na elimu ya kutosha.

Anasema tayari amefanikisha ujenzi wa vyumba 13 vya madarasa katika shule za msingi na sekondari ambazo zilikuwa na upungufu.

“Tangu nimeingia kipaumbele changu kingine ni kwenye elimu, uhakika wa madarasa ya wanafunzi kujifunzia yanaongeza ubora wa elimu kwenye jimbo langu. Japo tumeshajenga vyumba 13, bado ujenzi unaendelea,” anasema.

Kwa upande wa kidato cha tano na sita, anasema amefanikiwa kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili na bweni la kutosha wanafunzi 48 katika Shule ya Sekondari Bulunde.

Anasema ikiwa wanafunzi wataandaliwa mazingira mazuri ya elimu wanaweza kufanya vizuri kwenye mitihani yao jambo ambalo, anaendelea kulisimamia kwa ukaribu.

Anasema mkakati wake ni kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo wanapata huduma za maji safi na salama na kwamba katika utekelezaji, tayari wamechimba visima virefu sita.

Anaongeza kuwa wakati Rais John Magufuli alipopita kwenye jimbo hilo, alimwomba mradi wa maji katika mji wa Nzega na kwamba tayari wamepatiwa zaidi ya Sh200 milioni na hivyo mradi umeanza kujengwa.

“Kukamilika kwa mradi huu kutawawezesha wananchi wa mji wa Nzega kupata uhakika wa maji,” anasema.

Miradi mingine aliyoahidi na kuanza kutekelezwa ni ujenzi wa kituo cha mabasi cha mjini Nzega ambacho kimekamilika kwa asilimia 70 kikijengwa kupitia halmashauri.

Anasema kituo cha mabasi ni kati ya maendeleo yanayosaidia kukua kwa uchumi wa jimbo hilo ambalo linahitaji kuboreshwa.

“Niliahidi kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa kituo hiki na kwa uhakika nimefanikiwa kwa asilimia 70. Naendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa tunakamilisha ujenzi wake,” anasisitiza.

Ujasiriamali

Bashe anasema moja ya maeneo yanayosaidia kuongeza kipato kwa wananchi ni ujasiriamali.

Anasema mkakati mkubwa anaoufanya kwenye jimbo hilo ni kuhamasisha wananchi kuanzisha vikundi vya kiuchumi na kuvisajili ili iwe rahisi kupewa fursa pale zinazopotokea ikiwamo mikopo ya gharama naafuu.

Tayari vikundi 40 vya wananchi wa jimbo hilo vimekopeshwa fedha kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Anasema kupitia ofisi yake wametoa mkopo wa Sh20 milioni kwa ajili ya kuwakopesha wananchi hao huku kampuni ya simu ya Aitel nao wakitoa Sh20 milioni.

“Kwa hiyo ikiwa wananchi watatumia fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa wanawake watafanikiwa kiuchumi,” anasisitiza.

Madini

Mbunge huyo kijana anasema wachimbaji wadogo wa jimbo lake wanatarajia kukabidhiwa eneo namba saba kwa ajili ya machimbo ikiwa ni moja ya ahadi zake, wakati akiwania ubunge.

Aidha, anasema wapo katika hatua za mwisho katika mchakato wa kurudisha uwanja wa ndege kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo.

Changamoto zilizopo jimbo

Anazitaja changamoto zinazolikabili jimbo lake kuwa ni pamona na ubovu wa miundombinu, uhaba wa maji na umeme.

Hata hivyo, anasema changamoto hizo zinaendelea kutatuliwa ikiwamo ya umeme ambayo tayari vijiji vyote 43 vya wilaya yake vimeingizwa katika Mradi wa Nishati Vijijini (Rea) awamu ya tatu.

Hata hivyo, ana uhakika kuwa changamoto hizo zitamalizika ikiwa, kila mmoja atatimiza wajibu wake ipasavyo.

Nje ya ubunge

Mbali na utumishi wake kwa wananchi, Bashe ni miongoni mwa viongozi wa Kampuni ya New Habari Corporation.

Anasema amefanikiwa kutekeleza majukumu yake yote bila wasiwasi kutokana na kuugawa muda wake vilivyo.

Anabainisha kuwa kipindi cha kuwapo bungeni anajitahidi kuhakikisha hakosi ratiba yoyote ili aweze kutimiza wajibu wake wa msingi kikatiba wa kuwatumikia wananchi.

“Naugawa muda wangu vilivyo, asilimia 30 ya muda wangu kwa mwaka nakuwa bungeni, asilimia 40 nakuwa jimboni na muda unaobaki ni kwa ajili ya kazi zangu na familia pia,”anasema.